Thursday, September 6, 2012

Siri Mauaji Iringa Zaanza Kufichuka


POLISI WALIOTEKELEZA OPERESHENI WADAIWA KUSAFIRISHWA KUTOKA MIKOA MINGINE, WAANDISHI WA HABARI IRINGA WASUSIA MKUTANO WA DCI MANUMBA
INADAIWA kwamba askari waliokuwa katika operesheni ya kuzuia mkutano wa Chadema katika eneo la Nyololo wilayani Mufindi, Iringa na ambayo ilisababisha kifo cha Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi walitolewa katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Mbeya.

Tayari tukio hilo limeibua mjadala mzito kiasi cha kumfanya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kuunda tume huru kubaini chanzo cha tukio hilo. Marehemu Mwangosi alizikwa juzi nyumbani kwao Tukuyu, mkoani Mbeya.

Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kuwa polisi hao kutoka mikoa hiyo mitatu wakiwa wamesheheni vifaa mbalimbali likiwamo gari la maji ya kuwasha, walisafiri siku moja kabla ya mkutano huo wa Chadema na baadaye kuzuka vurugu zilizosababisha kifo hicho.
Marehemu Mwangosi aliuawa kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu ambao ulisambaratisha vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.

Chanzo cha habari kutoka mkoani Dodoma kilisema: “Hapa kwetu kuna askari 10 na tunawafahamu kwa majina. Waliondoka hapa siku moja kabla ya tukio hilo wakiwa na gari la washawasha.”
Chanzo hicho kilisema kwamba awali, hawakuwa wakifahamu kama baadhi ya wenzao walichukuliwa na kupelekwa Iringa. “Tulikuja kuona kwenye gazeti picha na tulipofuatilia tukaelezwa kuwa ni kweli Dodoma ilitoa askari kwenda Iringa.”

Askari mwingine aliyekuwa katika operesheni hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, alikiri kuwa hadi jana baadhi yao walikuwa bado wako Iringa na kwamba walikwenda kwa agizo la wakubwa wake wa kazi.
“Sisi ni Watanzania, lakini tumelazimika kuyafanya hayo kwa sababu ya mkate (malipo). Kwa kweli haikuwa haki, kuwatoa askari na silaha kutoka mikoa mitatu kana kwamba wanakwenda kupigana vita!”

Alidokeza kwamba, askari wote waliotoka Dodoma walikuwa njiani kurudi mkoani humo, jana lakini gari la maji ya kuwasha liliendelea kubaki huko Iringa likiwa na dereva wake na askari mmoja mwenye cheo cha inspekta. Askari huyo alisema kwamba gari hilo lililazimika kubaki kutokana na hitilafu.

“Wengine wamerudi lakini, kuna wengine wenye gari la kuwasha bado walikuwa Iringa, gari lao limepata hitilafu kidogo,” kilisema chanzo hicho kutoka mjini Dodoma.

Mmoja wa askari hao alidaiwa kwamba hiyo inaweza kuwa moja ya sababu ya askari hao kumshambulia marehemu Mwangosi wakati mwenzao anayemfahamu akijaribu kuwazuia. "Hii inaonyesha kuwa askari hao waliompiga walikuwa hawamjui na huyu aliyekuwa akiwazuia, alimjua.”

Makamanda watupiana mpira

Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen hakukubali wala kukanusha na badala yake alisema: “Mambo yote hayo yanatakiwa kujibiwa na Kamanda wa Iringa.”
Aidha, alisema sakata la kifo cha mwandishi huyo kwa sasa liko katika vyombo vya uchunguzi hivyo asingekuwa tayari kulizungumzia.

“Siwezi kusema kama askari wangu walikwenda huko au hawakwenda, isipokuwa ninachoweza kusema ni kwamba suala hilo lipo katika vyombo husika hivyo waachiwe wao au Kamanda wa Iringa ndiye mwenye majibu.”
Alipotajiwa jina la mmoja wa askari aliyeonekana katika picha za video na magazeti za tukio hilo kwamba anatokea katika moja ya vituo vyake, kamanda huyo alisema: “Mimi yakitokea Dodoma nitazungumza wala siyo mtu mwingine kwa hiyo, mambo ya Iringa siwezi kuyazungumza na kama tutaanza kila Kamanda kuzungumza jambo hilo hamuoni kuwa itakuwa ni kama vurugu?”

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alipopigiwa simu yake iliita tu bila kupokewa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile alisema kwa kuwa tukio hilo limefanywa na polisi, mambo mengi yatazungumzwa lakini akasisitiza kwamba hajapeleka askari Iringa.
Alisema hakukuwa na agizo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi wala ombi kutoka Polisi Iringa kutaka askari wa kuongeza nguvu... “Taarifa hizo ni za uzushi kwani hazina ukweli wowote.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani alikanusha pia kuwapeleka askari wake Iringa akisema: “Hizo taarifa siyo za kweli. Hakuna askari yeyote aliyekwenda Iringa wakati wa vurugu zile.”

Mkutano wa DCI wavunjika

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema: “Hayo yote yameundiwa tume ngoja tuiachie ifanye kazi yake.”
Awali, DCI Manumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari mkoani Iringa, ambao hata hivyo, ulivunjika baada ya kutokea kutoelewana baina yao.

Manumba alitaka kueleza ripoti ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, lakini waandishi hao walikataa kumsikiliza wakisema hawauamini uchunguzi huo kwa kuwa ulifanywa na polisi peke yao.

Kabla Manumba, hajaanza kuzungumza, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Iringa (IPC), Frank Leonard alisema kutokana na msimamo wa waandishi wa habari wa mkoa huo hakutakuwa na uhusiano wa kikazi na polisi hadi pale tume zilizoundwa kuchunguza kifo hicho zitakapotoa taarifa sahihi juu ya mauaji hayo.

“Msimamo wetu ni kusitisha uhusiano wa kikazi baina yetu na jeshi la polisi hususan Mkoa wa Iringa, tumekuja hapa kwa sababu DCI umetuita na kama unataka kutupa taarifa ya kifo cha ndugu yetu basi waambie hao maofisa wa jeshi wa Iringa watoke nje,” alisema Leonard.

Akijibu madai hayo Manumba alisema: “Nia yangu ni kutoa taarifa ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, ndiyo maana niliwasiliana na mwenzenu ili tuweze kuzungumza, Polisi Iringa wataendelea kuwepo na waandishi wa habari mtaendelea kuwepo, matukio kama haya yapo na yataendelea kuwepo.”
Licha ya maelezo hayo, hakuna mwafaka uliofikiwa na mkutano huo ukavunjika.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili baadaye, DCI Manumba alisema: "Ni vyema wao wangenisikiliza kujua ninataka kuwaambia nini. Lakini, kwa kuwa kuna mkanganyiko, nimeona ni vyema jambo hili lisubiri tume ndipo watakuja kulizungumza.”

Waikataa Tume ya Nchimbi
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiponda tume ya Dk Nchimbi kikieleza kuwa imeundwa ili kurudisha uhusiano kati ya Polisi na waandishi wa habari na si kutafuta chanzo cha tatizo.

Juzi, Dk Nchimbi alitangaza kamati ya kuchunguza mauaji hayo inayoongozwa na Jaji Mstaafu, Steven Ihema na wajumbe, Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, Mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu.

Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu alisema Dar es Salaam jana kwamba: “Hii si tume ya kuchunguza mauaji, bali ina lengo la kurudisha uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari ili kuwasahaulisha wananchi kwa sababu imeundwa na waziri ambaye naye anatakiwa kuhojiwa.” “Tunamwomba Rais Jakaya Kikwete ateue tume kama anavyoelekezwa na Sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 1992, ambayo inaruhusu kumhoji yeyote kasoro yeye Rais.”

Lissu alisema Rais Kikwete angeunda tume hiyo na Waziri Nchimbi na IGP Said Mwema wanatakiwa kujiuzulu ili kupisha uchunguzi akidai kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba walitoa amri ya mauaji hayo.
“Dk Nchimbi anatakiwa kumuiga Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye alijiuzulu akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya kutokea mauaji, akijiuzulu atajijengea heshima tofauti na sasa kwani wananchi wamesikitishwa na mauaji hayo,” alisema Lissu.

Mwanasheria wa Chadema, Mabere Marando alidai kwamba kuna mkakati uliowekwa na Serikali wa kukidhoofisha Chadema baada ya kuonekana kwamba ni tishio kwa CCM.

Mbali na Chadema, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), pia limesema halina imani na kamati hiyo likisema imekuwa kawaida kwa Serikali kuunda tume ambazo hazileti ripoti kwa wananchi.
“Tume zimekuwa zikiundwa bila faida yoyote, huku zikipewa muda kuchunguza yaliyotokea lakini matokeo yake huwa hakuna ripoti wanayorudisha,” alisema Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya.

Kaaya alisema tume zimekuwa zikiundwa na kuigharimu Serikali fedha nyingi za walipa kodi, lakini ripoti zake zinaendelea kuwa siri.

Imeandikwa na Habiel Chidawali, Dodoma, Hamida Sharrif Morogoro, na Tumaini Msowoya, Iringa na
Lasteck Alfred na Juliana Malondo.

Tendwa Atamani Kuifuta CHADEMA

 Msajili wa vyama vya siasa nchini John Tendwa amesema sasa amechoka kusikia mauaji kwenye mikutano ya kisiasa ya CDM na atatumia rungu lake kufutia usajili chama chochote kitakachoshindwa kutunza amani ya nchi.Tendwa amewaambia waandishi wa habari hatishiki na chama chochote kuwa na wabunge kwani sheria inamruhusu kufuta chama hata kama kina wabunge 100.

Katika hali ya kushangaza Tendwa ameshauri vyama visubiri nyakati za uchaguzi ndipo vifanye mikutano ya kisiasa.Hata hivyo amekiri sheria inaruhusu vyama kufanya mikutano na maandamano wakati wowote.

Source:Habari Radio Tumaini.

CCM Yataka Uchunguzi Kifo Cha Mwangosi

Yataka usichukue muda mrefu
 Yataka ubaini pia mazingira ya kuuawa mwandishi huyo.
 Yatoa pole kwa wafiwa, Wanahabari na Watanzania.

NA MWANDISHI WETU, MWANZA
CCM imevitaka vyombo na tume zilizoundwa kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini kila kitu ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira yaliyosabaisha kipigo
hadi kufa mwandishi huyo.

Aidha imetaka uchunguzi usichukue muda mrefu ili ukweli kuhusiana na kadhia hiyo ujulikane mapema na hatua zichukuliwe kwa kila atakayebainika kuwa sababu au chanzo cha vurugu na kifo cha mwandishi huyo.

Aidha imesema imepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari watatu wa Polisi wakati wa vurugu hizo na kimetoa pole kwa wafiwa, wanahabari wote nchini na wote walioguswa na msiba huo kwa namna moja au nyingine.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye katika taarifa ya CCM kwa vyombo vya habari, leo jijini hapa, kuhusiana na sakata la vurugu hadi kifo cha mwandishi huyo, juzi mkoani Iringa.

"Itakumbukwa tarehe Septemba 2, 2012 katika operesheni za CHADEMA mkoani Iringa kulitokea vurugu zilizosababisha kuuawa kwa mwandishi wa habari mzoefu,nDaudi Mwangosi na kujeruhiwa vibaya kwa polisi watatu wa kikosi cha kutuliza ghasia. Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari hao", Nape alisema katika taarifa hiyo, na kuongeza:

"CCM inachukua nafasi hii kutoa pole kwa wafiwa, wanahabari nchini na wote walioguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine na tunatoa mwito kwa vyombo na tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza swala hili, vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini yote - ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira ya kifo cha ndugu yetu".

Alisema CCM inasikitishwa na mfululizo wa matukio ya watu kupoteza maisha au kujeruhiwa katika mikutano na operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na CHADEMA nchini hasa zile zilizofanyika kwa kukaidi amri halali za vyombo vya ulinzi na usalama.

Alikumbusha baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na lile la kuuawa kwa kada wa CCM Mkoani Singida, kuuawa kwa Ally Hassan mjini Morogoro na la juzi la kuuawa kwa Mwangosi Mjini Iringa, kujeruhiwa kwa askari polisi Iringa na matukio mengine mengi ambayo yametokea wakati CHADEMA wakiendesha operesheni zao mbalimbali nchini.

"Matukio haya si mazuri kutokea kwenye shughuli za Chama cha siasa. Kwakweli ni aibu, inayohitaji uwajibikaji,hata kama ni wa kisiasa. Inapotokea shughuli za chama chako zinasababisha kupotea kwa maisha ya watu kila unapozifanya na bado usitake kuwajibika, inahitaji roho ngumu na ujasiri wa aina yake" alisema Nape katika taarifa hiyo na kuongeza;

"Inakuwa mbaya zaidi pale vifo hivi vinaposababishwa na Chama hicho kutotii amri halali zilizotolewa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi inayovipa pia uhalali vyama vya siasa kuwepo na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria".

"Laiti Chama hicho kingesubiri siku chache zilizobakia kabla ya Sensa kuisha kabla ya kuendelea na mikutano yake ni dhahiri mauaji haya yasingetokea. Lakini kauli za kukebehi na uamuzi wa kukaidi amri ya Jeshi la Polisi na kusema "tupo tayari kwa lolote" ni ishara kwamba Chama hiki kiliandaa na kujiandaa na fujo zilizotokea", alisema Nape.

CCM imetoa mwito kwa vyama vya siasa na wanasiasa kwa ujumla kujenga utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria na kusema kwamba amani na utulivu vilivyopo nchini ni kazi nzuri iliyojengwa kwa muda mrefu na waasisi wa taifa la Tanzania kwa kujenga utamaduni wa kuzingatia utawala wa sheria.
Na Bashir Nkoromo

HUYU NDIO MWANDISHI ALIEJISALIMISHA POLISI MWENYEWE KATI YA WALE WATATU WALIOTANGAZWA KUSAKWA BAADA YA KIFO CHA MWANGOSI.

 Kwa sababu za kiusalama ilikua picha yake isiwekwe hapa lakini yeye mwenyewe ameidhinisha iwekwe kwa sababu haogopi, Francis Godwin ni huyo mwenye nguo nyeusi.
                                 Muda mfupi baada ya Marehemu Daudi kulipukiwa na bomu.

Siku mbili baada ya kifo cha mwandishi mwenzao wa habari (Daudi Mwangosi) aliefariki kutokana na kulipukiwa na bomu akiwa mikononi mwa polisi waliokuwa wanatawanya wafuasi wa Chadema huko Iringa, mwandishi wa habari Francis Godwin ambae alikua rafiki wa marehemu amejisalimisha polisi kufata masharti ya taarifa iliyotolewa kwa yeye na wenzake wawili kusakwa na polisi.

Exclusive na millardayo.com namkariri Godwin akisema “kutokana na hali halisi ya kushuhudia tukio la mauaji ya Mwangosi, nilifukuziwa kwa nyuma na gari lisilokua na namba pia nilipofika nyumbani niliambiwa kuna watu walikuja kuniulizia lakini hawafahamiki, na taarifa zikatoka kwamba tunasakwa”

Kuhusu kujisalimisha, Godwin amesema aliamua kufanya huo uamuzi baada ya kusikia taarifa za kusakwa kwake pamoja na waandishi wengine wawili, jana (september 5) aliamua kujisalimisha mwenyewe Polisi akiwa amesindikizwa na waandishi wa habari kama hamsini ambapo baada ya kufika pale walikutana na  kamishna wa makosa ya jinai Tanzania Robert Manumba ambae ilibidi ahoji polisi Iringa kama ni kweli wanamtafuta Godwin na wenzake.

Namkariri Godwin akisema “baada ya kumuuliza mmoja kati ya maofisa wake kama ni kweli wanamtafuta Godwin ofisa huyo alijiumauma na baadae akasema hatumtafuti, baada ya hapo waandishi wa habari tulisimama tukaondoka kwa sababu ya kutokubaliana na kilichotaka kuendelea kuhusu taarifa ya uchunguzi ya Manumba”

Kingine kilichoendelea baada ya hapo ni Club ya waandishi wa habari Iringa kuziomba redio mbalimbali za iringa ambazo zimekua zikirusha matangazo ya polisi jamii kusimamisha matangazo hayo ambapo wamiliki wa vyombo hivyo wamekubali ombi.

Francis Godwin ambae alikua karibu na marehemu Daudi Mwangosi muda mfupi kabla ya kuuwawa kwa bomu amesema “Nilijua kwamba mimi ni miongoni mwa waandishi watatu wanaotafutwa kwa sababu marehemu kabla ya kifo akiwa amekamatwa nilitaka kwenda kumuokoa pale lakini nilipokua namsogelea Daudi akaniambia Godwin mdogo wangu kimbia… wakati nakimbia kama hatua 20 mbele nyuma nageuka nasikia mlipuko mkubwa, kuangalia ni Wangosi amekufa na nilibahatika kupiga baadhi ya picha ambapo askari waliokuwepo walipoona narudi kwenye eneo hilo walinionyeshea bunduki ikabidi ninyooshe mikono juu kwamba jamani mimi nakuja kwa heri wakaniambia potea”

Godwin amesema baada ya kugeuka na kuanza kukimbia walianza kumfukuzia ila bahati nzuri gari yake ilikua mbali, baada ya kutishwa na polisi walipokwenda hospitali ulipopelekwa mwili wa marehemu ilibidi waanze kutoa mabango ya wanahabari yaliyobandikwa kwenye gari yao pamoja na kutoa namba za gari, alianza safari ya kuondoka lakini kuna gari zilikua zinamfukuzia kwa nyuma mpaka alipofika nje kidogo ya mji wa Iringa na kuingia mitaani ndio akafanikiwa kukimbia.

Kwenye sentensi ya mwisho Godwin anasema ameibiwa siri na askari mmoja ambae alimwambia kuhusu kutafutwa kwake yeye na waandishi wa habari awengine mbapo alimuonya kwamba msimamo na kauli aliokua ameutoa pamoja na ushahidi wa tukio la mauaji ndio vimefanya atafutwe.

by MillardAyo in News

Magazeti ya Leo Alhamisi 6th September 2012