Monday, October 15, 2012

FUJO UWANJANI KWENYE MECHI.



 Wachezaji mbalimbali akiwemo Yaya Toure wakilindwa na kuondolewa uwanjani baada ya mashabiki wa Senegal kuvamia uwanja kwa kukasirishwa na maamuzi ya refa kuwapa penati Ivory Coast ambapo Didier Drogba alifunga goli la pili.



                          Mpaka mpira unavunjwa Ivory Coast walikua wameifunga mbili bila Senegal.


      Mashabiki wakisaidiwa kushuka kuingia uwanjani baada ya fujo kuzidi kwenye ngazi za juu za uwanja.
Unaweza kuangalia Mechi hii ilivyokuwa.

Magazeti ya leo Jumatatu 15th October 2012

























Mukama Aikamua CHADEMA...!

 *Asema inakabiliwa na ukame wa viongozi waliopikika kimaadili
 * Hata kupata wagombea hutegemea 'iokoteze' walioshindwa michujo au chaguzi za CCM
* Asena kwa mtaji huo haiwezi kuwa chama chenye tija na hatma njema kwa taifa.



 KATIBU Mkuu wa CCM, Wilson Mukama amesema Chadema hakiwezi kuwa chama chenye tija na hatma njema kwa taifa kutokana na kulazimika kuokoteza hata wagombea wake kutokana na wanaoshindwa kwenye michujo au chaguzi ndani ya CCM. Alisema, Chadema na vyama vingine vya upinzania hapa nchini, vinazama katika hali hiyo, kutokana na kutokuwa na tanuru imara linalowawezesha kutoa viongozi waliopikika kimaadili, kama ilivyo ndani ya CCM. Amesema, Chadema wanaposema, kwamba kwa CCM kutowafukuza au kuwanyima uongozi baadhi ya wana-CCM ni kuizika CCM, huko ni kulia kinyume kwamba kwa kutofanya hivyo CCM imewakosesha watu ambao wangehamia kwao hivyo chama chao kinakufa.

Mukama alisema hayo jana wakati wa sherehe ya kuwapongeza wana-CCM Kata ya Msasani kwa kukamilisha chaguzi zao ndani ya chama katika kata hiyo, iliyofanyika kweny6e ukumbi wa Maisha Club, Msasani jijini Dar es Salaam. Mukama alisema, CCM ni taasisi iliyojengwa katika misingi imara na mshikamano wake ni kama ngumi inayoundwa na vidole vitano na kitaendelea kuwa imara kwa sababu viongozi wake wanatokana na tanuru lililowapika kimaadili wakapikika.

 "CCM bwana ni tasisi yenye viongozi wenye chimbuko la maadili, siyo kama vyama vingine vinaongozwa na wenye vilabu vya usiku halafu eti navyo ni vyama vya kuweza kuongoza nchi", alisema Mukama. Alisema kutokana na CCM kuwa chama chenye chimbuko la maadili bora, ndiyo sababu kila kinapofanya uchaguzi wa kupata viongozi wake huwa ni wa kihistoria kwa kuwa anayepenya kuwa kiongozi huwa amepita kwenye tanuru la uchujwaji wa hali ya juu.

 "Juzijuzi tulipokuwa tunateua majina ya wagombea, Kamati yetu ya maadili, haikuacha kuchunguza hatua kwa hatua na kwa makini kama kila aliyeomba uongozi anazo sifa bora na zinakidhi viwango vya kushinda anayetakiwa kuondolewa yeye abaki, hivi ndivyo chama chenye misingi ya uadilifu ya uongozi kinavyokuwa", alisema Mukama na kuongeza:- "Sasa hivi vyama vingine vinaweza kufanya mchujo wa aina hii? thubutu.

Si mlisikia juzi juzi mbunge mmoja alijaribu kuonyesha nia ya kutaka uenyekiti wa Chama fulani, wee mliona alivyofurumushwa". Mukama alisema, wanaosema CCM inakufa ni wavivu kufanya tathmini au wanasema hivyo kudanganya watu na nafsi zao huku wenyewe wakiwa wanajua kwamba CCM ni imara tena kwa vigezo.

 "Hivi jamani tujiulize na wao (wapinzani) wakitaka pia wajiulize chama chenye mwelekeo wa kufa kinaweza kupata wagombea ambao ni Wazee, Vijana kina baba na kina mama tena wengi wasomi kabisa waliobobea hadi ngazi za uprofesa, wanaokanyagana kwa wingi kama tulivyoona wakiomba uongozi katika nafasi mbalimbali? ", alihoji Mukama. Alisema, tutokana na hali ya uchaguzi ndani ya Chama iliyojionyesha katika ngazi za mikoa, baada ya kumalizika ngazi ya taifa, CCM itakuwa itakuwa imara zaidi tayari kwa kutwaa dola tena baada ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Katika hafla hiyo, wanachama wa Kata hiyo, waliuopongeza uongozi wa juu wa CCM kwa namna ulivyoweza kuweka taratibu zilizo wazi na za haki katika kuhakikisha uchaguzi ndani ya chama unazaa viongozi walio dhabiti. Mapema, Mukama alikabidhi hati kwa vijanan na makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM, ambao wameshiriki katika shughuli mbali mbali za kuimarisha chama kwa namna moja au nyingine.
 NA BASHIR NKOROMO

Makongoro Aanguka Usiku Wa Nyerere

ASHINDWA KUTETEA KITI MARA, AMPA ANGALIZO MSHINDI, TARIMBA ATAMBA DAR, WAMBURA ATUPWA MAKONGORO Nyerere ameadhimisha vibaya kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha baba yake, Mwalimu Julius Nyerere baada ya kuangushwa kwenye uchaguzi wa kuwania Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara uliofanyika juzi na kumalizika usiku wa kuamkia jana. Jana ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 13 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga yaliyokwenda sanjari na kuzimwa kwa Mwenge wa Uhuru.

Katika uchaguzi huo wa Mkoa wa Mara, Makongoro aliyekuwa akitetea kiti hicho, alipata kura 422 na kuzidiwa na mpinzani wake wa karibu, Christopher Sanya aliyepata kura 481 huku tisa zikiharibika. Uchaguzi huo ilibidi urudiwe kwa kuwashindanisha wagombea wawili, kwani katika awamu ya kwanza wagombea wote hawakupata nusu ya kura kama kanuni za chama hicho zinavyotamka.

 Awali, katika nafasi hiyo wagombea walikuwa watatu. Katika awamu ya kwanza, Sanya alipata kura 469, Makongoro (402) na mgombea mwingine, Enock Chambiri aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara alipata kura 144. Baada ya matokeo hayo ya awali, Chambiri aliondoka ukumbini hapo. Matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa, yalitangazwa na Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Nazir Karamagi.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Makongoro alisema kuwa anakubaliana na matokeo hayo na kumuasa mshindi kufanya kazi kwa mujibu wa katiba. Pia alimtaka mshindi huyo kuvunja makundi aliyosema yameshamiri ndani ya chama hicho.

 “Naomba uwe mwadilifu, Mkoa huu wa Mara ni mgumu sana kuufanyia kazi. Kazi ya uenyekiti siyo lelemama, hii ndiyo nafasi kubwa ambayo itatusaidia katika uchaguzi wa 2015.” “Wewe ndiye kiongozi mkuu wa mkoa huu wa kupanga uongozi katika uchaguzi mkuu hivyo ukishindwa tutayumba, tunaomba utoe ushirikiano na ukemee hii dhambi ya kukata majina, kwani inaweza ikaingia kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa.”

 Waliochaguliwa katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri ya Mkoa kupitia wilaya ni Josephat Seronga, Ester Nyarobi, Zuhura Makongoro, Jackson Waryoba, Josephat Kisusi na Felister Nyambaya. Wengine ni Grace Bunyinyiga, Thabita Idd, Abdallah Jumapili, Kananda Kananda, Mariam Mkono na Samson Gesase. Katika nafasi ya uenezi, Maximillian Ngesi amefanikiwa kutetea nafasi yake kama ilivyokuwa kwa Katibu wa Uchumi na Fedha, Marwa Mathayo.

  MWANANCHI

Tanzania Yapata Shujaa Mwingine

                                                  Wilfred Moshi safarini kuelekea kileleni.
                                 
                                          Wilfred Moshi akipeperusha bendera ya Tanzania kileleni Mlima Everest
 Mh Peter Kallaghe akiwa katika picha ya pamoja na timu nzima ya TWENDE PAMOJA. Kutoka kushoto Lee Patterson, Mike Knox (Director) Wilfred Moshi, Mary Iannarelli, Fiona Macpherson na Veronica Avinou

Imeandikwa na Freddy Macha kwa ushirikiano na Urban Pulse

Picha zote Ihsani ya Wilfred Moshi na Urban Pulse

 Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi yetu kijana Wilfred Moshi, Mbongo wa kawaida tu (anayefanya kazi ya upagazi kuwahudumia watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro), ameweka rekodi mpya ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda Everest - mlima mrefu kushinda yote duniani.

 Hivi karibuni, Moshi,   alialikwa majuma matano nchini Uingereza kutembelea shule mbalimbali za Scotland akakutana na takribani wanafunzi 5,000 .
Wanafunzi walitaka kufahamu namna alivyopanda mlima Everest wenye mita 8,848 (futi 29, 029). Mlima huu mgumu kuukwea kuliko yote ulimwenguni umewahi kupandwa na na watu 4,000 toka ulipoanza kufikiwa kileleni na Edmund Hillary na Sherpa Tenzig Norgay mwaka 1953. Kati ya hao 200 walifariki. Mwaka huu wanne wameshafariki wakiijaribu shughuli hii inayochukua   miezi miwili na kugharimu Dola 100,000 (Shilingi milion 157,500,000) Linganisha na mlima Kilimanjaro unaodai  siku tano na gharama (ikiwepo vifaa husika) Dola 2,000 (Shilingi milioni 3, 161).

Wilfred Moshi ni Mtanzania wa kwanza na Mwafrika wa tatu kufikia kilele cha kitendawili hiki   (kilichoitwa “Chomolungma” na wenyeji kabla ya kubatizwa jina la Everest na Waingereza enzi za ukoloni)  Mei 19, mwaka huu.
Wilfred aliyezaliwa mwaka 1979 na kumaliza kidato cha sita shule ya Kilimanjaro Boys, amekuwa akipanda mlima Kilimanjaro tangu angali bado shuleni na miaka 19.
Mara baada ya kuwasili Edinburgh, Scotland alikaribishwa bungeni akakutana na Waziri wa Sheria mheshimiwa Kenneth MacAskill na viongozi wengine. Safari ilikirimiwa na shirika la “Twende Pamoja” lililoanzishwa na Mike Knox miaka 30 iliyopita. “Twende Pamoja” imejenga ushirikiano kati ya wanafunzi wa Scotland na shule 34   za Kitanzania. Ni moja  ya mashirika, watu binafsi  na wafadhili mbalimbali ulimwenguni waliochangia fedha za kumwezesha Moshi kupanda mlima Everest.

Balozi wetu Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe vile vile alisafiri toka London kumtembelea Wilfred Moshi na kumpa heko. Umbali wa London had Scotland ni kama Dar es Salaam hadi Kigoma!

Kwanini Moshi anahusudu kupanda milima?
Ukweli sisi bado hatuoni umaana (au umuhimu) wa kupanda milima. Anasema lengo lake lilikuwa kutimiza ndoto ya Mtanzania wa kwanza kupanda Everest. Pili, upandaji milima ni moja ya njia zinazoweza kusaidia kujenga jamii kwa misaada na fadhila za mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO). Tujiulize vipi alisaidiwa na watu wengi namna hiyo kuchangia fedha takikana? Tatu, Moshi amethibitisha ukiwa na moyo na jitihada unaweza kufanya lolote. Ushujaa na ushupavu wake utasaidia kuwahamasisha Watanzania kuwa ukitaka kufanya jambo lolote lile unaweza ili mradi uwe na moyo na nidhamu.

Mpanda milima mashuhuri, Mike Hamill, aliyeshakwea milima yote   mikubwa saba duniani anasema katika kitabu chake kipya (“Climbing Seven Summits”) wapanda milima ni watu wenye moyo wa kufikia malengo na kufanikiwa katika maisha yao.
 Akiwa Uingereza Moshi alipanda mlima wa Ben Nevis  mrefu kuzidi  nchi hii-  wenye mita 1,344 (futi  4, 409). Baada ya kuimudu milima mitatu sasa , Wilfred Moshi ameazimia kupanda milima  katika mabara yote 7 duniani. Anasema amebakisha milima mitano: Aconcagua ( Marekani ya Kusini ), Kosciuszko (Australia), Vinson Massif ( Antarctica) McKinley(Alaska) na  Elbrus(Urusi).

Mungu ambariki Mtanzania huyu mwenye jazba na hamasa anayetuletea sifa.
Soma habari zaidi:
http://wilfredmoshi.wordpress.com/

Mwili Wa Kamanda Barlow Kuagwa Leo

Mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (52), utaagwa leo, Oktoba 15, 2012, katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa jeshi hilo mkoani humo Lilian Matola, imesema kwamba shughuli ya kuaga mwili huo itaongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inpsekta Jenerali Saidi Mwema.

Matola alisema kwamba, viongozi wengine wa kiserikali watakaoshiriki ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi, Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo, wakuu wa wilaya na viongozi waandamizi wa jeshi hilo.

 Alisema kuwa shughuli za kuaga zitaanza saa 3:00 asubuhi baada ya mwili kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na kupelekwa kwanza nyumbani kwake Pasiansi. Baadaye saa 4:00 hadi saa 6:00 mchana itafanyika Ibada ya kumuombea kabla ya kusomwa kwa wasifu wake na salamu kutoka kwa IGP, Makamanda wa mikoa mingine na viongozi mbalimbali vya Vyama vya siasa.

Matola alisema kuwa, mwili wa marehemu Barlow utasafirishwa mchana kwenda jijini Dar es Salaam ambako taraibu nyingine za kuomboleza zitafuata kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa taratibu za maziko.