Thursday, August 23, 2012

Magazeti Ya leo Alhamisi 23rd August 2012

Taasisi Za Kidini Zakanusha Uamsho



Taasisi mbalimbali za kidini hapa nchini zilizopata usajili rasmi kwa Mrajis Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimekanusha kuhusika na tamko lililotolewa na Amiri Mkuu wa Jumuiya ya Uamsho, Sheikh Mselem Ali la Waislamu wa Zanzibar wagomee kushiriki katika Sensa ya Watu na Makaazi Kitaifa inayotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.

Wakizungumza na Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga Wawakilishi wa Taasisi hizo wamelaani tabia ya Uamsho ya kujipa Mamlaka ya kuzisemea Taasisi hizo.

Aidha,wameitaka Jumuiya ya Uamsho kuthibitisha ni kikao gani kilichokaa na kuzungumza na Taasisi za Kidini na kuamua kwa pamoja kutowa tamko hilo la kupinga kushiriki kwa Waislamu katika Sensa.

Aidha, wameihakikishia Afisi ya Mufti na Serikali kuwa watashiriki katika Sensa ili kusaidia maendeleo ya Zanzibar na kutatua baadhi ya migogoro ya kijamii na sio kujiingiza katika siasa na kupingana na Serikali kama ambavyo imekuwa ikifanya Jumuiya ya Uamsho.

Taasisi zimewataka Waislamu kushirikiana na Serikali na kuachana upotoshaji unaofanywa na Uamsho.

Aidha, wameitaka Jumuiya ya Uamsho kuachana mara moja kutumia kivuli cha umoja wa Taasisi za kidini Zanzibar wanapoamua mambo yao kwani Jumuiya hizo nyingi hazikubaliani na Sera yao ya fujo na vurugu.

Mwisho.
Imetolewa na:
Idara ya Habari(MAELEZO) Zanzibar
23/08/2012

Je Umewahi kutumia Maziwa ya Soya.Hakika ukijaribu hutaacha yana ladha zuri na bora kwa afya ya watoto wako na familia yako ni halisi hayana chemical yoyote. tumia bidhaa za kitanzania.

            Yanapatikana Supermarket karibu zote mjini Arusha.Pia ukihitaji unaletewa popote ulipo.

Chenge Kumtetea Mramba Kesi Ya Ufisadi

WAZIRI wa zamani wa Fedha, Basil Mramba ameanza kujitetea katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni huku akiwataja mashahidi sita akiwamo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge kuwa mashahidi wake.

Mashahidi wengine watakaomtetea Mramba katika kesi hiyo, ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mwakilishi wa Kampuni ya M/S Alex Stewart Government Business Assayers, Erwine Florence, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, John Cheyo na Mtaalamu wa Ushauri wa Masuala ya Kodi, Florian Msigala.

Baada ya kutaja idadi hiyo ya mashahidi, Mramba aliliambia jopo linaloongozwa na Jaji John Utamwa akisaidiwa na Jaji Sam Rumanyika, Msajili Sauli Kinemela kuwa shahidi wa sita ambaye wanatarajia kumwita, bado hajathibitisha kama atakwenda kutoa ushahidi au la.

Mramba alieleza kuwa kati ya mashahidi hao anaotarajia kuwaita kumtetea, watatu watawasilisha nyaraka na wengine watafika mahakamani.

Licha ya kuwataja mashahidi hao, Mramba aliiambia Mahakama kuwa atatoa utetezi wake kwa njia ya kiapo.

Mbali na Mramba, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja nao wameiambia Mahakama kuwa na wenyewe watajitetea kwa njia ya kiapo na pia watatetewa na mashahidi hao.

Lakini Mgonja aliongeza shahidi mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Karisti.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, Mramba alianza kujitetea na Wakili wake Hurbert Nyange alimtaka aieleze Mahakama chimbuko la kesi inayomkabili.

Mramba alisema ana umri wa miaka 71. Alidai kuwa chimbuko la kesi hiyo ni malalamiko yaliyokuwapo bungeni kwa wananchi na kwenye vyombo vya habari kuwa ingawa Tanzania ina migodi kadhaa ya dhahabu, haijafaidika kwa sababu migodi hiyo ilikuwa inaiibia Serikali na kuidanganya juu ya uzalishaji na uuzaji wa madini hayo nje ya nchi.

Jeshi La Polisi Lataja Orodha Ya Vijana 1,446 Walioteuliwa Kujiunga Na Jeshi Hilo

JESHI la polisi Tanzania limetoa ajira 1,446 kwa Vijana wa kidato cha nne wa mwaka 2011,kidato cha sita mwaka 2012 na vijana walioko kambi za JKT Mafinga, Mlale, Ruvu, Mgambo Oljoro , Bulombola, Kanembwa, Itende, Nachingwea na Mgulani.

Kati ya hao 951 ni walio hitimu kidato cha nne na sita mwaka 2011/2012 na 495 kwa Vijana waliokuwa katika Kambi za JKT za JKT Mafinga, Mlale, Ruvu, Mgambo Oljoro , Bulombola, Kanembwa, Itende, Nachingwea na Mgulani.

Maelekezo Muhimu:-1. Vijana wa kidato cha nne wa mwaka 2011,kidato cha sita mwaka 2012 na vijana walioko JKT Mafinga, Mlale, Ruvu, Mgambo Oljoro , Bulombola, Kanembwa, Itende, Nachingwea na Mgulani waliochaguliwa kujiunga na Jeshi la Polisi baada ya mchakato wa usaili uliokamilika hivi karibuni wanatakiwa kuripoti Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi kati ya tarehe 06/10/2011 na 07/10/2012 kwa ajili ya zoezi la usajili litakaloanza chuoni hapo tarehe 8.10.2012.

2. Vijana hao wanatakiwa kuripoti tarehe 05/10/2012 kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa kwa ajili ya kuwaandalia usafiri wa kuwapeleka Chuoni.

3. Vijana wanaotoka katika makambi ya JKT yaliyotajwa hapo juu wataripoti kwa makamanda wa Polisi wa mikoa iliyo karibu nao.

Vijana wa kidato cha nne na sita wataripoti kwa makamanda wa Polisi wa Mikoa waliojiandikisha wakati wa zoezi la usaili lililoendeshwa mwezi Julai, 2012.

4. Atakaeamua kuripoti kwa Kamanda wa Polisi ambako hakupangiwa atalazimika kujigharimia usafiri hadi Chuo cha Polisi Moshi

5. Vijana hawa wanatakiwa kufika chuoni wakiwa na mahitaji yafuatayo:

a) Vyeti vyao vyote vya masomo(Academic Certificates/Result slip pamoja na Leaving certificates) kidato cha Nne/Sita, Vyeti vya kuzaliwa (Original Birth certificates). Hati ya kiapo cha kuzaliwa haitakubalika.

b) Mashuka mawili rangi ya Bluu Bahari (light blue)c) Chandaruad) Nguo za michezo(Track suit nyeusi,Tshirt blue na Raba)e) Pasi ya Mkaaf) Ndoo moja.1g) Pesa kidogo ya kujikimu.

6. Kwa mujibu wa kanuni za chuo ni marufuku kufika chuoni na simu ya mkononi, atakayepatikana na simu atafukuzwa chuoni hapo. Chuo kitaelekeza na kusaidia kufanya mawasiliano.

7. Hakikisha jina lako liko kwenye orodha hii. Jeshi la Polisi halitahusika na gharama zozote kwa atakaye kiuka maagizo haya.

CHADEMA Watuhumiwa Kutoa Rushwa Kwa Watanzania Waishio Marekani

UONGOZI DMV
WASHINGTON DC
MWENYEKITI, Katibu na Mweka hazina, wa Jumuia ya Watanzania waishio Marekani, wanashutumiwa na wanajumuia wa Washignton kuwa wamepokea rushwa kutoka kwa Chadema kwa ajili ya kufanyia pickic na party ya usiku, vitakavyofanyika Jumamosi hii, Agosti 25, 2012.

Habari za madai za shutuma hizo zinasema kuwa Jumuia ilikuwa na fedha taslim zisizozidi Dola 2000 za Marekani zinazotosha kufanya party ya mchana ya picnic peke yake, lakini kwa cha kushangaza wakati wanajumuia wakiwa wanahoji kwa nini party ya usiku ifanyike wakati Jumuia haina fedha za kutosha, Viongozi hao wameweza kuja na fungu kubwa la fedha ambazo watazitumia kufanya party zote mbili kubwa na za kifahari zitakazoambatana na chakula na vinywaji mchana na usiku bure.

Kama haitoshi kutokana na fungu hilo, pombe zitakuwa za bure hadi saa nane usiku, wakati ukumbi na muziki vikiwa vimelipiwa kwa Cash siyo mkopo.

"Habari za kuaminika na ushahidi upo zinasema kuwa Katibu wa Jumuia Bwana Amosi Cherehani ni Mweka hazina wa Chadema Washigton na ndiye ambaye ameweza kuhamasisha fedha hizo kutoka Chadema iliziweze kufanya hafla hiyo", Imsema taarifa iliyotumwa kwa mtandao kutoka Marekani.

"Wananchi wanahoji kwa nini Mwenyekiti ambaye alichaguliwa kwa kishindo ameweza kukubali kadia hii wkati Jumuia haifungamani na chama chochote cha siasa?" Imehojiwa katika taarifa hiyo.

"Kutokana na kadhia hiyo, wakereketwa wa Jumuia wameipa Mamlaka Kampuni ya ERNEST & YOUNG kufanya "INDEPENDENCE AUDITING" ya Jumuia ili kujua "INCOME AND EXPENDITURE za Jumuia yao zometoka wapi na zimetumika vipi kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa", Taarifa imesema.

Tarrifa imesema wanajumuia wanaomba kuitisha mkutano ili kupiga kura a maoni ya kutokuwa na imani na uongozi kwakuwa bado mchanga. .."Na tuliuchagua kwa imani, hatutaki vyama vya siasa vituingile...Rushwa ni adui wa Haki"

Chanzo: Bashir Nkoromo.

Waziri Wa Maliasili Na Utalii Ahudhuria Mkutano Wa tisa Wa Sullivan Malabo, Equatorial Guinea

Waziri wa maliasili na utalii balozi Khamis Kagasheki (kushoto) akijadiliana jambo na rais mstaafu wa Nigeria jenerali Olusegun Obasanjo mjini Malabo, Equatorial Guinea ambapo wanahudhuria mkutano wa tisa wa sullivan unaojadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya bara la Afrika.

Picha na Pascal Shelutete.

CCM Kukata Rufani Dhidi Ya Hukumu Ya Kesi Uchaguzi Igunga

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakikuridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, dhidi ya Mbunge wa jimbo la Igunga, Peter Dalally Kafumu.

Taarifa iliyolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye mchana leo, imeseme kufuatia kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Mary Shangali, kitakata rufani.

"Chama Cha Mapinduzi kimetafakari hukumu ya kesi ya uchaguzi iliyotolewa jana Agosti 21, 2012 na Mahakama Kuu kanda ya Tabora. Kimejiridhisha na kufanya uamuzi wa kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kesi ya uchaguzi, dhidi ya Mbunge wa jimbo la Igunga mkoani Tabora Dokta Dalaly Peter Kafumu.Kusudio hilo linatokana na kutorishwa na hukumu hiyo". imesema taarifa hiyo.

Jana Jaji Mary Shangali katika hukumu yake, alisema ametengua ushindi wa Dk. Kafumu baada ya kurishishwa na madai saba kati ya 17 yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo na Mlalamilikaji, aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Chadema, Joseph Kashindye.

Dk. Kafumu wa CCM alitangazwa kushinda kiti na Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Igunga, katika uchaguzi mdogo uliofanyika, Septemba mwaka jana, baada ya kujiuzulu aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Rostam Aziz.

Mwanasheria Wa CCM Makao Makuu Achukua Fomu Ya Kugombea Ujumbe NEC

 Mwanasheria wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Grorious Luoga (kulia) akiwa na mama yake mzazi Antonia Mselewa kushoto baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuchaguliwa nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kupitia wilaya ya Songea vijijini,katikati katibu wa chama wilayani songea Bi Lidya Gunda.
Mwanasheria wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Makao Makuu,Grorious Luoga (kulia) akikabidhi mchango wa shilingi 100,000 kwa chama hicho Wilaya ya Songea vijijini ili ziweze kusaidia katika mchakato wa chaguzi mbalimbali ndani ya chama,kushoto katibu wa chama hicho songea vijijini,Lidya Gunda.