Thursday, May 23, 2013

SHEHA WA TOMONDO- ZANZIBAR ALIYEMWAGIWA TINDIKALI JANA USIKU

Sheha Mohammed Omary Said aliyemwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana akiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja Unguja akipatiwa matibabu, Sheikh Mohammed amepata maumivu makali sehemu za kifuwa na jicho kuumia

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi,Mukhadam Khamis,amesema chombo kilichotumika kumwagia tindikali Sheha huyo kilipatikana eneo la tukio na kwamba polisi imekichukua kwa kukichunguza kitaalam ili kugundua aliyekuwa akikitumia kwa kuangalia alama za vidole.

Sheha huyo alimwagiwa tindikali jana usiku wakati alipotoka nje ya nyumba yake kuchota maji na ndipo mhalifu huyo alipomwagia tindikali na kwamba hakuweza kumtambua.

Sheha Mohammed Kidevu akiwa katika wodi ya Hospitali kuu ya Rufaa Mnazi Mmoja akipata matibabu ya majaraha ya kitu kinachosadikiwa kwa Tindi Kali,akipata matibabu hayo katika hospitali hiyo.

RAIS KIKWETE ATANGAZA VITA KUHUSU VURUGU ZA MTWARA.....AMESEMA SERIKALI YAKE ITAWASULUBU WACHOCHEZI WA VURUGU

WAKATI hali ikizidi kuwa tetea Mkaoni Mtwara kufutia Mapigano yaliyoanza jana Mkoani humo Rais Kikwete amevunja ukimwa wake na kutoa amri  wahusika wakuu wa tukio hilo kusakwa mara moja.

Akizungumza katika eneo la Kizota, Dodoma wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Dodoma kwenda Iringa, Rais Kikwete  alisema wote waliohusika na vurugu hizo watasakwa na kuchukuliwa hatua kali.

Rais Kikwete alisema rasilimali inayopatikana mahali popote pale nchini inatakiwa kutumiwa na Watanzania wote... “Hivi watu wa  Nyarugusu wadai dhahabu ya pale au kinachopatikana Chalinze basi kisitumiwe na watu wa Morogoro! Hivi tutakuwa na taifa kweli?,”  alihoji kwa ukali Rais Kikwete.

ASKARI ALIYENASWA NA MAGUNIA 18 YA BANGI HUKO HIMO AWATOROKA POLISI

ASKARI Polisi Koplo Edward, anayedaiwa kusafirisha dawa za kulevya (bangi) gunia 18 huko Himo, Kilimanjaro tarehe 18, Mei 2013, ametoroka chini ya ulinzi wa askari polisi saba na kutokomea kusikojulikana.

Mtuhumiwa huyo alikuwa dereva wa gari aina ya Toyota Landcruiser namba PT. 2025 la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema askari huyo akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi saba, walikwenda nyumbani kwake kwa ajili ya ukaguzi, na walipofika nyumbani kwa  mtuhumiwa, walimwamini na kumwacha kuingia ndani peke yake nao waliingia ndani ili kuendelea na upekuzi, na ndipo mtuhumiwa alipofungua mlango wa nyuma ya nyumba yake na kukimbia bila ya wao kufanikiwa kumkamata

Alisema polisi imemkamata Inspekta wa Polisi Izaack Manoni aliyekuwa anasimamia upekuzi huo: “Inspekta Manoni yupo chini ya ulinzi na hatua za kinidhamu dhidi yake zitachukuliwa,” alisema ACP Sabas na kuongeza: 

“Mtuhumiwa Edward, anayetafutwa kwa sasa alishafukuzwa kazi, akipatikana atafikishwa mahakama ya kiraia kusomewa mashitaka ya kufanya biashara ya dawa za kulevya,” alisema.

Alisema tayari mtuhumiwa mwenzake ambaye ni askari polisi mwenye namba G. 2434 PC George, amesomewa mashitaka yake jana.

Mbali na mtuhumiwa huyo, watuhumiwa wengine waliokamatwa na magunia 30 ya bangi wilayani Arumeru nao wamepandishwa kizimbani kusomewa mashitaka yao.

via gazeti la MTANZANIA

Magazeti ya leo Alhamisi 23rd May 2013





MKURUGENZI WA MASHITAKA NCHINI ATAKA LWAKATARE ASHITAKIWE KWA UGAIDI TENA

MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, amewasilisha ombi katika Mahakama ya Rufaa nchini, akiomba itengue uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wa kumfutia mashitaka matatu ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.

Dk. Feleshi aliwasilisha ombi hilo juzi kwa njia ya maandishi, ambapo katika maombi yake anaiomba mahakama hiyo iitishe mwenendo wa shauri lililotolewa uamuzi huo na Jaji wa Mahakama Kuu, Lawrence Kaduri Mei 8, mwaka huu na kuupitia upya na ifute uamuzi huo kwa kuwa una makosa kisheria.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Dk. Feleshi anadai Mahakama Kuu haikuombwa kumfutia mashitaka Lwakatare kama Jaji Kaduri alivyotoa uamuzi huo, bali aliiomba mahakama iitishe majalada ya kesi ya msingi iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18 na 20 mwaka huu.

RASLIMALI ZA NCHI NI MALI YA TAIFA ZIMA....WALIOANDAMANA HUKO MTWARA TUTAWASHITAKI'... RAIS KIKWETE

                                                    Polisi wawasaka waandamanaji Mtwara
Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewaonya watu wanaosababisha uvunjifu wa amani nchini humo kuwa watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Onyo hilo linafuatia ghasia ambapo ofisi kadha, maduka na nyumba zimechomwa katika mkoa wa Mtwara ulioko kusini mashariki mwa Tanzania jana

Akihutubia kupitia televisheni ya taifa, TBC1, Rais Kikwete amesema wale waliokamatwa na polisi wakati wa ghasia hizo watashitakiwa.

Ghasia hizo zilianza muda mfupi baada ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni. Akizungumzia madai ya waandamanaji hao, Rais Kikwete amesisitiza kuwa raslimali za nchi ni mali ya taifa zima.

BUNGE LAAHIRISHWA TENA LEO MPAKA UFUMBUZI WA GESI MTWARA UTAKAPOJULIKANA


 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Anna Makinda ameliahirisha tena bunge leo asubuhi ili kupisha kamati ya uongozi ya Bunge iendelee kukutana ili kutoa maamuzi na tamko kuhusu vurugu za Mtwara zilizojotokeza jana na kusababisha mtu mmoja kufariki dunia na uharibifu mbalimbali kutokea ikiwemo kuchomwa moto nyumba za viongozi wa serikali,chama cha mapinduzi na nyumba ya mwandishi wa habari wa TBC.
Pia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini umesimamishwa kwa muda mpaka ufumbuzi wa tatizo la vurugu hizo utakapopatiwa suluhisho.

Kesho bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Afrika Mashariki itajadiliwa.