Kwa mujibu wa TBC1 katika taarifa ya habari ya saa mbili usiku leo July 19 2012, mpaka sasa idadi ya waliopoteza maisha kwenye ajali ya MV SKAGIT ni 68 ambapo baadhi ya maiti tayari zimetambuliwa na tayari majeruhi zaidi ya 100 walikua wamefikishwa hospitali huku watu ambao hawajaonekana wakiwa ni 91.
Mpaka jana usiku kwenye taarifa ya habari saa mbili usiku, ni watu saba pekee walioripotiwa kupoteza maisha kwenye ajali hiyo.
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar zimetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia July 19 2012 ambapo kituo cha mawasiliano kwa ndugu wanaohitaji kujua habari za ndugu zao waliopata ajali kwa upande wa bara ni ofisi ya mkuu wa mkoa Dar es salaam.
Kutoka bungeni ni kwamba wabunge wamekubaliana posho za leo (July19) hawatazipokea na badala yake zitapelekwa kama rambirambi kwenye ajali.
Spika wa bunge Anne Makinda ambae aliahirisha kikao cha bunge leo mpaka kesho amesema “tulikua tunaamini kwamba kutakua na mazishi ya halaiki lakini Serikali ya Mapinduzi imesema hapana mpaka sasa”
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini SUMATRA imesema cheti cha ubora cha meli hiyo kilianza tarehe 24 August 2011 na muda wake unaisha tarehe 23 2012 ambapo imefahamika kwamba meli hiyo ilisajiliwa na Mamlaka ya usafiri wa baharini Zanzibar (ZMA) na ilikua imepitishwa kubeba abiria 300 na mizigo isiyozidi tani 26 ambapo Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge William Lukuvi amesema meli ilikua imebeba watu 290, watu wazima ni 250, watoto ni 31 na wafanyakazi 9 wa meli.
No comments:
Post a Comment