Monday, July 23, 2012

Barua Ya Chadema Kwa Waheshimiwa Madiwani Wa CCM Na TLP, Manispaa Ya Arusha

Sisi Madiwani wa CHADEMA tumefikiri na kutafakari kwa kina kuhusu mustakabali wa maendeleo ya wananchi wa Manispaa ya Arusha Mjini. Kwa nafasi yetu ya wawakilishi na utetezi wa wananchi Arusha kwa umoja wetu ni vema tufikiri na tutafakari kwa kina kwa pamoja hasa kipaumebele ikiwa ni kutanguliza HAKI na MAENDELEO katika kumlenga kila mkazi wa aliyepo katika Halmashauri yetu. NI vema tukawa WAKWELI na WAZELENDO kwa wananchi wetu wa Arusha, huku wote tukijua kwa kina kile kilichotokea Arusha.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro wa Uchaguzi wa MEYA wa manispaa ya Arusha, ambayo ilitokana na ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi wa Meya ambayo akidi yake ilikuwa haijatimia. Ikumbukwe kuwa Mhe. Kivuyo ambaye katika sakata hilo alijikuta akichaguliwa kwa hila kuwa NAIBU MEYA, alifikia hatua ya kujizulu nafasi hiyi na kukiri mbele ya waandishi wa habari na wananchi wa Arusha kuwa uchaguzi uliofanyika haukuwa wa haki na yeye alipewa nafasi hiyo kwa hila, kitu ambacho baada ya tafakari ya kina aliamua kujiuzulu ili asiwe sehemu ya dhambi hiyo na kujikuta anakalia KITI CHA DAMU. Jambo hili pia limekuwa likisemwa na baadhi ya madiwani wa CHAMA CHA MAPINDUZI pindi tunapokutana nao kuwa mfumo wa chama cha CCM unazuia kuyatamka haya lakini ukweli ni kuwa huo uchaguzi wa meya uliofanyika na Mhe Gaudence Lyimo kupata nafasi hiyo ulikuwa batili kwa mujibu wa kanuni, lakini mbaya zaidi, umepelekea damu kumwagika, jambo ambalo ndio baya.

Wote tunashuhudia jinsi ambavyo mgogoro huu ulivyo na madhara makubwa sana kwa wananchi wetu na sisi pia ambao ni sehemu ya jamii hiyo hiyo. Mbali na kusababisha watu watatu kupoteza maisha,

pameendelea kutokea sintofahamu kubwa kutoka kwa wananchi jambo ambalo limeendelea kuzidisha hasira kwa wananchi kwa serikali. Jambo hili ni vema likafanyiwa kipimo maana mchezo huu na hila hii inaweza kuzaa balaa ambalo sio rahisi kulimudu tena.

Dharau na makusudi yanayofanywa na chama cha mapinduzi, mathalani Mhe Gaudence Lyimo na MKURUGENZI wa halmashauri katika kupuuzia wito wa CHADEMA kuwa HAKI haikutendeka, KANUNI zilivunjwa na hivyo uchaguzi wa MEYA ufanyike upya kwa kufuata kanuni sasa inafika mahali haivumiliki na hapo ndipo itakuwa mikononi mwa wananchi na sio CHADEMA tena.

Sambamba na hali hii, pia mgogoro huu unatumiwa na watendaji wa Halmashauri kufanya mambo yao yasiyo ya kiuadilifu kwani hakuna udhibiti wa kabisa katika uendeshaji wa halmashauri yetu. Waheshimiwa madiwani, katika ukweli huu, MKURUGENZI na huyo anayeitwa MEYA watatoa wapi ujasiri na kujiamini "moral authority" ili hali wao wameshiriki dhambi mbaya ya kuchakachua kanuni za kufanya uchaguzi wa meya isivyo halali na mbaya zaidi Mhe Gaudence kuendelea kung’ang’ania nafasi hiyo kwa kiwango cha damu ya watu kumwagika bila hata kujali??

Hata hivyo, hata kama Mhe Gaudence Lyimo hatajali wito huu ambao kwetu ni wito wa mwisho kwake na chama chake, jambo hili tunaliacha kwa MUNGU mwenye HAKI atashughulika nae kwa wakati wake na muda si mrefu tutapata majibu ya maombi yetu. Pili tunaliacha jambo hili kwa wananchi ili waamue kwa sababu wameshajua wazi kuwa Mhe Gaudence Lyimo na chama chake waliamua na wameendelea kuwafanyia uhuni katika mji wao. Sisi tumeliacha kwao waamue watakavyoamua.

Tunafahamu kabisa katika nafsi na mioyo yenu mnafahamu uchaguzi haukuwa halali lakini mnashindwa kusimamia ukweli kwa sababu ya ubinafsi na kukosa uzalendo kwa wananchi wa Arusha kwa kutanguliza maslahi yenu mbele, kitu ambacho tusingependa kipewe tafsiri hiyo

Tunawasihi kwa dhati kabisa tuamue kwa pamoja kwa manufaa ya Arusha tukubaliane kama viongozi wazalendo, wapenda maendeleo na wenye hofu ya MUNGU tufanye uchaguzi wa MEYA wa Halmashauri ya Arusha ambao utakuwa ni halali kwa vyama vyote.

Nchi nyingi za Afrika kumekuwa na vita vya wao kwa kwao kwa sababu ya uchu wa madaraka. Hili limetokea pia hapa Arusha watu wamekufa kwa sababu ya MEYA, hii ni aibu na ni dhambi kwa kung’ang’ania madaraka ambayo si haki.

Waheshimiwa madiwani wenzetu hata juhudi za serikali kufanya maendeleo wananchi wengi wa Arusha bado hawana imani na serikali yao kwa sababu ya MEYA tu. Hivi sasa kuna mradi wa ujenzi w barabara unaondelea ukweli ni kwamba jambo hili ni zuri lakini wananchi wanalibeza sana kama vile linafanywa kwa hila. Kwa nini iwe hivi??

Kimsingi tunataka MEYA ambaye yupo huru kutembelea kata zote kwa ajili ya maendeleo bila kujali itikadi ya chama chake. Hatutaki MEYA anayevizia misiba na harambee.

Mwisho tunamwomba Mh. Gaudence Lymo atafakari kwa kina kwa kumuomba MUNGU wake ampe hekima na ujasiri wa kuchukua maamuzi magumu ya kujiuzulu nafasi ya UMEYA na uchaguzi wa kidemokrasia ufanyike kwani utampa heshima na amani katika maisha yake yote.

Tunaomba Waheshimiwa Madiwani wenzetu kwa pamoja tuseme dhambi hii imetosha na tutubu kwa kufanya uchaguzi wa haki na Amani. Na kwa dhati kabisa yeyote atakayechaguliwa hata kama ni Mh. Gaudence tutampa ushirikiano wa dhati kabisa.

Tunaomba ushirikiano wenu katika jambo hili ambalo ni la msingi kwa maendeleo ya watu Arusha. Kila mmoja kwa imani yake aombee jambo hili kwani halitaki ushabiki linahitaji utulivu wa akili.

WAHESHIMIWA MADIWANI, FANYENI TAFAKARI YA KINA, ZINGATIENI JINSI WANANCHI KATIKA KATA ZENU WANAVYOWATAZAMA, ni matumaini yetu kuwa tutafanya uchaguzi wa MEYA ndipo tufanye uchaguzi wa Naibu MEYA. Na jambo hili litakuwa ni ushindi na sifa iliyotukuka kwa MADIWANI WOTE na sio kundi fulani la watu.
Asanteni sana
Doita Isaya Harri
Mwenyekiti madiwani wa CHADEMA
Nakala:
Katibu wa CHADEMA (M)
Katibu wa CCM (M)
Katibu wa TLP (M)
Mkurugenzi wa Halmashauri – Arusha Mjini

Odama: Mambo mazuri hayahitaji haraka


Msanii huyo ni mmiliki wa Kampuni ya J-Film 4 Life Production, alisema kwamba kuna mambo kadhaa ameamua kuyaweka kwanza sawa.

Ni yule  Mwigizaji na Mtayarishaji wa Filamu nchini, Jennifer Kyaka ‘Odama’ alisema kwa sasa anajipanga kwanza na hataweza kununua muswada ‘Script’ hadi hapo mapema mwakani.

Nia na dhumuni la msanii huyo kuanzisha kampuni yake ni, ilikuwa kuhakikisha anatoa kazi iliyokuwa bora na sio kulipua na hiyo itamsaidia kufanya vyema sokoni na kuweza kurudisha hata zile gharama za matengenezo.

Mbali na hilo msanii huyo hupokea kazi za wasanii wengine na kuzitengeneza, alidokeza mbali na hilo amekuwa akiwashauri hata wasanii wengine wanaotengeneza kazi kwake watoe kazi zenye ubora ambazo zitajikita zaidi kufunza, kuelimisha na kuiasa jamii zaidi ya kuburudisha.

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya akutana na Spika Makinda

 Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni mlezi wa Hospitali ya CCBRT Mhe. Anne Makinda akisalimiana na  Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Mhe. Jose Manuel Barroso alipowasili Hospitalini hapo jana kujionea shughuli za Hospitali hiyo. Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya umekuwa ukiichangia fedha nyingi hospitali hiyo.
                                            Rais Barosso akisaini kitabu cha wageni.
  Watoto Dema Emmanuel (6) na Goodson George (16) wakimkabidhi mgeni rasmi zawadi ya ‘gari’

Spika wa Bunge mama Anne Makinda na uongozi wa CCBRT Wakimuaga kiongozi huyo.
                                              Picha ya pamoja na wafanyakazi CCBRT

MMILIKI WA MELI YA SKAGIT NA NAHODHA WAKE MBARONI

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
Jeshi la Polisi Zanzibar linawashikilia wafanyakazi sita wa meli ya MV Skagit akiwemo mmiliki wake Bw. Said

Abdulrahman pamoja na Nahodha wa meli hiyo Bw. Mussa Makame Mussa na wanahojiwa kufuatia tukio la ajali ya meli hiyo

iliyosababisha vifo vya baadhi ya abiria  waliokuwa wakisafiri kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Bandari ya Zanzibar.

Watuhumiwa hao walikuwa wakihojiwa katika Ofisi za Upelelezi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi mjini Zanzibar ambapo Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, ACP Yusuph Ilembo, amesema watuhumiwa hao wawataweza kufikishwa

mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.Kamanda Ilembo amesema kuwa Makachero wa Jeshi la Polisi wanaendelea na uchunguzi na kutafuta taarifa nyingine
zinazohusiana na tukio hilo.

Hata hivyo, Nahodha wa zamu siku ya tukio hilo la kupinduka na kuzama kwa meli hiyo ya MV Skagit, Bw.Mussa Makame Mussa, ameelezea kwa ufupi jinsi ajali hiyo ilivyotokea na namna yeye alivyonusurika katika ajali hiyo. Amesema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya kupigwa na dharuba na mawimbi yaliyoambatana na upepo mkali, ambapo yeye alinusurika kufa maji baada ya kuruka kwa kutumia mlango wa mbele wa meli hiyo na kuanza kuogelea ambapo alijichanganya pamoja na na abiria wengine walionusurika na kuokolewa na vyombo vya uokozi.

Wakati huo huo, Wapiga mbizi wa Vikosi vya Ulinzi na usalama leo wamefanikiwa kuzupata maiti ngingine za watu watano akiwemo mwanamke mmoja na wanaume wanne.

Katika upekuzi wa maiti hizo, Makachero wa Polisi walibaini kitambulicho cha kupigia kura kutoka kwa mmoja ya mwili wa marehemu kitambulicho kilichokuwa na jina la Philip John Busiya aliyezaliwaq mwaka 1977 katika kijiji cha
Mapilinga kilichopo katika Kata ya Igokelo wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Kupatikana kwa miili hiyo mitano, kunaifanya idadi ya maiti kufikia 73. Maiti nyingine 68 zilipatikana siku za mwanzo baada ya kutokea kwa ajali hiyo ambapo kati ya hizo, maiti 54 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi.

Idadi ya miili ya watu waliopoteza maisha katika boti ya MV Skagit, imeongezeka kutoka 68 na kufikia 73, baada ya vikosi vya uokozi, kufanikiwa kuopoa miili ya watu watanao, katika eneo la tukio karibu na kisiwa kidogo cha Chumbe,
kilichopo pembezoni mwa mji wa Zanzibar.

Maiti hiyo iliyopewa namba 72, pamoja na maiti nyingine nne, zimezikwa katika makaburi ya pamoja ya Kama yaliyopo nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Eneo hilo la Kama pia lilitumika kwa kuwazika watu wengine waliokosa ndugu wakati wa ajali ya meli ya Spice Islander iliyotokea Septemba 9, mwakaja 2911.

Kupatikana kwa miili hiyo, kumetokana na juhudi zinazoendelea kwa kuvishirikisha vikosi vya ulinzi na usalama, wazamiaji wa makampuni binafsi pamoja na Mamlaka ya Bandari Zanzibar wakati wakiwa katika harakati za kuitafuta boti hiyo, ili kuweza kubaini kama kuna miili mingine iliyosalia kwenye Meli hiyo chini ya Bahari.

Aidha, juhudi za kutaka kuiibua Meli hiyo zinaendele ambapo wazamiaji wa JWTZ, Polisi, KMKM, JKU, Bandari na wale wa Makampuni binafsi na wale wa kujitegemea wakiendelea na kazi ya kutafuta mahali ilipo meli hiyo ili kuona kama

wataweza kupata miili mingine iliyonasa kwenye vyumba vya meli hiyo ambayo imekokotwa na maji kutoka eneo ilipozama meli hiyo.

Magazeti ya Leo Jumatatu 23rd 2012