Saturday, July 28, 2012

NGORONGORO HEROES YAWAAHIDI USHINDI WATANZANIA

Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) imeahidi ushindi kwenye mechi yake dhidi ya Nigeria (Flying Eagles) itakayochezwa kesho (Julai 29 mwaka huu).

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Algeria itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo (Julai 28 mwaka huu) ofisi za TFF, Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen na nahodha wake Omega Seme wamesema timu yao iko tayari kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Kenya.

Michelsen amesema timu yake imepata mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Rwanda, lakini pia aliishuhudia Flying Eagles ikicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) uliofanyika Julai 24 mwaka huu jijini Kigali.

“Timu iko vizuri na wachezaji kama Frank Domayo, Simon Msuva na Ramadhan Singano ambao pia wanachezea timu A (Taifa Stars), hivyo uzoefu wao ni muhimu kwa mechi ya kesho.

“Nigeria ni mabingwa watetezi wa michuano hii kwa hiyo tunatarajia upinzani mkubwa, lakini tumejiandaa kwa hilo. Nigeria ni nchi yenye mfumo mzuri wa timu za vijana, na sisi tunaelekea huko huko” amesema Michelsen.

Naye Kocha Mkuu wa Flying Eagles, John Obuh amesema haijui vizuri Ngorongoro Heroes lakini anaiheshimu kutokana na ukweli kuwa inacheza raundi ya pili baada ya kuitoa Sudan katika raundi ya kwanza.

“Sina mchezaji yeyote anayecheza mpira wa kulipwa nje ya Nigeria, lakini tumekuja kushinda ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza raundi ya mwisho na hatimaye tucheze fainali mwakani,” amesema Obuh aliyefuatana na nahodha wake Samuel Okan ambaye ni mlinda mlango.

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Moses Osano ni sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A ni sh. 10,000.

Osano atasaidiwa na Peter Keireini na Elias Wamalwa wakati mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Thomas Onyango. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Charles Masembe kutoka Uganda.

CAF YAMTEUA HAFIDH ALI KUSIMAMIA MECHI YA WASUDAN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua mwamuzi wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Hafidh Ali kuwa Kamishna wa mechi kati ya El Ahly Shandy na Al Hilal zote za Sudan.

Shandy ndiyo mwenyeji wa mechi hiyo namba 98 ya Kombe la Shirikisho itafanyika Agosti 5 mwaka huu na itachezwa Uwanja wa Shandy ulioko katika mji wa Shandy.

Mwamuzi wa mechi hiyo ni Raj Seechun kutoka Mauritius ambaye atasaidiwa na Balkrishna Bootun, Jean Daniel Telvar na Parmendra Nunkoo, wote pia kutoka Mauritius. Mratibu Mkuu wa mechi hiyo ni Paul Bassey wa Nigeria.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Bunge Lanuka Rushwa(Fedha za mafisadi zawatokea puani wabunge)

BUNGE jana liliwaka moto baada ya baadhi ya wabunge kuwanyooshea vidole wenzao kwa madai kupokea rushwa kwa lengo la kuwapigia debe mafisadi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaowafilisi Watanzania.

Wabunge hao wanadaiwa kuwaunga mkono mafisadi ili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wake, Eliakimu Maswi, waonekane hawafai.

Akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti kwa wizara hiyo jana, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), alisema kwa wiki nzima waziri na watendaji wake walikuwa wakidhalilishwa na baadhi ya watu kwa kupitia wabunge wakitaka Rais Jakaya Kikwete awaondoe kwa madai kuwa walikiuka sheria ya manunuzi ya umma na kuipa zabuni kampuni ya PUMA Energy.

“Mheshimiwa mwenyekiti baadhi ya makampuni ya mafuta yalikuwa hapa Dodoma na kutoa chochote kwa wabunge na hili si kwa upande wa serikali ya CCM bali wabunge wa pande zote tukiwemo wapinzani. Msione watu wanazungumza kwa nguvu hapa kutetea, hawa wamepewa chochote,” alisema.

Huku akishangiliwa na karibu wabunge wote, Selasiani alisema wanaohoji kuwepo ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma anawashangaa kwani katika jambo la msingi lazima uamuzi uwe mgumu huku akitolea mfano wa Yesu Kristo alivyoivunja Sabato aliyoiweka mwenyewe.

“Mheshimiwa mwenyekiti Maswi ametishwa tunajua hilo, ametumiwa meseji za vitisho, ameombwa rushwa na baadhi ya wabunge wenzetu hapa. Tunawajua wako wabunge wanafanya biashara na TANESCO, lakini humu waongea kwa nguvu na jazba wakijifanya watetezi wa wananchi kumbe ni nguvu ya rushwa,” alisema.

Selasini alimtadharisha Waziri Muhongo kuwa yeye ni msomi asiyetokana na siasa hivyo hawajui wanasiasa lakini ni vema afanye kazi kwa nguvu bila kutetereka na atawazoea.

Mbunge huyo pia alipendekeza sheria ya wahujumu uchumi irejeshwe ili wahusika wakiwemo wabunge waliohusika katika sakata hilo wahukumiwe kama wahaini.

“Wako wenzetu humu wamekuwa wakijifanya wapambanaji wanaongea kwa nguvu kuhusu ufisadi lakini leo wamekuwa madalali wa mafisadi na hawa wako kote CCM na huku kwetu wapinzani,” alisema.

Selasini alizungumza baada ya kutanguliwa na wabunge wenzake, Anne Killango Malecela wa Same Mashariki na Christopher Ole Sendeka wa Simanjiro (CCM), ambao walionekana kupishana katika kuwaunga mkono waziri na watendaji wake. soma zaidi http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=38649

Kuunganishiwa Umeme Sasa Kuanzia Sh180,000

SERIKALI imetangaza kushusha gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo kwa viwango ambavyo ni kati ya asilimia 60 na 77 kwa wakazi wa vijijini na kati ya asilimia 29 na 65 kwa wananchi waishio sehemu za mijini.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliambia Bunge jana kuwa gharama za kuunganishiwa umeme kwa wateja walioko kwenye umbali usiozidi meta 30 (single phase) ambao hawahitaji nguzo sasa zitakuwa Sh177,000 kwa wateja wa vijijini na mijini itakuwa Sh320,960 badala ya Sh455,108 ambazo zilikuwa zikilipwa awali bila kujali mteja aliko.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake ya 2012/2013 bungeni Dodoma jana, waziri huyo alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja waishio mijini.

Profesa Muhongo alisema pia Serikali imeshusha gharama za uunganishaji wa umeme kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja katika maeneo ya vijijini ambao sasa watalipa Sh337,740 na mijini Sh515,618 badala ya Sh1,351,884 zilizokuwa zikilipwa awali.
“Punguzo hilo la pili ni sawa na asilimia 75.02 kwa wateja wa vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa Sh454,654 na mijini watalipa Sh696,670 badala ya Sh2.001 milioni zilizokuwa zikilipwa awali.

“Punguzo hili ni sawa na asilimia 77.28 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza. “Viwango hivyo vya gharama vitaanza kutumika Januari mwakani bila kisingizio.”

Chimbuko la Punguzo
Hatua ya kushushwa kwa gharama za kuunganishiwa umeme zimekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete alipolilekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupunguza gharama hizo ili kupata wateja wengi zaidi.

Machi 18 mwaka jana, Rais Kikwete aliitaka Tanesco, kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi ili wengi wapate huduma hiyo sambamba na kuongeza wateja wanaotumia umeme kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.

Akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, Rais Kikwete alisema gharama hiyo ikipunguza, itaiwezesha Tanesco kupata wateja wengi ikilinganishwa na sasa.
Kauli ya Rais ilitokana na maelezo ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, William Mhando (ambaye sasa amesimamishwa kazi) kuwa Tanesco ilikuwa ikifanya mazungumzo na Benki za Akiba na Azania ili zitoe mikopo kwa wateja kwa ajili ya kuunganishiwa umeme.

Chanzo. http://www.mwananchi.co.tz

Magazeti ya Leo Jmamosi 28th July 2012

Michuano ya Olympics Yafunguliwa London 2012.



        Tuwaombee Matanzania Wenzetu wanaowakilisha Nchi Yetu waweze kufanya vizuri.

Hakika Arusha Leo Imebarikiwa

                                                             Watu  Wakiendelea Kuingia uwanjani



     Maombi haya yamefanywa na Safina redio hakika mungu ametenda maajabu watu ni wengi sana wakiwa  wamevalia magunua wakifanya toba kwa tanzania na familia zetu, MUNGU IBARIKI TANZANIA.