Wednesday, April 3, 2013

RAIS KIKWETE AELEZA ALIVYOOMBEWA DUA NA WAISLAMU ILI AFE.....

                                                Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’ amelilipua kundi dogo la Waislam waliowahi kumsomea Itikafu ili yeye na viongozi wawili wa serikali wafe kwa kile kilichodaiwa na kundi hilo kwamba, wamekuwa wakiiangamiza dini yao.

Hayo yalisemwa na JK mwenyewe katika hotuba aliyoitoa ikulu Machi 31, 2013 ambayo ni utaratibu aliojiwekea wa kuwahutubia Watanzania kila mwisho wa mwezi.

JK alikuwa akijibu tuhuma zinazoelekezwa kwake kutoka pande zote za dini ya Kiislam na Kikristo kwamba amekuwa akipendelea upande mwingine.

Akizungumza bila kumung’unya maneno lakini katika hali iliyoonesha kusikitishwa na madai hayo, JK alisema:
“Ndugu wananchi, nyaraka na kauli kalikali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislam zinanishawishi kuamini haya niyasemayo. Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili makuu.

“Kwanza, kwamba kila upande unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi ya dini yake. Kauli na mihadhara ya kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya mambo yanayotolewa mifano.

“Na pili kwamba, kila upande unailaumu serikali kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na serikali haichukui hatua.  Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao kuuawa na Waislam lakini serikali haichukui hatua. 

“Kwa ajili hiyo wanadai kuwa serikali imeshindwa kulinda uhai wa raia wake. Wanasema pia kwamba serikali inapendelea upande wa Waislam.

“Waislam nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na serikali haichukui hatua yoyote ya maana. Waislam wananyanyaswa katika nchi yao, wanakamatwa hovyo, hawapewi fursa sawa, na kwamba serikali inawapendelea Wakristo.

“Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi shughuli za Wakristo kuliko za Waislam kama vile harambee za kujenga makanisa na shule za makanisa. Naambiwa kuwa mwepesi kushiriki maziko ya maaskofu kuliko mashehe wanapofariki dunia.

“Ipo misikiti mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife.  Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.

“Ndugu wananchi, napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wowote.  Hatufurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislam na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati mbalimbali,” alisema JK bila kuitaja misikiti hiyo.

Hata hivyo, kuna madai kwamba, misikiti hiyo, mmoja upo Temeke, miwili ipo Kariakoo ambapo waumini wake wamewahi kukesha kwa ajili ya dua ya Itikafu kwa viongozi hao jambo ambalo rais amekanusha kuangamiza imani yoyote nchini.

No comments: