Friday, January 4, 2013

SHELUKINDO : Namuunga mkono lowassa 2015

MBUNGE wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo ametangaza kuchukua kile alichokiita uamuzi mgumu ili kuhakikisha kuwa Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa anamrithi Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.Shelukindo alitoa kauli hiyo Jumapili wakati akiwasalimia wakazi wa Monduli baada ya kukaribishwa kuchangia ujenzi wa Hosteli ya KKKT katika sherehe za kukaribisha Mwaka Mpya zilizofanyika nyumbani kwa Lowassa ambazo pia zilihudhuriwa na makada kadhaa wa CCM.

Jana alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, Shelukindo alisema: “Ni kweli mimi ni muumini wa Lowassa, ila pale (mkutanoni) sikumtaja kwa sababu najua chama kina taratibu zake na muda wa mchakato wa kumpata Rais haujafika.”

“Niliposimama niliwaeleza kuwa nisingeweza kuchangia fedha nyingi kwa sababu watu wangu wana njaa huko Kilindi. Pia kule (Kilindi) tunaendesha harambee ya aina hiyohiyo. Ila nikawaambia zawadi yangu kwa Wanamonduli ni kufanya uamuzi mgumu ili mwaka 2015 apatikane Rais mzalendo na anayeweza kufanya uamuzi mgumu na kwa wakati.”

Shelukindo aliendelea: “Niliposema hivyo, umati uliibuka kwa shangwe na kunitaka nimtaje nitakayeshirikiana naye, lakini nikawaambia kuwa huu si wakati mwafaka ila baadaye nilichangia Sh500,000.”

Shelukindo alisema harambee hiyo ilitarajiwa kuchangishwa Sh100 milioni lakini zikapatikana Sh70 milioni.

Mbali na Shelukindo, makada wengine wa CCM waliohudhuria sherehe hizo ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mngeja.

Awali, akizungumza katika sherehe hizo, Lowassa aliwataka Watanzania kutumia mwaka huu wa 2013 kufanya uamuzi mgumu katika kila changamoto inayowakabili.

“Salamu zangu za Mwaka Mpya kwa Watanzania: Nawaomba wapitishe uamuzi mgumu kwa kila changamoto watakazokabiliana nazo,” alisema. Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na umaskini na kuongeza kuwa mtu akiamua inawezekana.

Lowassa aliwahi kusema bungeni akiitaka Serikali kuwa na tabia ya kupitisha ‘uamuzi mgumu’ katika kuwaondolea wananchi kero akisema bila kuthubutu ni vigumu kukabiliana na changamoto.

Katika sherehe hizo, Lowassa pia alizungumzia taarifa zilizozagaa mitandaoni kuwa sherehe yake hiyo ilikuwa ni ya kisiasa akisema: “Wameandika katika mitandao ya kijamii kuwa kuna sherehe kubwa ya kisiasa. Mimi nawaambia wa waache porojo hizo. Nimekuwa nikiandaa sherehe hizi tangu mwaka 1995, wao wakitaka waige mfano huu.”

Chanzo MWANANCHI

No comments: