HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO
(MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013______________________
I. UTANGULIZIMheshimiwa Spika,
kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya Upinzani
kuhusu Bajeti ya Nchi ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni
za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007.Mheshimiwa Spika, Natoa
pongezi za dhati kabisa kwa Ndugu William Augustao Mgimwa, Mbunge wa
Jimbo la Kalenga mkaoni Iringa kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri wa
Fedha na Uchumi. Vile vile nawapongeza Ndugu Saada Mkuya na Ndugu Janeth
Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge na baadaye kuwa Manaibu Mawaziri
katika Wizara hii nyeti sana. Ninawapa pole pia maana Wizara ya Fedha
sio Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea kuisimamia Wizara hii
kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka miwili
iliyopita. Mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi,
mtakapoharibu tutawawajibisha.Mheshimiwa Spika, Ni
dhahiri kwamba Mwaka wa Fedha uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa
Watanzania. Ni mwaka ambao gharama za maisha zilipanda kwa kasi kubwa
sana na
juhudi za Serikali kuwakwamua wananchi na hasa wananchi wanyonge kutoka
kwenye lindi la ufukara ziligonga mwamba. Kambi ya Upinzani inawapa
pole Watanzania kwani hili ndilo walilochagua. Muhimu ni kuvumilia mpaka
uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko ya Serikali ili kuweka Serikali
itakayoongozwa na CHADEMA na itakayoweza kukabili changamoto za sasa na
za baadaye. Mheshimiwa Spika, naomba tufanye mapitio kidogo ya Bajeti inayomaliza muda wake.
- UTEKELEZAJI WA BAJETI ILIYOPITA
Mheshimiwa Spika,
kabla ya kutoa bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani ni vema kufanya
tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopita ili kuona ni kwa
namna gani Serikali inathamini fedha za walipa kodi, na dhamira yake ya
kuleta maendeleo ya kiuchumi katika Taifa. Katika kufanya hivyo,
tutapitia baadhi ya maeneo ambayo Kambi ya Upinzani tunaona kuwa
hayakutekelezwa katika bajeti iliyopita.Kupunguza Makali ya MaishaMheshimiwa Spika,
Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilitangaza nia yake ya
kupunguza makali ya maisha. Hatua mbali mbali zilichukuliwa ikiwamo
kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya Dizeli na Petroli, kuanza
kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula
kwa Wakala wa Chakula. Serikali ilitumia shilingi bilioni 296 na dola za
Marekani milioni 183 kwenye Umeme. Vilevile Serikali ilitumia shilingi
bilioni 27 kununua Mahindi na kusambaza kwenye masoko. Mheshimiwa Spika, licha
ya hatua hizo zilizochukuliwa Mfumuko wa Bei uliongezeka maradufu
kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia
17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la kupunguza
makali ya maisha kwa wananchi. Sio tu kwamba Serikali imeshindwa
kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua za
Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha.Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani Bungeni katika Hotuba yake mbadala ya mwaka 2011/12
iliitaka Serikali kushughulikia msingi wa mfumuko wa Bei hapa nchini
ambao ni uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula. Tumeelezwa na Waziri
Kivuli wa Mipango na Uchumi kwamba Chakula peke yake ni asilimia 48 ya
kapu la bidhaa na huduma ambazo mwanachi anatumia. Mfumuko wa Bei ya
Chakula kinacholiwa nyumbani na kwenye migahawa ilikuwa asilimia 25
mwezi Aprili 2012 (BoT monthly Economic Review, May 2012). Vile vile
mfumuko wa bei wa nishati inayotumika nyumbani na mafuta ya Dizeli na
Petroli ulifikia asilimia 25 pia mwezi Mei mwaka 2012. Ni dhahiri kwamba
iwapo tutadhibiti mfumuko wa bei ya chakula tutaweza kushusha mfumuko
wa bei kurudi kwenye tarakimu moja.Mheshimiwa Spika,
Serikali inapendekeza hatua zilezile ilizofanya mwaka wa fedha
unaokwisha kwa kutoa vibali kwa Wafanyabiashara vya kuagiza Mchele na
Sukari. Katika hotuba yake Waziri wa Fedha anasema ‘….Serikali ilitoa
vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani
200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya Sukari…’(uk 9
ibara ya 15). Baada ya hatua hii bei ya Sukari ilipanda kutoka tshs 1700
mpaka tshs 2800 kwenye maeneo mengi nchini. Waziri wa Fedha katika
hotuba yake anatoa suluhisho. Ninanukuu. ‘…hatua za haraka ambazo
Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa Sukari na
mchele kutoka nje….’! Serikali inachukua hatua zilezile kwa tatizo lile
lile ikitegemea matokeo tofauti.Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea pendekezo lake la mwaka jana
kwa Serikali kutoa vivutio kwa wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa
wingi. Miongoni mwa vivutio hivyo ni: i. Kuwekeza kwenye barabara za vijijini ili mazao yao yafike kwenye masoko na kupata bei nzuri, ii. Kuwekeza
kwenye Usambazaji wa Maji vijijini ili kina mama wasitembee mwendo
mrefu kutafuta maji na hivyo kutumia muda mwingi kwenye uzalishaji, iii. Kuwekeza kwenye Umeme vijijini ili wafanyabiashara wa vijijini waongeze thamani ya mazao.Kwa mfano, kuuza Unga badala ya Mahindi. iv. Kuwekeza kwenye miundombinu ya Umwagiliaji vijijini ili wakulima wazalishe muda wote wa mwaka. v. Kuwekeza
kwenye Elimu vijijini na pia Afya vijijini ili wananchi wetu wawe na
Afya bora na waelimike katika mbinu za uzalishaji bora.Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaamini kuwa, hakuna mbadala wa kudhibiti mfumuko wa
bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa wananchi
wetu. Serikali inafikiria uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia wakulima
wakubwa ambao watageuza wananchi wetu kuwa Manamba na vibarua ndani ya
nchi yao. Tuwekeze kwa watu wetu vijijini ili waongeze uzalishaji na kwa
kufanya hivyomfumuko wa Bei ya chakula utakuwa historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula isipokuwa Kilimo.Mhesimiwa Spika,
Tunatambua kuwa hatua tunazotaka Serikali ifanye ni za muda wa kati.
Kwa muda mfupi tunataka Bodi ya Mazao mchanganyiko, Wakala wa Hifadhi ya
Chakula na Bodi ya Sukari zipewe fedha kuagiza Mchele na Sukari na pia
kununua kutoka kwa wakulima na kusagisha Mahindi. Wafanyabiashara
waagizaji wa Chakula washindane na Taasisi hizi za Umma badala ya kuwapa
vibali ambavyo hutolewa kwa rushwa na hivyo kuongeza bei za bidhaa
hizo. Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira.Mheshimiwa Spika,
Serikali imesema kwamba ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na
tatizo la Ajira kwa kuongeza fursa za ajira. Miongoni mwa hatua
zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza mitaji katika Benki ya Rasilimali,
Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp. Pia Serikali
imetangaza kwamba imeajiri walimu, maafisa ugani na watumishi wa Afya.
Hatua kama hizi pia zimetangazwa kwa mwaka wa Fedha wa 2012/13 ambapo
pia Serikali imetangaza kuajiri watumishi 71,756.Mheshimiwa Spika,
Duniani kote Serikali haizalishi ajira bali ajira huzalishwa na Uchumi
mzima ambapo Serikali ni sehemu tu ya Uchumi (Jobs are created by an
economy). Takwimu zinaonyesha kwamba kila mwaka Tanzania inaingiza
kwenye soko la Ajira watu takribani laki saba. Shughuli za Uchumi
zikiongezeka ndio Ajira zinatengenezwa. Serikali inafikiria nini kuhusu
vijana takribani milioni nane walio shule za Msingi hivi sasa, Vijana
milioni 1.7 walio katika Shule za Sekondari hivi sasa, Vijana 200,000
waliopo vyuo vya Ufundi na Wanachuo 180,000 walio katika Vyuo vya Elimu
ya Juu (takwimu kutoka kitabu cha hali ya uchumi, 2012 sura ya 19).
Serikali ambayo bado inategemea takwimu za Ajira za Mwaka 2006
inajitamba kwa kuajiri watu 70,000. Mheshimiwa Spika,
Jukumu la Serikali ni kujenga mazingira ya wananchi kupata ajira ama
kwa kujiajiri au kwa kuajiriwa na shughuli za uchumi. Lakini ukweli ni
kwamba Serikali imeshindwa kushughulikia tatizo la Ajira na hasa ajira
kwa vijana. Tatizo la Ajira kwa Vijana ni Bomu litakalokuja kutulipukia
vibaya sana kama hatutakuwa makini nalo. Hii ni nchi ya Vijana.
Kutoshughulikia masuala yao ni kutoshughulikia masuala ya nchi.Mheshimiwa Spika,
changamoto ya ajira kwa vijana Bajeti mbadala imeiwekea mikakati mipana
ya kiuchumi kwa kuanzisha miradi mikubwa ya Umma itakayomeza vijana
waliopo mtaani na kuanzisha kwa makusudi na kwa kasi Vyuo vya Ufundi
stadi na Vyuo vya Ufundi na Mafunzo vingi. Kambi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza Uwekezaji wa Miundombinu Vijijini kama njia ya kupunguza
tatizo la ajira kwa vijana. Vilevile tunapendekeza Miradi mikubwa ya
kuongeza mazao ya Kilimo hasa Pamba, Korosho na Katani ili kupanua
Ajira. Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kujenga VETA katika kila
Halmashauri ya Wilaya na Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa ili kutoa
ujuzi kwa vijana ili waweze kukabili maisha yao. Badala ya Serikali
kukopa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida, Serikali ikope kujenga Vyuo vya
Ufundi Stadi na vyuo vya Ufundi na Mafunzo. Ni Lazima viongozi sio tu
tuwe makini bali tuonekane kuwa makini tunaposhughulikia suala la Ajira
kwa Vijana.Sera ya MapatoMheshimiwa Spika, Kambi
ya Upinzani Bungeni ilitangaza vipaumbele katika sera ya Mapato ambavyo
ni pamoja na kukusanya Mapato ya Serikali mpaka zaidi ya asilimia 20 ya
Pato la Taifa ili kuwezesha kujitegemea kupata fedha za miradi ya
maendeleo. Pia Kambi ya Upinzani inakusudia kufanya marekebisho
mbalimbali ya sharia za kodi ili kulinda viwanda vya ndani vinavyotumia
malighafi za kilimo na mifugo za hapa nchini, kupanua wigo wa Mapato kwa
kutunga sheria ya kulazimu kila Mtanzania kujaza fomu za marejesho ya
kodi na kurekebisha viwango vya kodi ya Mapato (PAYE). Vile vile
tunapendekeza kufanya marekebisho ya sheria za kodi kwenye sekta za
madini na mawasiliano ili kuongeza mapato ya Serikali.Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa Fedha 2011/12 Serikali ilichukua hatua mbalimbali
katika masuala ya Kodi. Katika Bajeti mbadala pia tulipendekeza hatua
mbali mbali ambazo tuliona zitaongeza mapato ya Serikali na hivyo
kutuwezesha kuendeleza nchi yetu. Baadhi ya hatua mbalimbali
tulizopendekeza Serikali imetangaza kuzitekeleza.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika Bajeti Mbadala ya mwaka
2011/12 ilipendekeza masuala yafutayo ili kuongeza mapato ya Serikali.
- Hatua
zifuatazo zilipendekezwa ili kuweza kukabiliana na ukwepaji wa kodi
unaofanywa na makampuni makubwa ya kimataifa (Multinational
Corporations) na hatimaye kulipunguzia taifa mapato:
(i) Kutunga
sheria kwa kuimarisha zaidi sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004
kwamba, mikopo ya makampuni kwenye uwekezaji, kwa sababu za kikodi,
isizidi asilimia 70 ya mtaji wote uliowekezwa na hii ianze mara moja
bila kujali mikataba iliyopo.(ii) Kutunga
sheria kuhakikisha kwamba riba kwenye mikopo kutoka Makampuni
yanayohusiana (sister companies) haitaondolewa kwenye kutoza kodi (not
tax deductible). (iii) Kuhakikisha
kwamba mauziano ya Kampuni yoyote ambayo mali zake zipo Tanzania
yanatozwa kodi ya asilimia 30 % kama ‘ongezeko la mtaji’ (‘capital
gains’).Mheshimiwa Spika,
katika mapendezo haya ni pendekezo moja tu ndilo limechukuliwa na
Serikali katika Bajeti ya mwaka 2012/13 nalo ni pendekezo la ‘capital
gains tax’. Hata hivyo Pendekezo la Serikali lina makosa makubwa sana ya
kifundi. Waziri wa Fedha Mhe. Mgimwa amesema, ninanukuu ‘Kuanzisha kodi
itokanayo na uuzaji wa rasilimali ya uwekezaji (capital gains tax)
kwenye uuzaji wa HISA za kampuni mama ya nje ya nchi’Mheshimiwa Spika,
Ukisoma pendekezo letu kwa haraka utaona kama Serikali imelichukua
lilivyo, lakini kwa jicho la kiuchumi pendekezo la Serikali na lile la
Kambi ya Upinzani ni mambo tofauti sana. Pendekezo la Serikali
linazungumzia HISA. Mamlaka ya Mapato Tanzania haitakuwa na mamlaka
(jurisdiction to tax) kutoza kodi kwa Kampuni mama (as a source or even
residence). Mamlaka ya Mapato Tanzania ina mamlaka na Mali (assets)
zilizopo Tanzania za Kampuni mama. Kwa mfano, wakati kampuni ya Barrick
inanunua mgodi wa Bulyanhulu haikuinunua Kampuni ya Kahama mining ltd
bali ilinunua hisa zote za Kampuni ya Sutton Resources. Vile vile,
wakati Zain inanunua Celtel, haikununua Celtel Tanzania ltd bali Celtel
Africa BV ambayo ilikuwa inamiliki Celtel Tanzania BV ambayo ilimiliki
Celtel Tanzania ltd. Hivyo hivyo ilikuwa kwa AirTel ilipoinunua Zain. Kukwepa
mitego hii ya Mashirika ya Kimataifa (MNCs) sheria itaje kwamba Kodi
hii itozwe kwa Mali zilizopo Tanzania na sio kwa HISA kama
alivyopendekeza Waziri wa Fedha. Hata hivyo Kambi ya Upinzani inatambua hatua hiyo ya Serikali kuchukua wazo hili ili kuongeza Mapato ya nchi. Misamaha ya KodiMheshimiwa
Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali iliahidi kupunguza
misamaha ya Kodi mpaka kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa. Ahadi hii
haikutekelezwa na Serikali na badala yake imerejea kuahidi tena. Waziri
wa Fedha ameliambia Bunge katika hotuba yake, nanukuu ‘kuendelea kufanya
mapitio ya sharia mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la
kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo’ (uk.39). Badala ya Serikali
kutuambia hivi sasa misamaha ya kodi imefikia asilimia ngapi, imeendelea
kutoa ahadi isizoweza kutekeleza.Mheshimiwa
Spika, Katika Taarifa ya Utafiti uliofanywa na Jopo la Taasisi za dini
hapa nchini waliyoiita ‘The One Billion Dollar Question’ imeonekana
kwamba Tanzania inapoteza takribani shilingi trilioni 1.7 kutokana na
misamaha ya kodi, ukwepaji wa kodi, utoroshaji wa mitaji nje na
udanganyifu katika biashara ya kimataifa. Fedha hizi ni zaidi ya jumla
ya Bajeti za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Nishati na Madini. Fedha hizi
ni zaidi ya Mkopo ambao Serikali itadhamini kwa TPDC ili kujenga Bomba
la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Fedha hizi zinazopotea
kutokana na misamaha ya kodi ni zaidi ya gharama za Ujenzi wa Gati mpya
katika Bandari ya Dar es Salaam. Kambi ya Upinzani inawapongeza Viongozi
wa Dini kwa kufanya kazi hii nyeti sana lakini tunampongeza zaidi
Mtafiti Mtanzania Dokta Prosper Ngowi kwa kushiriki katika utafiti huu.
Tunaishauri Serikali kusoma Taarifa hii na kutekeleza mapendekezo yake
ili kuongeza mapato ya Serikali. Lugha za kufanya mapitio kila mwaka
hazisaidii, wananchi wanataka kuona misamaha ya kodi imepungua mpaka
kiwango kinachostahili cha asilimia 1 ya Pato la Taifa.Kurekebisha mfumo wa Kodi ya MapatoMheshimiwa Spika,
Bajeti mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza kuifanyia marekebisho
sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004. Tunarejea pendekezo letu na
kuongeza pia kwamba sehemu ya kodi ya Mapato inayotoa fursa
(grandfathering) kwa Kampuni za Madini kutumia sheria ya kodi ya Mapato
iliyofutwa ya mwaka 1973, ifutwe. Pendekezo letu lina lengo la kutaka
kuweka mfumo wa ‘straightline method of depreciation’ ya asilimia 20
badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini hufanya ‘100% depreciation’
kwenye Mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa
‘Corporate Tax’.Mheshimiwa Spika,
Serikali imeamua kupandisha kiwango cha chini cha kipato ili kutoza
kodi ya Mapato (PAYE) kutoka tshs 135,000 mpaka tshs 170,000 bila
kushusha kodi yenyewe. Hii haitamsaidia mwananchi hata kidogo kwani bado
kiwango cha kodi cha asilimia 14 kipo juu sana. Vile vile kiwango cha
chini cha pato litakalotozwa kodi kitawaathiri wafanyakazi wa Serikali
maana ndio ambao Serikali ina mamlaka ya kutangaza kima cha chini cha
Mshahara wao na kuwaacha wafanyakazi wa Sekta Binafsi ambao wengi
hulipwa kiwango kidogo sana cha mishahara. Kimsingi kutokana na tangazo
lake, Waziri wa Fedha ametangaza kima kipya cha chini cha mshahara kuwa
kitakua tshs 170,000. Mheshimiwa Spika,
tunarejea kauli yetu kwamba kupanda kwa gharama za maisha kumepunguza
uwezo wa matumizi ya wananchi walioajiriwa na kulipwa mishahara ambayo
inakatwa kodi (PAYE). Tunapendekeza kwamba PAYE ianzie asilimia 9 kutoka
asilimia 14 na kiwango cha chini cha kutoza kiwe tshs 150,000.
Tunatambua kuwa kodi hii ni chanzo kikubwa cha Mapato kwa Serikali
ambapo kwa mwaka huu wa Fedha kinatarajiwa kuingiza takribani shilingi
bilioni 1,437 (asilimia 18 ya Mapato yote ya kodi yanayokusanywa na TRA)
kutoka Idara ya Kodi za Ndani (Wafanyakazi wa Serikali tshs 115bn,
Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma tshs 47bn na Wafanyakazi wa Sekta
binafsi tshs 312bn) na Idara ya Walipa kodi wakubwa (Wafanyakazi wa
Serikali tshs 450bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma Tshs108bn na
Wafanyakazi wa Sekta Binafsi tshs 406bn). Hata hivyo wananchi
wanapobakia na pesa za matumizi kodi nyingine kama VAT na Ushuru wa
Bidhaa huongezeka na hivyo kupunguza kiwango cha Mapato ya Serikali
ambayo yangepotea kutokana na uamuzi huu. Mheshimiwa Spika,
Hata hivyo bado kuna haja ya kuangalia upya ‘tax brackets’ na
kuzirahisisha kwa kuzipunguza na kuongeza kiwango cha kodi ya Mapato kwa
watu wenye kipato kikubwa zaidi. Mheshimiwa Spika,
ili kuongeza mapato kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa kambi ya
Upinzani inapendekeza mabadiliko katika viwango vya juu vya kodi ya
Mapato ambapo tunapendekeza kupandisha kiwango cha juu kabisa cha
kukokotoa kodi ya mapato (PAYE) kiwe shilingi milioni kumi na kodi iwe
asilimia 42 kutoka asilimia 30 ya sasa. Mheshimiwa Spika,
Tunapendekeza kwamba mtu yeyote anayepata mapato ya zaidi ya shilingi
10,000,000 alipe kodi ya Mapato ya shilingi 500,000 kujumlisha na
asilimia 42 ya tofauti ya shilingi 10,000,000 na shilingi 3,200,000 kama
inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini. Lengo la mapendekezo haya ni
kuwafanya watu wenye kipato kikubwa walipe kodi zaidi kulingana na
kipato wanachopata maana hivi sasa masikini wanalipa kodi nyingi zaidi
kuliko wenye nacho.
| Mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi | Kodi (PAYE) | Mapendekezo ya mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi | Kiwango kipya cha Kodi (PAYE) |
| Mapato yanayozidi shilingi 720,000 | Sh. 112,500 ongeza 30% ya kiasi kinachozidi sh. 720,000 | Mapato yanayozidi 720,000 lakini hayazidi sh. 3,199,199 | Sh.112,500 ongeza 30% ya ziada ya sh. 720,000 |
|
| Mapato yanayozidi sh. 3,200,000 lakini hayazidi sh.9,999,999 | Sh.190,000 ongeza 38% ya ziada ya 3,200,000. |
|
| Mapato kuanzia sh. 10,000,000 na kuendelea | Sh. 500,000 ongeza 42% ya mapato yake. |
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo haya hayatapunguza Mapato ya Serikali kwani wigo wa kodi
utakuwa umeongezeka kwa kuwagusa wafanyakazi katika sekta binafsi na pia
kupata kodi zaidi kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.Mheshimiwa Spika, vile vile Kambi ya Upinzani inaendelea kupendekeza kuwa mchakato uanze ili kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na zaidi awe anajaza fomu za kodi (tax returns)
kila mwaka. Suala hili ni muhimu sana na litangazwe mwaka huu ili tuwe
na mwaka mzima wa kujitayarisha ili lianze Mwezi Julai mwaka 2013.
Mtanzania yeyote, awe na kipato au asiwe na kipato ajaze Tax Returns.
Mfumo huu utatoa takwimu muhimu sana kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na
utasaidia sana hapo baadaye kupanua wigo wa Mapato. Tunapendekeza
marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato ili mfumo huu uwepo kisheria
ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.Mheshimiwa Spika, Vile vile, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwa Real Estate Regulatory Authority kama tulivyofanya kwa mwaka uliopita
na kwamba kila mwenye nyumba ya kupangisha lazima atambuliwe na kulipa
kodi inavyostahili. Lengo ni kuhakikisha Sekta ya Nyumba inatoa mapato
ya kutosha kwa Serikali na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi inayofanywa na
wenye nyumba.Presumptive TaxMheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani
Bungeni ilipendekeza mwaka 2011/12 kwamba ushauri wa Mradi wa kuboresha
mfumo wa kodi (Tax Modernisation Project) ambao ulishauri kwamba ipo
haja ya kuainisha Kodi ya VAT na Presumptive Tax, utekelezwe. Tunashauri
kuwa kodi anayotozwa mfanyabiashara ndogondogo kabla hajaanza kufanya
biashara ifutwe kabisa. Uamuzi huu utapunguza mapato ya Serikali
(Shilingi bilioni 21.6 kwa mujibu wa Kitabu cha Bajeti Vol. I) katika
kipindi cha muda mfupi lakini itakuwa ni chanzo kikubwa sana cha mapato
katika kipindi cha muda mrefu.Vyanzo vipya vya MapatoMheshimiwa Spika,Pamoja
na kupitia vyanzo vya mwaka jana na kulinganisha na mapendekezo ya
Serikali, Kambi ya Upinzani bado inapendekeza vyanzo vya ziada mwaka huu
ili kuboresha Mapato ya Serikali.Kupanua wigo wa Skills Development levyMheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunapenda kushukuru kuwa wazo letu la kutoza kodi ya skills development levy
tuliyopendekeza katika hotuba yetu ya mwaka uliopita lilifanyiwa kazi
na serikali lakini kwa mwaka ujao wa fedha tunaitaka serikali kuipitia
upya kodi kwa kuongeza wigo wa wachangiaji ili kuwa na fedha za kutosha
kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu.Mheshimiwa Spika, tunapendekeza kiwango cha tozo ya kuendeleza stadi (skills development levy – SDL) kishuke
kutoka asilimia 6 ya sasa mpaka asilimia 4. Tunapendekeza kuwa Waajiri
wote walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Lengo ni
kupunguza mzigo kwa Waajiri na kuondoa ubaguzi kwani wanaofaidika na
tozo hii (wanafunzi wa elimu ya Juu) pia huajiriwa na Serikali na
Mashirika ya Umma. Serikali ilipanga kukusanya tshs 161bn kutoka katika
tozo hii kwa mfumo wa sasa. Mheshimiwa Spika, Marekebisho ambayo Kambi ya Upinzani inayapendekeza yataongeza mapato ya Serikali mpaka tshs 320bn.Mheshimiwa Spika,
Waziri wa Fedha katika tozo hii amesema Serikali ‘itapitia upya maudhui
ya viwango vya tozo’ hii. Kambi ya Upinzani imetamka maudhui na viwango
na tunaiomba Serikali itekeleze pendekezo hili.Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza mgawanyo wa tozo hii urekebishwe kwa kuongeza mapato yatakayokwenda kwenye Vyuo vya Ufundi mchundo. Mheshimiwa Spika,
kama wanafunzi wetu watasomeshwa na kodi hii basi tuangalie upya mfumo
wa Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Fedha inayopatikana kwenye Kodi
hii itumike kusomesha kwa ‘grant’ wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi
darasani na kuwapunguzia mzigo wa mikopo. Vile vile tuangalie kama
tunaweza kukopesha wanafunzi malazi na chakula tu na kutoa bure ada na
mafunzo kwa vitendo pamoja na vitabu. Kulinda kazi za WasaniiMheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani mara kwa mara tumekuwa tukieleza jinsi wasanii
wanavyoshindwa kunufaika na kazi zao kutokana na kukosekana mfumo rasmi
wa kiserikali unaozuia wizi wa kazi za wasanii. Pamoja na serikali
kukubali kuahidi kuwa na mfumo rasmi wa kuzuia wizi wa kazi hizo,
serikali haijaweka wazi mfumo rasmi utakaokuwa unatumika kuzuia wizi huo
na hatimaye wasanii kunufaika na kazi zao.Mheshimiwa Spika,
Kambi ya upinzani katika hotuba ya Wizara ya Habari Vijana na Michezo
kwa mwaka uliopita tulingumzia suala hili na tulishauri kwamba kuwe na
utaratibu wa kuweka stiker maalumu zinazotolewa na mamlaka za
serikali kuonyesha uhalali wa muuzaji wa kazi za wasanii. Serikali
imetekeleza pendekezo letu. Hata hivyo tuna maoni tofauti kuhusu namna
ya kutekeleza pendekezo hili.Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, serikali mwaka 2006 kupitia gazeti
la Serikali Na. 18 la tarehe 10 Mwezi wa Februari, ilianzisha utaratibu
wa HAKIGRAM kama stiker maalumu za kazi halali za wasanii zinazotolewa
na COSOTA. Kambi ya Upinzani tunapendekeza utaratibu huo uendelee na
Mamlaka ya Mapato TRA ihusike kukusanya mapato kwa ajili ya kazi hiyo na
COSOTA wataratibu utoaji wa HAKIGRAM. Hii itaenda sambasamba na kuzuia
uchakachuaji wa HAKIGRAM hizo ili kutopoteza lengo la kuweka mfumo huo.
Stiker zisitolewe na TRA bali zitolewe na COSOTA na TRA isimamie eneo la
Mapato tu. Hii itasaidia kwani stiker hizi hazitatumika kupata mapato
peke yake bali pia kuweka kumbukumbu muhimu za kazi za wasanii.Mapato kutoka Sekta ndogo ya Mawasiliano ya SimuMheshimiwa Spika, serikali
imekuja na pendekezo la kuendelea na kutoza ushuru wa bidhaa kwenye
masuala ya huduma ya mawasiliano ya simu, jambo ambalo litamgusa
mtumiaji wa huduma hiyo ambaye ni mwananchi wa kawaida na hivyo kuongeza
gharama za simu. Kambi ya Upinzani inapinga kabisa kuongeza ushuru wa
bidhaa kwenye muda wa Maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi.Mheshimiwa Spika,
Hoja ya wananchi hapa ni kwamba Kampuni za Simu za mkononi hazilipi
kodi ya kutosha na hasa kodi ya Makampuni (corporate tax). Waziri Mkuu
alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti mwaka 2011 alitangaza Kampuni ambazo
ni walipa kodi wakubwa katika kipindi cha miaka 5 iliyopita. Katika
orodha hiyo kulikuwa na Kampuni moja tu ya Simu za Mkononi (Kampuni ya
AirTel). Mheshimiwa
Spika, wakati wananchi wanataka kodi zaidi kutoka Kampuni za simu,
Serikali inapendekeza kuongeza kodi kwa mwananchi anayetumia simu.
Kampuni zilipe kodi ya Mapato na sio kukandamiza wateja kwa ushuru wa
bidhaa ilihali huduma zenyewe za simu hazina ubora.Mheshimiwa Spika,
Vilevile wananchi wanalalamika kwamba Kampuni za simu za Mkononi
hajiweki wazi mapato yake yote hali iliyopelekea Kamati ya Bunge ya POAC
kuiagiza TCRA kufunga mtambo utakaoweza kuijulisha TCRA mapato yote
ambayo kampuni za Simu zinapata. Serikali ya Ghana ilifanya hivi na
kupandisha maradufu mapato yanayotokana na sekta ndogo ya simu. Hivi
sasa Ghana, nchi yenye watumiaji wa simu milioni 17 ukilinganisha na
Tanzania yenye watumiaji 23 milioni, inakusanya asilimia 10 ya Mapato ya
Serikali kutoka kwenye kampuni za Simu peke yake. Iwapo Tanzania
ikifikia kiwango cha Ghana cha asilimia 10 ya Mapato ya ndani ya
Serikali kutoka kwenye kampuni za simu, Tanzania itaweza kukusanya zaidi
ya Shilingi bilioni 860 kutoka kwenye sekta ndogo ya simu peke yake.
Hata hivyo mazingira ya Ghana na Tanzania ni tofauti na hivyo
tunapendekeza kiwango kutokana na hali yetu.Mheshimiwa Spika, Shirika la TCRA kupitia zabuni nambari AE-020/2010-11/C/04 imetangaza ‘request
for expression of interest for design, development, installation and
Management of Telecommunication monitoring system under build, operate
and transfer’ ili kupata chombo cha kufuatilia Mapato ya Kampuni za
Simu. Kwa mujibu wa ratiba zilizotangazwa na TCRA chombo kitakuwa
kimeanza kazi mwishoni mwaka huu wa 2012. Kwa dhati kabisa napenda
kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA na watumishi wote kwa kutekeleza
maelekezo ya Kamati ya Bunge kwa haraka ili kuhakikisha mapato kwa nchi
yetu.Mheshimiwa Spika,
kilichotushangaza ni kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi hakugusia kabisa
suala hili muhimu sana kwa mapato ya Serikali badala yake Serikali
imekimbilia kukandamiza wanyonge watumiaji wa Simu na kuyaacha Makampuni
ya Simu yakilipa kiduchu kutoka kwenye mapato yao.Mheshimiwa Spika,
uamuzi huu wa kufuatilia mapato ya Kampuni za Simu na Marekebisho
tunayopendekeza ya kujenga uwezo zaidi wa TCRA kwa kuwa na Idara ya
‘Revenue Assurance’ na kurekebisha sheria ya TCRA kwa kuweka wazi
makujumu ya TRA ndani ya TCRA, utaiingizia Serikali mapato ya takribani
tshs 660bn.Mheshimiwa Spika,
katika eneo hili la Sekta ya Mawasiliano ninaomba kurejea kuitaka
Wizara ya Fedha itoe maelezo hapa Bungeni namna ambavyo Hisa za serikali
katika Kampuni ya MIC Tanzania ltd inayomiliki Kampuni ya Tigo
zilivyouzwa. Mheshimiwa Spika Serikali ilikuwa inamiliki hisa asilimia
26 katika Kampuni hii. Kwa mujibu wa kumbukumbu nilizoziona Hisa hizi
zote ziliuzwa kwa thamani ya dola laki saba kwa mwana hisa mwenza mnamo
mwezi Februari mwaka 2004. Kampuni hii leo inapata mapato ya Tshs
bilioni 20 kwa mwezi,
tuliuza hisa zetu asilimia 26 kwa dola laki saba! Laki Saba dola! Kambi
ya Upinzani inataka uchunguzi maalumu katika mauzo haya na Taifa
liambiwe nini kilitokea na hatua gani za kuchukua dhidi ya waliouza
mali hii ya Umma bila zabuni wala kuzingatia thamani ya fedha.Kuzuia mauzo ya ngozi ghafi nje ya nchiMheshimiwa Spika, Kambi
ya Upinzani imeshangazwa na hatua ya serikali kuja na pendekezo la
kuongeza ushuru kwenye bidhaa ya ngozi ghafi inayosafirishwa nje kutoka
asilimia 40 hadi 90 lengo likiwa ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi hiyo
na kuiongezea thamani. Mheshimiwa Spika,
kwa nchi iliyo na mianya mingi ya rushwa kama Tanzania hatua hii
haitakuwa na tija kwa kuwa wafanyabiashara wengi wa ngozi ghafi wamekuwa
na tabia ya kupunguza takwimu za kusafirisha ngozi ghafi na hivyo
kupelekea serikali kukosa mapato mengi sana. Serikali inafahamu kwamba
hata ushuru wa mauzo nje wa asilimia 40 haukuweza kutatua tatizo la
viwanda vya ndani kukosa malighafi. Kambi ya Upinzani haikubaliani na
Pendekezo la Serikali kwani halitatatua tatizo la kukuza sekta ndogo ya
Ngozi nchini.Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kuzuia kabisa kusafirisha ngozi
ghafi kwenda nje na badala yake kuwe na mpango wa kutumia ngozi ghafi
hapa nchini na kuleta tija katika uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira
na kuongeza thamani ya mauzo nje.Mheshimiwa Spika,
hatua ya kuzuia ngozi ghafi kusafirishwa kwenda nje kwa Tanzania
itakuwa sio suala jipya kwa sababu Ethiopia imezuia na kuwekeza katika
kiwanda cha viatu, mikanda na bidhaa za ngozi. Kutokana na Mpango wa
Mendeleo ya Ethiopia (GTP – Growth and Transformation Plan) sekta ya
Ngozi itaingiza fedha za kigeni za thamani ya dola za Kimarekani bilioni
4 kwa mwaka. Hii ni sawa na fedha za kigeni ambazo Tanzania inapata
kutoka kwenye Dhahabu na Utalii kwa pamoja. Ethiopia nchi iliyokuwa
inatembea na bakuli na kulia njaa
leo inakuwa nchi ya kupigiwa mfano na sisi Watanzania! Rais Yoweri
Kaguta Museveni wa Uganda pia amepiga marufuku kuuza ngozi ghafi nje.
Hata nchi ya Pakistani ambayo ndio ngozi zetu zinakwenda nayo imepiga
marufuku mauzo ya ngozi ghafi nje. Serikali ipige marufuku Mauzo ya
ngozi ghafi nje ya Nchi ili kulinda viwanda vya ngozi nchini, kuoongeza
Ajira na kuongeza mapato ya Fedha za kigeni.Kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa za MaziwaMheshimiwa
Spika, sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini inahitaji kuwekewa maazingira
ya kukua ili izalishe ajira na mapato ya kodi kwa Serikali. Wakati
Tanzania ndio nchi ya Afrika Mashariki inayoongoza kwa kuwa na Ng’ombe wengi lakini inaongoza kwa kuagiza
maziwa kutoka nje yenye thamani ya dola za kimarekani 3.6m. Wakati
Kenya imelinda soko la Maziwa na Bidhaa za Maziwa kwa kuondoa (zero
rating) kodi ya VAT kwenye bidhaa za Maziwa, Waziri wa Fedha hajaonyesha
kabisa juhudi zozote za kujengea uwezo sekta ndogo ya Maziwa hapa
nchini na hivyo kuweza kuondolewa kabisa katika ushindani na kujikuta
wafugaji wanakosa kabisa soko la kuuza maziwa yao hapa nchini. Nchi za
Rwanda na Uganda pia zimelinda Maziwa na Bidhaa za maziwa kwa njia hii.
Ni muhimu Serikali kuwianisha kodi hii na Nchi nyingine za Afrika
Mashariki.Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kufanya marekebisho kwenye sharia ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kufanya ‘zero rating’ kwenye Maziwa na Bidhaa za Maziwa zinazozalishwa hapa nchini kwa kipindi cha miaka 5 ilikufikisha uzalishaji wa angalau lita 500,000 za maziwa kwa siku kutoka lita123,000 za sasa na kuweza kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya elfu tatu.Mheshimiwa Spika, hatua zote za kuongeza mapato tulizopendekeza pamoja na hatua za Bajeti Mbadala iliyopitaambazo
tunarudia kuzipendekeza zitaongeza Mapato ya Serikali kwa takribani
shilingi bilioni 2,885 kama inavyoonyeshwa katika jedwali hapa chini.
NYONGEZA YA VYANZO VYA MAPATO MBADALA 2012/2013
| Chanzo cha Mapato | Makisio - Bilioni |
| Marekebisho ya kodi za misitu ikiwemo Mkaa |
|
| Kupunguza misamaha ya kodi, kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa Biashara ya Nje |
|
| Mauzo ya hisa za serikali |
|
| Marekebisho ya kodi Sekta ya madini (kodi ya Mapato, Kodi ya CGT na ushuru mbalimbali) (25% ya Mauzo ya Madini Nje) |
|
| Marekebisho ya Kodi na Usimamizi bora wa Mapato Kampuni za Simu |
|
| Marekebisho ya Kodi ya SDL |
|
| Mapato ya wanyamapori |
|
| Kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta- kampuni za madini |
|
| Usimamizi wa mapato ya utalii |
|
| Kuimarisha biashara katika EAC kwa kuongeza mauzo |
|
| JUMLA |
|
Mheshimiwa Spika,
kama nilivyosema hapo juu, vyanzo hivi vya mapato ni mjumuisho wa
vyanzo ambavyo katika hotuba zetu mbadala za nyuma tumekuwa
tukipendekeza, ambapo tumevifanyia marekebisho kulingana na hali halisi
ya uchumi ulivyo kwa sasa, pamoja na kupendekeza baadhi ya marekebisho
ya sheria za kodi ili kuongeza mapato zaidi kwa Serikali.DENI LA TAIFA Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inasikitika kwa serikali kuendelea kutengeneza madeni
kwa Taifa kwa kuendelea kukopa zaidi kwa matumizi ya kawaida ya
serikali. Wakati Serikali inasisitiza kwamba Deni letu linastahmilika,
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anaonyesha mashaka makubwa sana
kutokana na kasi ya kukua kwa Deni la Taifa. Taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni la Taifa
linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka shilingi trillion 10.5 mwaka
2009/2010 hadi shilingi trillion 14.4 mwaka 2010/2011. Kwa mujibu wa
Waziri wa Fedha Deni la Taifa limefikia shilingi trillion 20.3 mpaka
ilipofika mwezi Machi mwaka 2012. Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012
ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia shilingi trillion
22. Mheshimiwa
Spika, Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali bali
ni kwamba tunakopa kufanyia nini? Bajeti ya Mwaka 2012/13
inayopendekezwa inaonyesha kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni
8.7 kama makusanyo ya ndani na itatumia shilingi trilioni 10.6 kama
matumizi ya kawaida. Ni dhahiri kwamba sehemu ya mikopo ambayo serikali
inachukua sasa itakwenda kwenye matumizi ya kawaida. Hatutaki mikopo kwa
ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari nk. Tuchukue
mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi
zaidi. Bajeti inaonyesha kwamba Serikali itakopa shilingi takribani
trillion 5 mwaka 2012/13. Serikali ikubalikutekeleza mapendekezoya
Kambi ya Upinzani ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupanua wigo wa
kodi katika maeneo muhimu kama sekta ya madini na mawasiliano, kuzuia
misamaha ya kodi, kutokomeza ukwepaji kodi, na kuepuka matumizi mabaya
ili kuepuka madeni yasiyo ya lazima.Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kusisitiza kwamba Bunge lifanye
ukaguzi maalumu kuhusu akaunti ya Deni la Taifa ili kuweza kubaini
ukweli kuhusu ustahmilivu wa Deni na mikopo ambayo Serikali inachukua
kama inakwenda kwenye Maendeleo na miradi ipi na kama miradi hiyo ina
tija. Vilevile tumependekeza kwamba Mikopo yote ambayo Serikali
inachukua iwe inapata idhini ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi au
Bunge litunge sharia ili kiwango cha juu cha kukopa ambacho Serikali
haipaswi kuvuka. Kuiacha Serikali inaendelea kukopa bila mpango ni
kuliweka Taifa rehani na kupeleka mzigo wa kulipa madeni haya kwa kizazi
kijacho. Hatuwezi kukubali Wazee wetu waishi maisha yao, waishi maisha yetu na pia wakope maisha ya watoto wetu.Mheshimiwa Spika, Ukiangali
sura ya Bajeti ya Serikali, inaonyesha kuwa Serikali itakopa fedha
zenye masharti ya kibiashara ndani na nje yenye thamani ya Tshs.
Trilioni 2.89 kwa kipindi hiki cha 2012/13. Athari ya mikopo ya
kibiashara ya ndani ni kubwa sana kwa watanzania, kwanza inawafanya
wananchi hasa wajasiriamali wanaokopa kushindanana Serikaliyao,
kwani mabenki yatashindwa kuwakopesha wafanyabiashara au wakikopa
watakopa kwa masharti magumu na hasa riba kuwa kubwa. Jambo hili
linapunguza uwezo wa wazalishaji kuongeza uzalishaji hasa viwandani kwa
kukosa mikopo ya uendeshaji. Kama tulivyoshauri hapo juu, Serikali
ijiepushe na mikopo ya masharti ya kibiashara kwa kuongeza makusanyo ya
kodi.Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Serikali
kuwa imepata Mshauri Mwelekezi atakayeishauri katika kujiandaa kufanyiwa
tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni. Serikali ilieleze Bunge
ni lini na kwa namna gani zabuni ya kumpata mshauri huyu ilitangazwa na
kama Sheria ya Manunuzi ilifuatwa.Mwenendo wa Matumizi.Mheshimiwa
Spika, Serikali inapendekeza Bajeti ya TZS 15 trilioni(USD 8.75
Billion) katika mwaka 2012/13 kama ilivyowasilishwa na Waziri wa Fedha
na Uchumi wiki iliyopita. Uchambuzi wa vitabu vya Bajeti unaonesha
kwamba mafungu ya juu 5 yatakayoongoza kwa matumizi kwenye Bajeti hiyo
ni Kama ifuatavyo;
1. Huduma kwa Deni la Taifa Tshs 2.7 trilioni(USD 1.69 Billion)
2. Wizara ya Ujenzi. Tshs 1 trilioni (USD 625 Million)
3. Wizara ya Ulinzi Tshs 920 bilioni (USD 575 Million)
4. Wizara ya Elimu Tshs 721 bilioni (USD 451 Million)
5. Wizara ya Nishati na Madini Tshs 641 bilioni (USD 400 Million)
Jumla TZS 5.982 Trilioni(USD 3.74 Billlion)
Chanzo: Vitabu vya Bajeti kwa Wabunge
Mheshimiwa Spika,
Jumla ya mafungu haya ni sawa na asilimia 40% ya Bajeti yote, kwa hiyo
asilimia 40% ya Bajeti yote imepangwa kwa mafungu 5 tu na kati ya hayo
Wizara ni nne tu za Ujenzi, Elimu, Ulinzi na Nishati na Madini. Wizara
ya Kilimo wala Afya hazimo kabisa katika Wizara 5 zitakazopata fedha
nyingi zaidi katika Bajeti. Fungu lenye kiwango kikubwa zaidi ya Bajeti
kuliko vyote ni fungu 22 ambalo ni malipo kwa Deni la Taifa. Pia sehemu
kubwa ya fedha zilizotengwa kwa Ujenzi na Nishati ni madeni kwa
wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miaka ya nyuma. Shilingi bilioni 40
ambazo zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kiwira katika Wizara ya Nishati
na Madini ni kwa ajili ya kulipia Madeni ya Kampuni ya TanPower
Resources ambayo iliuziwa Mgodi wa Kiwira na kushindwa kuundeleza.Mheshimiwa
Spika, Madhara ya Deni la Taifa yanaonekana hapa katika matuumizi ya
Serikali ambapo tunapokuwa tunalipa madeni tunachukuwa rasilimali
fedha nyingi kutoka kwenye Miradi ya Maendeleo. Wakati Bajeti ya
Maendeleo ni shilingi trilioni 4.5, Bajeti ya kugharamia Deni la Taifa
ni shilingi trilioni 2.7 (sawa na nusu ya Bajeti nzima ya Maendeleo).
Mheshimiwa Spika,
Bajeti ya 2012/13 ni ya kulipa madeni zaidi kuliko Bajeti ya kuchochea
maendeleo ya Taifa letu. Bajeti hii pia yaweza pia kuwa ni Bajeti ya
kukopa zaidi maana jumla ya TZS 5.1 trilioni (USD 3.19 Billion)
zitachukuliwa na Serikali kama mikopo kutoka vyanzo mbalimbali. Mikopo
ya kibiashara ambayo ni mikopo ghali sana itachukuliwa kwa wingi zaidi
kuliko mwaka wa fedha uliopita.
Mheshimiwa Spika, Mgawanyo
wa rasilimali za nchi kwenye sekta za kipaumbele (Miundombinu ya
usafirishaji kama reli, bandari, ndege viwanja vya ndege n.k), Barabara,
nishati,kilimo na mifugo, ili kuinua uchumi zimetengewa fedha kidogo
sana kuweza kuleta tija kulingana na malengo ya Mpango wa Maendeleo kama
ulivyopitishwa na Bunge lako tukufu. Bajeti iliyotengwa kwa ajili ya
nishati imeshuka kwa kiwango cha shilingi 40 bilioni, pia kwa mwaka
uliopita fedha zilizotengwa kwa ajili ya miundombinu,reli na TEHAMA
zilitengwa shilingi 2,781.4 bilioni kwa 2011/12 ikilinganishwa na
shilingi 1,505.1 bilioni kwa mwaka 2010/2011,(hili lilikuwa ni ongezeko
la asilimia 85). Kwa bajeti ya mwaka huu inaonesha sekta zilezile za
vipaumbele; bajeti iliyotengwa ni shilingi 1.394.5 bilion ambayo ni
pungufu ya asilimia 49.86 kwa kulinganisha na mwaka 2011/2013.Mheshimiwa
Spika, wakati Waziri wa Fedha analiambia Bunge kuwa ametenga shilingi
bilioni 1,383 kwa ajili ya Usafirishaji na Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi
imetengewa shilingi bilioni 1,000 kati ya hizo. Wizara ya Uchukuzi yenye
Reli, Bandari, Viwanja vya Ndege na Usafiri wa Maziwa ya Tanganyika,
Nyasa na Viktoria imetengewa chini ya shilingi bilioni 380. Serikali pia
haijasema fedha ambazo zilitengwa na Bunge katika Bajeti inayomaliza
muda wake na kuzielekeza kwenye Wizara ya Miundombinu na Wizara ya
Uchukuzi zimetumikaje maana bado wakandarasi wanadai na fedha za Reli
hazikutoka zote kama ilivyopitishwa na Bunge.Mheshimiwa
Spika, Wizara nyingi hazikupata fedha za Maendeleo kama zilivyopitishwa
na Bunge. Halmashauri za Wilaya ndio zilipata hali mbaya zaidi katika
kupata fedha za Maendeleo ambapo kwa wastani ni asilimia 47 tu ya Bajeti
ndio ilipelekwa katika Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa.
Kutokana na hali hii Wabunge kama wawakilishi wa wananchi walihoji
Serikali kwenye Kamati zao na kupata majibu ambayo sio ya kuridhisha
hivyo kupelekea Wabunge kugomea baadhi ya Wizara.Mheshimiwa Spika,
Ushahidi wa hayo ni baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge kukataa
kukubali Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa baadhi ya Wizara zilizo
chini ya Kamati hizo. Wizara ambazo hazikupitishiwa /Kukubaliwa
makadirio yake ni pamoja na; · Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, · Wizara ya Uchukuzi, na
(nilishangaa kumwona Waziri wa Uchukuzi akiwaahidi wananchi pale
Jangwani kwamba Reli inakarabatiwa vya kutosha ilhali Kamati
haijapitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa kuwa haikupewa
fedha za kutosha)· Wizara ya Kilimo, Chakula na UshirikaMheshimiwa Spika, kabla Bunge lako tukufu halijajadili Makadirio ya Matumizi ya mwaka unaokuja ni vema Serikali itueleze kwanza fedha zilizotengwa mwaka uliopita na hazikufika hatima yake nini?Mheshimiwa Spika,
uwiano wa bajeti iliyotengwa kwa matumizi ya kawaida ambayo ni asilimia
70% wakati bajeti ya maendeleo asilimia 30% haiwezeshi nchi kupiga
hatua ya haraka ya Maendeleo. Kama ilivyoonyeshwa na Waziri Kivuli
Mipango na nitakavyohitimisha hotuba hii, Serikali imetayarisha Bajeti
hii bila kuzingatia masharti yaliyowekwa na Mpango wa Maendeleo
uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu ibara ya 63
(3)(c) kwa kutotenga asilimia 35 ya Mapato ya ndani ya Serikali kwenye
Bajeti ya Maendeleo.Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo katika miradi ya maendeleo katika bajeti zake. Kwa
mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), matumizi ya kawaida ya Serikali yanaongezeka huku matumizi katika
shughuli za maendeleo yanapungua mwaka hadi mwaka. Takwimu katika
jedwali hapa chini zinaonyesha
| Fungu | 2009/2010 | % | 2010/2011 | % |
| Fedha za matumizi ya kawaida (Sh) | 6,251,629,581,428 | 73 | 7,587,424,923,903 | 77 |
| Fedha za matumizi ya maendeleo (Sh) | 2,299,010,652,135 | 27 | 2,223,684,150,465 | 23 |
| Jumla | 8,550,640,233,563 | 100 | 9,811,109,074,368 | 100 |
Chanzo: Ripoti ya CAG, uk. 21Aidha,
kwa miaka miwili iliyopita yaani 2009/2010 na 2010/2011 kumekuwa hakuna
uwiano wa fedha za Maendeleo kama bajeti zilivyopitishwa na Bunge dhidi
ya fedha zinazotolewa na hazina kwa ajili ya maendeleo katika Wizara na
Idara. Tazama jedwali;
| Mwaka | Bajeti iliyoidhinishwa | Fedha halisi zilizotolewa | Tofauti (Sh) | % |
| 2009/2010 | 2,825,431,400,000 | 2,299,010,652,135 | 526,420,747,865 | 19 |
| 2010/2011 | 3,750,684,569,000 | 2,223,684,150,465 | 1,527,000,418,535 | 41 |
Chanzo: Ripoti ya CAG, uk.22Mheshimiwa Spika,
Kutokana na takwimu hizi, jumla ya Sh. 1,527,000,418,535 au asilimia
41 ya fedha zilizoidhinishwa kwa maendeleo hazikutolewa katika mwaka wa
fedha 2010/2011, na kiasi cha Sh. 526,420,747,865 au asilimia 19 ya
fedha zilizoidhinishwa mwaka 2009/2010 hazikutolewa pia. Hii ina maana
kuwa shughuli za maendeleo za kiasi hicho cha fedha hazikutekelezwa kwa
miaka husika.Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inatafsiri hali hiyo kama utovu mkubwa wa nidhamu ya
matumizi ya fedha za umma kwa upande wa Serikali, Vilivile inaonesha ni
jinsi gani Serikali yetu haithamini maendeleo ndio maana kila mwaka
Serikali inazidisha matumizi yake na kuhakikisha kuwa inayapata kwa
wakati huku ikipunguza bajeti ya maendeleo na kutotoa fedha zote kama
zilivyoidhinishwa na mbaya zaidi hata zile zinazotolewa hazitolewi kwa
wakati muafaka. Hii inafanya kukaa hapa Dodoma na kupitisha Bajeti kuwe
hakuna maana maana Bajeti haitekelezwi kama ilivyopitishwa.Mheshimiwa
Spika, Kiasi kinachotengwa kwa ajili ya maendeleo kimeshuka kutoka
shilingi trilioni 4.9 katika mwaka wa fedha 2011/12 hadi kufikia kiasi
cha shilingi trililioni 4.5 mwaka huu wa fedha 2012/13. Pamoja na
serikali kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika bajeti
iliyopita, bado imeendelea kupunguza bajeti ya maendeleo katika bajeti
hii. Ni dhahiri serikali haizingatii swala la maendeleo ya mwananchi,
pia kutoona njia ya kuweka mkazo katika maendeleo na kuendelea kupuuzia
maazimio ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano.Mheshimiwa Spika,
katika Bajeti mbadala, Kambi ya Upinzani imetenga asilimia 36.06 na
kukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kutoka katika mapato ya
ndani kwa matumizi ya maendeleo kama Mpango wa Maendeleo ya Taifa
ulivyoelekeza. Mheshimiwa
Spika, Tuliamua kama Taifa kwamba Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano
ndio safina yetu ya kuelekea nchi ya ahadi (middle income country).
Mpango ukapitishwa na Bunge na kuwekwa sahihi na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Inasikitisha kuona kuwa Serikali inatoboa kisiri
siri safina hii wakati tupo kati kati ya maji! Ninaamini wananchi
wanawaona wanaotoboa safina yetu na watawatosa kabla hawajazamisha Taifa
zima kwa kushindwa kutekeleza Mpango unavyoelekeza.Ubadhirifu wa fedha zinazotengwaMheshimiwa
Spika, pamoja na fedha za maendeleo kutolewa kidogo kulinganisha na
bajeti inayopitishwa na Bunge, bado kumekuwepo na matumizi yasiyo na
tija na ubadhirifu mkubwa.Mheshimiwa Spika, upotevu wa fedha za umma umeendelea kuwa kikwazo
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Uchambuzi
wetu juu ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kwa mwaka 2010/2011 pekee, umebaini takribani jumla ya Bilioni
12.9 (12,968,168,985) za fedha za umma zimepotea kama ongezeko kutoka
shilingi billion 11.9 (11,152,048,065) ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 14 ya upotevu wa fedha za Serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010,hii inaonyesha kuwa Serikali inaona ni jambo la kawaida kupoteza viwango hivi vya pesa za Serikali na kambi ya upinzani kuwasisistiza wananchi kuendelea kuitathmini Serikali yao sasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi dhidi ya Serikali yao.MAPENDEKEZO YA KAMBI YA UPINZANISERA YA MATUMIZI 2012/13 KWA BAJETI MBADALAMheshimiwa Spika,
lengo kuu la Bajeti Mbadala ni kuhakikisha uchumi unakua katika maeneo
ya vijijini kwa kati ya asilimia 6 na 8 ili kuleta Maendeleo ya wananchi
na kutokomeza umasikini. Kwa njia hiyo ni dhahiri wananchi wapatao
milioni 30 waishio vijijini watanufaika na matumizi ya raslimali zao.Vipaumbele vya bajeti ya Matumizi.(i) Kujenga
Mazingira ya Ukuaji wa uchumi vijijini (rural growth) kwa kuboresha
miundombinu ya umeme, barabara, maji na miundombinu ya Umwagiliaji.
Tunapendekeza kutumia shilingi bilioni 600 kila mwaka (bilioni 150 kwa
kila sekta niliyotaja). Fedha hizi zitasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo
Vijijini (Rural Development Authority – to be established) itakayokuwa
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (ii) Kukarabati
Reli ya Kati na matawi yake ya Tanga/Arusha na Mpanda. Tutatenga tshs
443bn kwa RAHCO kwa ajili ya Reli. Lengo ni kuhakikisha Reli ya Kati
inafikia uwezo wa kusafirisha Tani 1.5m kwa mwaka na hivyo kulipatia
Taifa fedha za kigeni katika sekta ya usafirishaji kupitia Bandari ya
Dar es Salaam. Tunataka sekta ya usafirishaji iliingizie Taifa fedha za
kigeni mpaka dola za kimarekani 1.5 bilioni kutoka dola 0.5 bilioni za
sasa.(iii) Kuboresha
Elimu na Afya hasa kwa Shule na Zahanati/Vituo vya Afya vya Vijijini
kwa kutoa motisha kwa wafanyakazi wa Sekta hizi walio kwenye Halmashauri
za Wilaya. Tunapendekeza posho za Mazingira ya Vijijini kwa Walimu,
Madaktari na Manesi sawa na mara moja na nusu ya Mishahara yao. Vile
vile tutaongeza mishahara ya Walimu, Manesi na Madaktari kwa asilimia
50, pamoja na kuboresha stahili zingine za kazi ili kuvutia Watanzania
wengi zaidi katika maeneo haya na kuboresha huduma zao kwa wananchi.(iv) Kuongeza Kima cha chini cha Mshahara kwa Wafanyakazi wa Umma mpaka Tshs 315,000 kwa Mwezi(v) Kuanzisha Pensheni ya uzeeni kwa Wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60.(vi) Kujenga
Uwezo wa Viwanda vya ndani ili Kuuza nje bidhaa za kilimo na mifugo
zilizoongezewa thamani. Tutazuia kuuza nje Korosho ghafi na Ngozi ghafi
kwa kuanzia. Lengo ni kufufua viwanda vyote vya nguo na kuanzisha
viwanda vipya kwa kutoa motisha kwa wawekezaji watakaotumia malighafi za
hapa nchini.(vii) Kupunguza
mzigo wa matumizi ya magari ya Serikali kwa kupiga mnada baadhi ya
‘mashangingi’ na kuweka mfumo wa kukopesha Magari kwa watumishi wote wa
Umma wanaostahili Magari kama alivyofanya Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania. Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Fedha na Uchumi, Waziri wa
Fedha alitamka, ‘….kufanya mapitio ya stahili za aina za magari kwa
viongozi wa ngazi
mbalimbali na kuandaa mwongozo wa kugharamia ununuzi wa vyombo vya
usafiri ili kupunguza matumizi ya magari, mafuta na matengenezo ya
magari…’ kama hatua za kubana matumizi. Hatua hii ya kupunguza gharama
za magari Waziri hakuisema kabisa katika hotuba yake Bungeni.(viii) Kuendelea
kusisitiza kufutwa kwa posho za vikao katika mfumo mzima wa malipo na
stahili kwa watumishi wa Umma. Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Fedha,
Waziri wa Fedha alitamka ‘…. Kufanya mapitio ya posho na stahili zote
kwa lengo la kuziwianisha….’ Suala hili nalo Waziri hakulizungumza
kabisa katika Hotuba yake Bungeni.(ix) Kuanzisha
Chuo Kikuu cha Mtwara (Mtwara University for Petroleum Studies) ili
kuzalisha wataalamu wa kutosha wa Sekta ya Mafuta na Gesi na kuliandaa
Taifa kuwa na wasomi mahiri wa maeneo hayo na hivyo kufaidika na Utajiri
wa Mafuta na Gesi uliopo nchini kwetu. Tunapendekeza shilingi bilioni
200 mwaka huu katika Bajeti ya Wizara ya Elimu kwa ajiri ya Mradi huu.(x) Kutunga sheria mpya ya Mashirika ya Umma (Public Corporations Act) ili kujengea uwezo Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vyema
Mashirika yote ya Umma ambayo Serikali inamiliki kwa zaidi ya asilimia
100 na kutoa nguvu za kisheria kwa Shirika la CHC kuweza kusimamia hisa
za Serikali katika Kampuni na Mashirika ambayo Serikali inamiliki chini ya asilimia 50.(xi) Kupunguza
gharama za safari za nje kwa kupunguza ukubwa wa misafara na madaraja
ya kusafiria. Eneo hili la safari za nje limekuwa likiigharimu Serikali
fedha nyingi sana. Mheshimiwa
Spika, kufuatia hatua mbali mbali za kikodi tulizozichukua Kambi ya
Upinzani inapendekeza Bajeti ya shilingi trilioni 15 ambazo zitapatikana
kwa Mapato ya ndani ya shilingi trilioni 11.9 na misaada na mikopo ya
kibajeti ya shilingi trilioni 3.2 kama ilivyopendekezwa na Serikali.
Kambi ya Upinzani inapendekeza Serikali kutokukopa kibiashara ili
kudhibiti ukuaji wa Deni la Taifa.Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba Serikali itatumia
shilingi trilioni 9 katika Matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 6
kama Matumizi ya Maendeleo. Katika fedha za Maendeleo, asilimia 35 ya
Mapato ya ndani yameelekezwa huko kama ilivyoagizwa na Mpango wa
Maendeleo ya Taifa ulioidhinishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba.
SURA YA BAJETI MBADALA YA MWAKA 2012/2013
| MAPATO |
|
| A | Mapato ya ndani |
|
|
| i)mapato ya kodi (TRA) |
|
|
| ii)Mapato yasiyo ya kodi |
|
|
| B | Mapato ya Halmashauri |
|
|
| C | Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS) |
|
|
| D | Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo nay a kisekta |
|
|
| i)Misaada |
|
|
| ii)Misaada na mikopo kisekta |
|
|
| iii)MCC(MCA-T) |
|
|
| Jumla ya Misaada na mikopo ya kibajeti |
|
|
|
|
|
|
| JUMLA YA MAPATO YOTE. |
|
|
| MATUMIZI |
|
|
| E | Matumizi ya Kawaida |
|
|
| H | Matumizi ya Maendeleo |
|
|
| (i)Fedha za ndani |
|
|
| (ii)Fedha za Nje |
|
|
| Jumla ya matumizi ya maendeleo |
|
|
| JUMLA YA MATUMIZI YOTE. |
|
|
HitimishoFedha za RadaMheshimiwa Spika, Wakati
Kamati za Bunge zilipokaa kujadili taarifa ya Serikali kuhusu Mfumo wa
Mapato na Matumizi, Waziri wa Fedha na Uchumi alitoa Taarifa kuhusu
Fedha za Rada zilizorejeshwa, jumla ya shilingi 72.3 bilioni ambazo
zilipokelewa tarehe 26 Machi, 2012. Kwa mshtuko wa Wabunge, Waziri
aliiambia Kamati kuwa mchakato wa manunuzi ya vitabu na madawati kwa
kutumia fedha hizi ulikuwa umeanza chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu
TAMISEMI. Fedha hizi hazijawahi kupitishwa na Bunge lako tukufu. Kitendo
cha Serikali kuzitumia kabla ya kupitishwa na Bunge ni kuvunja sheria
za Fedha kuhusiana na masuala ya Bajeti. Wakati Waziri akiwasilisha
Hotuba yake hakugusia kabisa suala la fedha zilizorejeshwa kutokana na
Ununuzi wa Rada!Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inataka maelezo ya Serikali juu ya
Fedha hizi na utaratibu wa kuzitumia. Kambi inataka kufahamu vigezo
vilivyotumika kuteua mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam kutumia
fedha hizi. Kambi pia inapenda kufahamu Deni lililochukuliwa kununua
Rada hii iliyoleta kashfa kubwa sana hapa nchini limefikia kiasi gani
kulilipa na tukililipa tutakuwa tumelipa kiasi gani kwa ujumla.Mheshimiwa Spika, Uumbaji wa bajeti ya Serikali umekuwa ni ule ambao unapendelewa zaidi na wale wavivu wa kufikiri, yaani mfumo rahisi, wataalamu wanauita Incremental Budgeting.
Mfumo huu hujikita zaidi katika kutizama ukuaji wa mapato na kugawa
mapato hayo kwa mtindo wa nyongeza ya asilimia Fulani toka katika bajeti
iliyotangulia. Mfumo huu huacha kuzingatia mambo mengi mtambuka. Mfano,
tunaweza tizama sekta mojawapo ya umeme ambapo tukifanya uumbaji wa
bajeti kwa mfumo wa kiasi cha nyongeza (incremental budget) kuna thamani
halisi ambazo ukizitizama kwa bei wazi ya soko tayari zimepaa sana
ndani ya miezi kumi na miwili. Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani Bungeni, tukiwa ni serikali ambayo tunasubiri
kukabidhiwa dola, tunapendekeza kwamba ni vema tukaanza kutizama
uwezekano wa matumizi ya Zero Budgeting ambapo japo ni mfumo
ambao unahitaji kazi ya ziada, lakini una faida sana kwani hutizama
mipango ya matumizi kulingana na wakati uliopo huku ikifanya rejea ya
wakati uliopita.Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kwamba Bajeti za Mashirika ya Umma
ziwe sehemu ya Bajeti Kuu ya Nchi kwani kuna masuala mengi
yanayotekelezwa na Mashirika haya na Wananchi kupitia Bunge hawayajui.
Ni vema katika mfumo mpya wa Bajeti tutakaokuwa nao kufuatia mapendekezo
ya Spika wa Bunge ambapo kutakuwa na Ofisi ya Bajeti ya Bunge na Kamati
ya Bunge ya Bajeti, Sheria ya Bajeti (Fiscal Responsibility Act/Budget
Act) izingatie suala la kuziweka kama viambatisho Bajeti za Mashirika ya
Umma katika Bajeti ya Nchi.Mheshimiwa Spika,
Bajeti ya Serikali ya mwaka huu kama ilivyowasilishwa na Waziri wa
Fedha imewasahau kabisa wananchi wa vijijini na haina mkakati wowote wa
kuwakomboa watanzania walio wengi wanaoishi huko. Mipango mingi ya
kikodi katika sera ya Mapato ya Serikali itasaidia wakazi wa mijini
ambao ni asilimia 25 tu ya Watanzania wote. Mheshimiwa Spika,
Kambi ya upinzani inapenda kuweka msisitizo kwamba Tanzania bado ni
nchi ya Wakulima maana robo tatu ya Watanzania wanaishi vijijini ambapo
hawajui hizi hadithi za Uchumi kukua tunazoimba na kupewa sifa kila
siku. Hawa ni watu milioni 30 ambao hawana Maji, hawana Umeme, mazao yao
hayafiki sokoni maana hawana barabara nzuri, shule wanazosoma watoto
wao hazina walimu maana wanakimbia mazingira magumu. Hawa Watanzania wa
chini milioni 30 (The Bottom 30M) tunaowawakilisha hawana bima mazao
yakiharibiwa na wala hawana pensheni wanapokuwa wamezeeka na kupoteza
nguvu za kufanya kazi. Hawa ‘The Bottom 30M’ bado wanaishi maisha
walioshi babu zetu. Hawa Watanzania milioni 30 tumewasahau. Tunajenga
Mataifa mawili ndani ya nchi moja, moja la mafukara (wanavijiji) na moja
la wanaojiweza (wamijini). Mheshimiwa Spika,
Kama tunataka kujibu kitendawili cha kuwa na Uchumi unaokua kwa kasi
lakini haupunguzi umasikini inabidi kuelekeza nguvu zetu vijijini walipo
Watanzania wengi. Kukuza Uchumi wa Vijijini kwa kuwekeza kwenye misingi
ya kujenga uchumi imara ndio njia pekee ya kutokomeza ufukara wa
Watanzania.Mheshimiwa Spika, Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani mwaka huu ni Bajeti ya Ukombozi wa mwananchi. Licha
ya kwamba tunahitaji ukuaji wa kasi zaidi wa uchumi. Changamoto sasa ni
namna gani ukuaji huu wa uchumi unawafikia wananchi milioni thelathini
wa Vijijini na kuboresha maisha yao. Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano uliwasilishwa Bungeni na Serikali na kupata pongezi nyingi sana kutoka kwa waheshimiwa wabunge lakini cha kushangaza Serikali
hii ya Chama Cha Mapinduzi imeshindwa kuutekeleza kwa vitendo mpango
huu wa Taifa. Mwaka wa kwanza Mpango haukuwekewa fedha kwa kuwa ulikuwa
wa Mpito. Mpango unahitaji angalau shilingi trillion Nane kila mwaka ili
uwezekutekelezwa. Mpango ulipata shilingi trillion moja tu mwaka 2011/12. Mheshimiwa Spika, KWA KUWA Bunge liliazimia namna ya kuhakikisha tunapata fedha za kuendeleza nchi yetu sisi wenyewe, naomba kunukuu ukurasa wa 92 kifungu cha 4.3.1 katika Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano toleo la kiswahili kama ifuatavyo ‘kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35 ya makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo kila mwaka’ mwisho wa kunukuu.Mheshimiwa Spika, KWA KUWA katika makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2012/13 Serikali imetenga asilimia sifuri ya Mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia Bajeti ya Maendeleo.
Serikali hii imeshindwa kusimamia ahadi zake yenyewe kama inavyoonekana
katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano. Serikali hii ya CCM
imeshindwa kuheshimu Uamuzi uliopitishwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.Mheshimiwa Spika,
KWA KUWA Kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(c ) madaraka ya Bunge ni pamoja
na ‘Kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi
unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria
ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo”. Bunge liliidhinisha Mpango kwa
mujibu wa ibara tajwa ya Katiba.Mheshimiwa Spika,
KWA KUWA Bajeti ya mwaka 2012/13 iliyowasilishwa Bungeni na Waziri wa
Fedha na Uchumi haikukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo kama ambavyo
ulipitishwa na Bunge, HIVYO BASI, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali iiondoe (withdraw) Bungeni Bajeti
iliyoileta ili ikatayarishwe upya ili ikidhi matakwa (compliance) ya
Mpango wa Maendeleo kama ulivyoidhinishwa na Bunge na kusainiwa na Rais
wa nchi.Mheshimiwa Spika Naomba Kuwasilisha
………………………………………………….Kabwe Zuberi Zitto,MbWaziri wa Fedha na Uchumi Kivuli18.06.2012
SURA YA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2012/2013.
| MAPATO |
|
|
| A | Mapato ya ndani |
|
|
|
| i)mapato ya kodi (TRA) |
|
|
|
| ii)Mapato yasiyo ya kodi |
|
|
|
| B | Mapato ya Halmashauri |
|
|
|
| C | Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS) |
|
|
|
| D | Mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo na ya kisekta |
|
|
|
| E | Mikopo ya ndani |
|
|
|
| F | Mikopo yenye masharti ya kibiashara |
|
|
|
|
|
|
|
|
| JUMLA YA MAPATO YOTE. |
|
|
|
| MATUMIZI |
|
|
|
| E | Matumizi ya Kawaida |
|
|
|
| (i) Deni la taifa |
|
|
|
| (ii) Mishahara |
|
|
|
| (iii) Matumizi Mengineyo |
|
|
|
| Wizara |
|
|
|
| Mikoa |
|
|
|
| Halmashauri |
|
|
|
| H | Matumizi ya Maendeleo |
|
|
|
| (i)Fedha za ndani |
|
|
|
| (ii)Fedha za Nje |
|
|
|
| Jumla ya matumizi ya maendeleo |
|
|
|
| JUMLA YA MATUMIZI YOTE. |
|
|
|
TOFAUTI KATI YA BAJETI YA SERIKALI NA BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI
| Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani2012/2013 | Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 |
| Kukuza uchumi vijijini. | Mwelekeo na malengo ya Serikali hauleweki, hatua zilizochukuliwa ni koboresha uchumi wa mijini. |
| Njia mbadala zinazotekelezeka za kupunguza mfumuko wa bei. | Kuwa na njia zilezile zilizoshindwa mwaka wa fedha uliopita za kupunguza mfumuko wa bei. |
| Kunufaika
na mapato ya mitaji “Capital gains” kwa kutoza kodi kwa mali za kampuni
zilizopo nchini kwa mauzo yanayofanyika nje ya nchi na hivyo kupanua
wigo wa TRA kutoza kodi | Kutoza hisa kwa mauziano ya hisa pekee kwa mauziano yanayofanyika nje. Hisa inapunguza wigo wa TRA kutoza kodi. |
| Kupanua
wigo wa kodi ya tozo la ujuzi (SDL)kwa kuijumuisha serikali na
mashirika ya umma na kupunguza mzigo kwa sekta binafsi pekee. | Kupitia upya SDL bila kuonyesha namna itakavyofanyika. |
| Kupunguza misamaha ya kodi kutoka 3% ya sasa hadi 1% ya pato la taifa. | Kurudia ahadi zilezile za mwaka jana za kupitia upya misamaha ya kodi bila kuleta mrejesho wa kile walichokifanya. |
| Kuboresha kodi sekta ya madini ili kupelekea taifa kupata nagalau 25% ya mazuo ya madini nje kama mapato ya serikali. | Kutokuwa na hatua yoyote ya kuongeza mapato ya Serikali kutoka katika sekta ya madini. |
| Kulipa kima cha chini cha mshahara kuanzia shilingi 315,000. | Kulipa shilingi 170,000 kama kima cha chini. |
| Kulipa pensheni kwa wazee wote kuanzia miaka 60 na kuendelea | Kutokuwa na mfumo wa pensheni kwa wote. |
| Kushusha
kiwango cha chini kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE) kutoka 14% hadi
9% ili kumpunguzia mfanyakazi makali ya maisha na kutoza kodi zaidi
kwa watu wenye kipato kikubwa | Kubaki
na kiwango kilekile cha chini cha kodi ya 14% na kubakiza mfumo ule ule
wa kodi ya Mapato unaomfanya Masikini alipe zaidi ya Tajiri. |
|
|
| Kuziba mianya kwa makampuni ya simu kukwepa kutokulipa kodi ya mapato. | Kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi na hivyo kumwongezea gharama mwananchi. |
| Kuondoa mikopo ya kibiashara ili kulipunguzia taifa mzigo wa madeni | Kuendelea mikopo na hivyo kuongeza deni la taifa. mingi ya kibiashara. |
|
|
| Kutenga
asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maendeleo kama ilivyoelekezwa kwenye mpango wa maendeleo wa miaka
mitano. | Kutenga asilimia sifuri ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo na hvyo kutokutekeleza mpango wa taifa . |
| Utegemezi wa Bajeti 21.3% | Utegemezi wa Bajeti 42.37% |
|
|
|
|
|
|
JEDWALI LA ULINGANISHO WA ASILIMIA KWA BAJTEI MBILI
| UPINZANI |
| SERIKALI |
|
| Mapato ya ndani |
| Mapato ya ndani |
|
| Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS) |
| Mikopo na Misaada ya kibajeti (GBS) |
|
| Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na y a
kisekta |
| Misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na y a
Kisekta |
|
| Mikopo ya masharti ya kibiashara ya ndani |
| Mikopo ya masharti ya kibiashara ya ndani |
|
| Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje. |
| Mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje. |
|
| Matumizi ya Kawaida |
| Matumizi ya Kawaida |
|
| Matumizi ya Maendeleo |
| Matumizi ya Maendeleo |
|
| Matumizi ya maendeleo fedha za mapato ya ndani |
| Matumizi ya maendeleo fedha za ndani |
|
| Matumizi ya maendeleo fedha za nje |
| Matumizi ya maendeleo fedha za nje |
|