Tuesday, July 3, 2012

Wenyeji 12 Wa Euro 2020

Platini anasema huenda ikawa bora michuano ya Euro 2020 kufanyika katika miji mbalimbali ya Ulaya

Michel Platini, rais wa shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA, amesema michuano ya Euro 2020 huenda ikafanyika katika miji mbalimbali mwaka 2020, badala ya kuwa na mji mmoja ambao utakuwa ni mwenyeji.

Utamaduni wa mashindano hayo huwa ni nchi moja, au mbili, kushirikiana katika kuwa mwenyeji, kama ilivyo wakati huu michuano hiyo kufanyika Poland na Ukraine.
Mashindano yajayo yatafanyika nchini Ufaransa, mwaka 2016.

"Euro 2020 inaweza kufanyika popote barani Ulaya," alielezea Platini. "Yanaweza kufanyika katika nchi moja yenye viwanja 12, au kufanyika katika uwanja mmoja katika miji 12 au 13 ya Ulaya."

Platini ameelezea kwamba wazo hilo pia linaweza kuokoa senti katika kuepuka gharama kubwa za ukarabati, na juhudi za kujenga viwanja vipya na kuimarisha viwanja vya ndege.

Uturuki ilitazamiwa na wengi kupata nafasi ya kuandaa mashindano ya mwaka 2020, lakini ombi la nchi hiyo limekumbwa na tatizo, kwa kuwa nchi hiyo pia ina nia ya kuandaa michezo ya Olimpiki mjini Istanbul, mwaka huohuo wa 2020.

Mataifa ya Uskochi, Wales na Jamhuri ya Ireland, rasmi pia yameelezea nia yao ya kuandaa michuano ya 2020.

Platini ametangaza kwamba uamuzi kamili utatangazwa kati ya mwezi Januari hadi Februari mwaka ujao.

Chanzo:BBC

Afisa Mkuu Mtendaji Wa Barclays Ajiuzulu

Afisa mkuu mtendaji wa benki ya Barclays Bob Diamond hatimaye amejiuzulu.Mwenyekiti anayeondoka Marcus Agius, ambaye alitangaza kujiuzulu kwake hiyo jana, sasa atakuwa mwenyekiti wa kudumu wa benki hiyo na ataongoza mikakati ya kumtafuta afisa mkuu mtendaji mpya.Benki ya Barclays, imekumbwa na kashfa ya kuongeza viwango vya riba kinyume cha sheria.
Chanzo:BBC

Mgomo Wa Madaktari: JK Akoleza Moto

Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara wa Sh3.5 milioni aache kazi, viongozi wa dini, wanasiasa, wabunge na wasomi wamemtaka apunguze jazba.Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema mgogoro wa madaktari na Serikali bado unajadilika huku Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika akienda mbali zaidi na kusema Serikali iache kisingizio cha Mahakama kulizuia Bunge kujadili mgogoro baina yake na madaktari, wakati yenyewe inajadili na kutoa maelezo.

Juzi, katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema Serikali haiwezi kuahidi kuwa inao uwezo wa kuwalipa madaktari mshahara huo na posho zote kwani ikifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa Sh7.7 milioni kwa mwezi kitu ambacho hakiwezekani.

Jana, wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema mgogoro huo kati ya Serikali na madaktari bado unajadilika na kusisitiza kuwa hotuba ya Rais Kikwete haijajibu madai ya madaktari.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema ingekuwa jambo jema kama kungekuwa na uwezekano wa mazungumzo kuendelea.

Alisema kauli ya Rais ni upande wa Serikali hivyo, ingekuwa vyema kama madaktari nao wangepata nafasi ya kujieleza.

Wanasiasa
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alimtaka Rais apunguze hasira na kuitaka Serikali ikubali kurudi katika meza ya mazungumzo hata kama ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuwapeleka mahakamani madaktari waliogoma.

Alisema kama Serikali haiwezi kulipa kiwango cha mshahara kilichopendekezwa na madaktari, irudi katika meza ya mazungumzo ili kutafuta suluhu ya mgomo huo unaowaumiza zaidi wananchi.

“Warudi kwenye meza ya majadiliano siyo kila mmoja kusema la kwake na kuacha mgomo kuendelea huku, watu wakiteseka hospitalini bila msaada wowote,’’ alisema Machali.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema Serikali haipaswi kuwafukuza madaktari kwa kuwa imetumia gharama kubwa kuwasomesha.

“Ikiwafukuza madaktari italazimika kuwaleta walio nje ya nchi ambao ni gharama kubwa… Serikali itatue mgogoro huu,” alisema.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema Serikali iache kutumia kisingizio cha Mahakama kulizuia Bunge kujadili mgogoro wa madaktari wakati yenyewe ikitoa ufafanuzi.

“Uamuzi wa Serikali kutoa kauli kupitia hotuba ya Rais una mwelekeo wa kukwepa wabunge kujadili hotuba husika ambayo awali, ilielezwa kuwa ingetolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni. Inawanyima haki wabunge wasitimize wajibu wa kikatiba wa Ibara 63 (2) wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema, kwa kuwa Bunge litajadili mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuanzia leo, ni muhimu wabunge wakajadili pia masuala ambayo Rais ameyaeleza kwa taifa na kutimiza wajibu wa kikatiba.

“Hotuba ya Rais imeendeleza kauli za upande mmoja ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali kuhusu mgogoro huo bila taifa kupewa fursa ya kupata maelezo na vielelezo vya upande wa pili, hivyo Serikali imetoa kauli yake hadharani badala ya bungeni au mahakamani.

Viongozi wa dini

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo alisema madaktari hao wanatakiwa kurudi kazini kwa kuwa tayari Serikali imeshasema kuwa haina fedha za kuwalipa na kuongeza kuwa hata kama wana madai yao, wadai wakiwa kazini.

“Asilimia kubwa ya madaktari wamesomeshwa na Serikali… Serikali hiyohiyo inawaeleza kuwa haina fedha za kuwalipa kama wanavyotaka, binafsi nawaomba tu warudi kazini kwa kuwa mgomo wao unawaathiri zaidi wananchi kuliko hata hao viongozi wa Serikali.

“Tunajua tulikotoka ila hatujui tunakokwenda, kama ni kuboreshwa kwa sekta nzima ya afya, Serikali imesema itatekeleza hilo, haiwezi kuyatekeleza kwa siku moja, haya mambo yanajadilika.

Alisema kama Serikali itakuwa na makosa yake, itayajibu mbele za Mungu... “Madaktari watekeleze wajibu wa kazi yao kwa uwezo wa Serikali iliyopo madarakani.”

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Kagera, Dk Methodius Kilaini alisema kanisa hilo haliwezi kuunga mkono mgomo huo.

Alisema pamoja na kuwa madaktari wana madai yao, jukumu lao kubwa ni kufuata maadili ya kazi yao ambayo hayawaruhusu kugoma.

Katibu Mkuu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Askofu David Mwasota alisema madaktari wanatakiwa kutenganisha siasa na maadili ya kazi yao.

“Hata kama Serikali ina makosa yake lakini, wao kuendelea kugoma si jambo zuri kwa jamii na hata mbele za Mungu, watumie njia nyingine kudai madai yao, lakini waendelee kutoa huduma. Madaktari ni watu muhimu, kurudisha viungo vya binadamu katika hali ya kawaida si kazi ndogo, warudi kazini kuokoa mamia ya Watanzania maskini.”

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Arusha Abdulkarim Jonjo alisema ipo haja kwa Serikali kukaa meza moja na madaktari hao.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mjini Kati, Thomas Laizer alisema mgogoro wa madaktari umalizwe kwa mazungumzo.

Alisema Serikali inapaswa kuwa wazi inapozungumza na madaktari kwa kueleza ni mambo gani yanawezekana na kwa muda gani ili, kuondoa migogoro.

Akizungumza juzi katika ibada maalumu katika kanisa la KKKT Kimandolu, alisema ili kuondoa hisia kuwa Serikali inahusika na tukio la kutekwa Dk Ulimboka ni lazima iundwe tume huru.

“Nadhani ili kuondoa haya maneno ambayo si jambo dogo, Serikali inapaswa kuunda tume huru kuchunguza tukio hili, kwani inawezekana waliohusika ni watu wengine tu wenye nia mbaya na Serikali lakini ili ukweli ujulikane ni muhimu kuwepo tume huru,” alisema Askofu Laizer.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum aliwataka madaktari kutii agizo lililotolewa na Mahakama kwa kurudi kazini.

“Rais ameshaeleza wazi kwamba Serikali haina fedha za kuwalipa kama wanavyotaka, warudi tu kazini na kuweka masilahi ya Watanzania mbele na kuacha kutanguliza masilahi binafsi,” alisema Sheikh Salum.

Wanaharakati

Mkurungezi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hotuba hiyo ya Rais haina jipya zaidi ya kurudia maelezo yake ya awali alipokutana na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Nilitarajia kuwa hotuba itakuwa tofauti lakini sivyo. Amerudia maelezo yaleyale aliyoyasema Machi 12 (mwaka huu) alipokutana na wazee katika Ukumbi wa Diamond Jubilee,” alisema Bisimba.

Wakili Peter Jonathan alisema kama kweli Serikali inataka kurudisha imani kwa Watanzania kuhusu tukio la Dk Ulimboka ni lazima ijisafishe kwa kuunda tume huru nje ya Serikali.

“Watafute hata Jaji mstaafu, si lazima atoke Tanzania kuongoza tume huru ikibidi tuchukue hata nje ya nchi ili wakitoa taarifa iweze kuaminiwa na jamii na hiyo ndiyo dhana sahihi ya utawala bora,” alisema.

Mjumbe wa Chama cha Watabibu wa Tiba Asili (ATME), Boniventure Mwalongo ameitaka Serikali kuacha kutumia nguvu kushughulikia madai ya madaktari badala yake ipanue wigo wa majadiliano ili kutatua tatizo hilo.

“Nimesikiliza hotuba ya Rais lakini, haijaonyesha kama kuna jawabu la mgomo hivyo wapanue wigo wa majadiliano ili kumaliza mgogoro huu,” alisema Mwalongo.

Habari hii imeandikwa na Fidelis Butahe,
Nora Damian, Bakari Kiango, Freddy Azzah, Daniel Mwingira, Dar; Daniel Mjema, Moshi; Mussa Juma, Arusha na Frederick Katulanda, Mwanza.
Chanzo:  http://www.mwananchi.co.tz


Dk. Mtaki: Usagaji Ni Starehe Kama Zingine ; Asema Ikizidishwa Inaharibu Saikolojia Ya Mchezaji

Dk. Magreth Mtaki.
GUMZO juu ya wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars kufanya vitendo vya kustareheshana, limetetewa na baadhi ya wataalam kuwa ni tendo linaloweza kufanyika kama lilivyo tendo lingine.

Mjadala ulizuka wiki mbili zilizopita juu ya kufanya vibaya kwa Twiga Stars kwa kufungwa jumla ya mabao 3-1 na Ethiopia katika mechi za kuwania kucheza Fainali za Afrika zitakazofanyika Equatorial Guinea baadaye Novemba.


Mkwasa alisema kuwa kufanya vibaya kwa timu hiyo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kuendekeza vitendo vya kusagana, lakini akasema kuwa waliokuwa wakifanya 'hayo mambo' (bila kuwataja) walitimuliwa.

Lakini vitendo hivyo vimetajwa kushamiri hasa katika timu zinazojumuisha wanawake ama wasichana wengi kwani kila mmoja anakuwa na tabia na mihemko yake kiasi cha kuwaathiri wengine.

Spoti Mikiki ilifanya mahojiano na Dk. Magreth Mtaki, daktari wa michezo wa siku nyingi kutoka Kurugenzi ya Michezo ambaye anasema kuwa kusagana (lesbianism) ni kama starehe nyingine ambayo watu wa jinsi mbalimbali wanafanya.

Anasema kuwa tatizo linakuja kuwa ni suala linalohusisha wasichana ama kinamama ndiyo maana linaleta mshangao, lakini hakuna tofauti na matendo mengine ama kustareheshana kwa watu wawili.

Dk. Mtaki ambaye pia ni Makamu wa Chama cha Soka ya wanawake Tanzania, TWFA, anasema kuwa kitendo cha kusagana, kwa upande mwingine kina athari kubwa kwenye timu kwani endapo kitafanywa kwa kuzidisha, inamaliza nguvu mchezaji.

"Hata ingekuwa wewe na mke wako, una mechi ya kimataifa ama ligi, halafu ukafanya tendo la ndoa kupitiliza, ni wazi itapunguza uwezo wako uwanjani, basi hata hawa wanaosagana, wakizidisha, lazima uwezo utapungua.

"Kingine ambacho naweza kusema, lakini sasa hii ni kwa mchezaji mwenyewe...hali hii itamfanya hatokuwa na hamu ya mwanaume akiamini kuwa mwanamke mwenzake anakata kiu.
Chanzo:  http://www.mwananchi.co.tz

Nimeipenda Hii


Magazeti ya leo Jumanne


Diwani wa Kata ya Makongo (Chadema), Deusdedit Jacob Mtiro.

                                Diwani wa Kata ya Makongo (Chadema), Deusdedit Jacob Mtiro.

ILIKUWA kama sinema pale Diwani wa Kata ya Makongo (Chadema), Deusdedit Jacob Mtiro alipoongoza kundi la vijana waponda kokoto kubomoa sehemu ya nyumba ya Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Kata ya Makongo, Judith Lungato Stambuli Ijumaa iliyopita nyumbani kwake Mlalakua, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Katika tafrani hiyo kiongozi huyo licha ya kuvunjiwa sehemu ya nyumba yake na kuchaniwa gauni na mtandio, habari za kipolisi zinasema Diwani Mtiro anatuhumiwa kwenda na wahuni kwa kiongozi huyo ambapo alipigwa na kusababisha mali zake kadhaa kuibiwa kutokana na vurugu kubwa iliyozuka.

Habari ambazo polisi wanazo ni kwamba mali alizoibiwa kiongozi huyo ni simu aina ya Blackberry yenye thamani ya shilingi 350,000, nguo aina ya dera na vitenge vyenye thamani kubwa, saa ya mkononi na nondo kadhaa zilizokuwa kwenye nyumba ya mama huyo.

Mwandishi wetu aliambiwa na kiongozi mmoja wa polisi kuwa tayari Diwani Mtiro amefunguliwa jalada Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Mlimani lenye namba UD/RB/4045/2012 (Shambulio la mwili).

Akizungumza na mwandishi wetu, Bi Stambuli alisema sehemu iliyosababisha ashambuliwe hakujenga hivi karibuni bali imejengwa miaka zaidi ya miwili iliyopita na wala haikuwa na usumbufu wowote kwa raia.

“Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wangu aliwahi kusuluhisha suala hili baada ya watu wenye roho mbaya kuvunja, wakaamriwa wajenge, tukiwa polisi alikiri kufanya kosa na wakaamua kunijengea kwa gharama zao, nilishangaa kuona Diwani Mtiro anakuja na kunibomolea tena bila hata notisi, ” alisema katibu huyo.

Baadhi ya wananchi wa Mlalakua akiwemo mzee Kariakoo, walisema kitendo alichofanyiwa mwanamke huyo ni cha kinyama na siasa imeingizwa, “Hakuna sehemu ilikuwa nadhifu kama hii kwani mvua ikinyesha watu walikuwa hawakanyagi tope.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alipopigiwa simu alisema hajapata taarifa ya tukio hilo na akaahidi kufuatilia.

Imeandaliwa Na Haruni Sanchawa.

Mwanamke azikwa akiwa hai Mbeya


                   Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Malamba, Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

KUMEZUKA vitendo vya unyama mkoani Mbeya vya kuzika watu wanaotuhumiwa kuwa ni washirikina wakiwa hai ambapo hivi karibuni watu wawili akiwemo mwanamke mmoja wamefanyiwa unyama huo.
Mwanamke aliyezikwa akiwa hai kwa tuhuma za kujihusisha na ushirikina ni Rozina Mwadala (60) ambapo tukio hilo lilitokea Juni 2, mwaka huu.

Mwanamke huyo alichukuliwa hatua hiyo baada ya kifo cha mmoja wa ndugu yake ambaye alifariki muda mchache baada ya kulalamika kuwa alikuwa akiumwa sikio na kichwa. Hata hivyo, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa tayari kuhojiwa na mwandishi wetu kwa hofu ya kukamatwa na polisi.

Kufuatia vitendo hivyo kushika kasi mkoani Mbeya, Mwenyekiti wa Muungano wa Jamii Tanzania (Mujata), Chifu Soja Masoko, amewaonya wananchi wa Kijiji cha Malamba, Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kuacha mara moja tabia za kujichukulia sheria mikononi alipokuwa akiwahutubia katika mkutano wa hadhara Juni 15, mwaka huu.

“Hasara yake mnaona. Sasa kufuatia kitendo hicho cha kikatili baadhi ya wananchi wamehama kijijini hapa kukwepa mkono wa sheria na shughuli za kiuchumi zimezorota,” alisema.

Mbali na mwanamke huyo kuzikwa hai, hivi karibuni mwanaume mmoja, Nyerere Kombwee naye alizikwa hai baada ya kutokea kifo cha mdogo wake kisha yeye kutohudhuria msibani ndipo wananchi wakamsaka na walipompata wakampiga na yeye akatoa vitisho kuwa damu yake isingeweza kwenda bure ndipo wakaamua kumzika akiwa hai.

DAKTARI MWINGINE ATEKWA

WAKATI Kiongozi wa Chama Cha Madaktari nchini Dk. Steven Ulimboka akiwa amesafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu, Daktari mwingine, John Chilinde ametekwa na kupigwa ambapo amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

Daktari huyo ambaye ni mkazi wa Tabata Kimanga , wilayani Ilala anayetibu katika Hopitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam alitekwa Ijumaa saa tano usiku akiwa anatoka baa iitwayo Flora Pub iliyopi Tabata jijini.

Habari zinasema akiwa anatoka katika baa hiyo, Dk Chilende alitekwa na vijana watatu ambao walimshambulia huku wakimuuliza kwa nini wamegoma kutibu watu katika hospitali za serikali.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Dk. Chilende alishambuliwa kwa dakika kumi na baadaye kutekwa kisha akaenda kutelekezwa akiwa hoi hajitambui hatua chache kutoka sehemu aliyokuwa anapigiwa .

Chanzo kimesema daktari huyo aliokolewa na dereva wa kibajaji ambaye alimkuta akigagaa chini huku akivuja damu mdomoni, alimpakia na kumpeleka Kituo cha Polisi Buguruni ambako alifunguliwa jalada namba BUG/RB/7974/ 2012 (Shambulio la kudhuru mwili), baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Amana kwa matibabu zaidi.

Afisa mmoja wa polisi wa Kituo cha Buguruni ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na akaongeza kuwa wahusika wa unyama huo wanasakwa kwani daktari huyo anamfahamu mmoja wa waliyemshambulia. Kamanda wa Kanda Maalum, Suleiman Kova hakupatikana kuzungumzia tukio hilo. Chanzo: Globalbuplisher

CHADEMA:TAARIFA KWA UMMA JUU YA MELI ZA IRAN NA BENDERA YA TANZANIA

KWA takribani muda wa juma moja sasa kumekuwepo na taarifa katika vyombo vya habari na njia mbalimbali za upashanaji habari, kuwa kampuni moja ya meli inayodaiwa kutoka Iran, inayojulikana kwa jina la NITC (National Iranian Tanker Company), inatumia bendera ya Tanzania, isivyo kihalali na kinyume kabisa na sheria za nchi na zile za kimataifa, kwa malengo ambayo hayajulikani.

Pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa taarifa kwenye Baraza la Wawakilishi tarehe 2 Julai 2012 kukanusha taarifa hizo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania   kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Uchukuzi kutoa taarifa kwa umma juu ya hatua ilizochukua kuchunguza madai hayo.

Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ieleze iwapo utaratibu huo umezingatia kwa ukamilifu United Nations Convention law of the Sea, kifungu cha 91,  Geneva Convention of Registration kifungu cha 6 na maazimio mengine ya kimataifa kuhusu usajili wa meli kubwa pamoja na usafirishaji wa mafuta.

Maelezo yaliyotolewa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayoongozwa na CCM na CUF yanaibua maswali kutokana  na kampuni ya Philtex ya Dubai inayoelezwa kupewa uwakala na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini- Zanzibar Maritime Authority (ZMA) kufanya kazi na makampuni mengine hivyo taarifa hizo hazijitoshelezi katika kuondoa uwezekano kwamba meli za NITC zilipeperusha bendera ya Tanzania.

Ili kujisafisha juu ya tuhuma hizo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipaswa kushirikiana na Serikali ya Muungano kufanya uchunguzi wa kubaini msingi wa tuhuma hizo na kuchukua hatua iwapo meli za NITC zilipeperusha bendera ya Tanzania bila ridhaa  ya serikali zote mbili.

Ikumbukwe kwamba hii si mara ya kwanza kwa baadhi ya maofisa wa ZMA kutuhumiwa kuruhusu vitendo vilivyo kinyume na sheria kama ilivyojitokeza wakati wa kashfa ya kuzama kwa meli ya Spice Islender.

Kwa upande mwingine, Serikali ya Muungano nayo haiwezi kukwepa kuwajibika kwa kuzingatia kuwa kuwa baadhi ya taarifa hizo katika vyombo vya habari vimewanukuu mawaziri wa serikali wakionekana kujikanyanga na kujikanganya juu ya suala hili nyeti la bendera ya taifa, ambayo ni moja ya utambulisho wetu rasmi kama Watanzania, kutumika kwa malengo yasiyojulikana na kampuni ya nje.

Moja ya vyombo vya habari hapa nchini, vimewanukuu mawaziri husika, Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, juu ya suala hilo.

Wakati Waziri Mwakyembe amenukuliwa akisema kuwa anazo taarifa za suala hilo, lakini asingeweza kulitolea kauli mpaka Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Tanzania Zanzibar azungumze, Waziri Membe yeye mbali ya kukiri kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria, anasema habari hizo zilikuwa za kushtushwa na ngeni kabisa, huku akisema kuwa vyombo husika vitalichunguza kwa makini.

Ukimya wa serikali yetu ambayo kwa hakika unatokana na udhaifu wake katika kuchukua maamuzi, sasa umesababisha kitendo hicho kutafsiriwa kuwa Tanzania inaibeba na kuisaidia Iran kukwepa vikwazo ambavyo nchi hiyo inatishiwa na mataifa ya Magharibi, hasa Marekani na Umoja wa Ulaya, kutokana na malumbano ya muda mrefu ambayo yanatokana na mataifa hayo kutumia mabavu na vitisho kuzichagulia baadhi ya nchi nyingine duniani, nini cha kufanya na rasilimali zake mathalani mzozo unaoendelea na Iran kuhusu urutubishaji wa madini ya urani.

Si nia ya CHADEMA kuingia katika mgogoro wa Iran na Mataifa ya Magharibi hapa kupitia mjadala wa madai hayo yaliyoandikwa kwenye vyombo vya habari; lakini CHADEMA kinatoa tamko kufuatia ukimya na kigugumizi kinachoikumba Serikali ya CCM, kila inapohitajika kufanya maamuzi ya haraka, hasa kuwalinda watu wake na hadhi ya utaifa wao na nchi yao ndani na nje ya nchi.

Ni kutokana na udhaifu wa serikali hii, ambayo umekuwa ukijidhihirisha pia kwa kushindwa kupanga bajeti inayojitegemea hasa kwa kutumia utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo nchi hii imebarikiwa, hali inayotufanya tuonekane taifa ombaomba na kupoteza heshima mbele ya mataifa makubwa na madogo, kuwa hatuna uwezo wa akili kuweza kujitegemea.

Utegemezi huu umefanya baadhi ya raia wa Nchi nyingine mathalani Mbunge aitwaye Howard Berman wa Bunge la Marekani, akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Nje, kupata uwezo wa kuandika barua ya dharau na kejeli kwa Rais Jakaya Kikwete, juu ya suala hilo la Meli za NIT kutuhumiwa kupeperusha bendera za Tanzania.

Kupitia tamko hili, CHADEMA tunaitaka serikali kutoa kauli madhubuti juu ya suala hilo ambalo tayari limechukua sura ya mjadala wa kimataifa usiokuwa na tija yoyote kwa mustakabali wa Watanzania. Suala la bendera ambayo ni utambulisho wa taifa letu, haliwezi kuwa suala la mchezo tu, ambapo mawaziri wazima hawawezi kutoa kauli za kina na kuchukua hatua zinazostahili.

Imetolewa tarehe 2 Julai 2012 na:
Hamad Mussa Yussuf
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar