Wednesday, November 14, 2012

Wanafunzi Wa Kitanzania Nchini Urusi Wakosa Malazi Na Chakula...!

Sisi wanafunzi wa kitanzania nchini Urusi ,tunakosa huduma za msingi kama vile malazi , chakula na bima ya afya.

   Serikali kupitia bodi ya mikopo ya elimu ya juu na Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi ,kwania njema iliamua kusomesha wanafunzi wa kitanzania katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Urusi.
Lakini kutokana na utendaji mbovu na ubinafsi wa baadhi ya watendaji wa Bodi ya mikopo, kumekua na ucheleweshwaji wa ulipaji wa pesa za kujikimu , malazi na bima ya afya kwa zaidi ya miezi mitatu sasa bila sababu za msingi toka kuanza kwa mwaka wa masomo 2012/13.

Hali hii imetupelekea wanafunzi kuanza kufukuzwa katika hosteli tunazoishi pamoja na kutopatiwa huduma za afya pindi tunapo ugua.Ikumbukwe kuwa katika nchi za ulaya huwezi pata matibabu kama huna bima ya afya.

Shukrani zetu za dhati ziende kwa Ubalozi wa Tanzania nchi Urusi kwa kushirikiana bega kwa bega na Wanafunzi katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili linalotukabili katika kipindi hiki kigumu pamoja na majuku mengi waliyonayo, pamoja na jitihada hizo mpaka sasa hakuna ufumbuzi wowote uliopatikana.

Tunaandika waraka huu kwa huzuni na masikitiko makubwa sana kwa sababu kutopatiwa mikopo mpaka sasa sio tu kunafanya wanafunzi waishi maisha magumu na hatari, vilevile kunatia aibu Taifa kwa kutolipa ada kwa wakati.

Tunaamini kabisa Serikali kupitia bodi ya mikopo ,wizara ya elimu na mafunzo stadi na ufundi na ubalozi wa Tanzania Nchini Urusi una  nia njema kabisa kusomesha vijana wake nje ya nchi, ispokua tu kuna baadhi ya watendaji wa bodi ya mikopo wamekua wazembe na kutowajibika kwani wamekua wakitoa majibu ya uongo na jeuri kwa uongozi wa wanafunzi na maafisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Urusi.

Ombi letu kwenu ni kutufikishia ujumbe huu kwa wahusika na watendaji wa ngazi za juu za bodi ili waweze kutusaidia sisi wanafunzi wa Urusi ambao tupo hatarini huku ugenini.

Tunatumaini kutokana na Uzito wa tatizo letu wahusika watalishughurikia na kulitatua tatizo hili kwa haraka zaidi na kutupa ufafanuzi wa ucheleweshwaji wa mikopo ya wanafunzi kwa zaidi ya miezi mitatu(3)

WANAFUNZI NCHINI URUSI.

CCM Yachagua Wajumbe Wa Sekretarieti Ya Halmashauri Kuu Ya Taifa.

                                             Abdulrahman Kinana-Katibu Mkuu wa CCM, Taifa
                                              Mwigulu Nchemba-Naibu Katibu Mkuu (Bara)
                                             Vuai Ali Vuai-Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar)
                                               Nape Nnauye-Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi
                           Asha-Rose Migiro- Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa
                                                Meghji-Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha
                                        Muhamed Seif Khatib, Katibu wa NEC, Oganaizesheni

Kikao hicho kitajadili juu ya kuunda na kupitisha majina yaliyopendekezwa na Mwenyekiti wa Chama Mapinduzi Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama ya Taifa (CC) pamoja na uundaji wa sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Mwenyekiti wa Chama kwa mujibu wa Kanuni na Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, anayo fursa ya kuteua wajumbe kumi(10) wa Halmashauri kuu ya Taifa, ambapo Mwenyekiti aliwateua wajumbe wanne(4) na akabakiza nafasi nyingine sita (6) miongoni mwa wajumbe hao ni Mhe. Asha-rose Migiro, Mhe. Zakhia Meghji, Mhe. Nape nnauye na Mhe. Abdulrahaman Kinana .

Baada ya uteuzi huo Mwenyekiti pia alipendekeza majina ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ambapo alipendekeza majina yafuatayo;

    Nafasi ya Katibu Mkuu, alimpendekeza Mhe. Abdulrahaman kinana.
    Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mhe. Vuai Ali Vuai.
    Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, Mhe. Lameck Madelu Nchemba.
    Katibu wa Oganaizesheni ni Ndugu Mohamed Seif Khatibu.
    Katibu wa Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, Asha-rose Migiro.
    Katibu wa Uchumi na Fedha, Zakhia A. Meghji.

Baada ya mapendekezo hayo, Halmashauri Kuu ya Taifa ilipitisha majina hayo na kuyakubali kuwa hao waliopendekezwa ndio hasa wanaofaa kuwa wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Pia, Mwenyekiti akawashukuru wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa waliopita na pia kuwataka wajumbe wapya kuchapa kazi, na kuwataka kujenga mustakabali wa Chama, Uimara na Umadhubuti kwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kusaidiana.

Picha na habari  Issa Michuzi

Marekebisho Ya Viingilio Kati Ya Serengeti Boys Na Congo


                                         TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
                                                                Novemba 14, 2012

MAREKEBISHO VIINGILIO SERENGETI BOYS v CONGO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko kwa kiingilio cha juu cha mechi ya raundi ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Congo Brazzaville itakayochezwa Jumapili (Novemba 18 mwaka huu).

Awali kiingilio cha juu katika mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni kilikuwa sh. 5,000. Lakini kwa lengo la kuwafanya wadau wa kiingilio hicho kuchangia gharama za mechi hiyo sasa kutakuwa na viingilio vitatu tofauti katika viti vya VIP.

Kwa VIP A ambayo ina viti 748 kiingilio kitakuwa sh. 10,000, VIP B inayochukua watazamaji 4,160 kiingilio ni sh. 5,000 wakati VIP C yenye viti 4,060 kiingilio ni sh. 2,000. Kwa sehemu nyingine (viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu) ambavyo jumla yake ni 48,590 kiingilio kitabaki kuwa sh. 1,000.

Timu ya Congo Brazzaville kwa taarifa tulizopata awali kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la Congo (FCF) ilikuwa iwasili jana (Novemba 13 mwaka huu) usiku. Lakini timu hiyo haikutokea na sasa tunatarajia itawasili leo (Novemba 14 mwaka huu) saa 8 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines. Congo itafikia Sapphire Court Hotel.

Wakati huo huo, Kamati ya Serengeti Boys itakutana na waandishi wa habari kesho (Novemba 15 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika kuanzia saa 5 asubuhi hoteli ya JB Belmont, ukumbi wa Ngorongoro.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Dar Express yanusurika kuanguka..



Basi la Dar Express lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda mkoani Arusha lilinusurika kuanguka baada ya kuacha njia na kugonga ukingo wa barabara ya Chalinze, Segera kama linavyoonekana katika picha

                    Source: http://www.wavuti.com/

Magazeti ya leo Jumatano 14th November 2012



Afya Ya Ndesamburo Yazua Utata

UTATA umegubika afya ya Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo huku taarifa zikidai kuwa anaumwa na anapatiwa matibabu nchini Uingereza.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Ndesamburo, Waziri wa zamani wa Elimu, Jackson Makwetta inaelezwa kuwa hali yake ni mbaya.

Ndugu wa karibu wa mbunge huyo wa zamani wa Njombe Kaskazini aliyekataa kutaja jina lake gazetini, alisema Makweta alianza kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu  jambo lililosababisha kulazwa katika Hospitali ya Consolata Ikonda iliyopo Wilaya ya Makete Mkoa wa Iringa.

"Hali yake ilianza kubadilika juzi akiwa hospitalini na kulazimika kumhamishia jijini Dar es Salaam ambapo alikodiwa ndege maalumu kwa ajili ya kwenda kupata matibabu zaidi," alisema.

Makwetta aliyetumikia Jimbo la Njombe Kaskazini tangu 1975 hadi 2010 kabla ya kustaafu, alishika nyadhifa mbalimbali ikiwamo Waziri wa Elimu.

Ndesamburo adaiwa kufanyiwa upasuaji

Taarifa zilizozagaa mjini Moshi zinadai Ndesamburo alifanyiwa upasuaji nchini Uingereza na anaendelea vizuri, lakini taarifa nyingine zikidai hajafanyiwa upasuaji bali anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

Ndesamburo hajaonekana katika medani za kisiasa kwa takriban mwezi mmoja sasa na hata kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kilema Kusini Wilaya ya Moshi Vijijini na Nanjara Reha wilayani Rombo hakushiriki.

Mbali na kutoshiriki katika kampeni hizo, mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, hakuhudhuria vikao vya Bunge vilivyomalizika Ijumaa kutokana na kuwapo kwake nje ya nchi.

Habari zisizo rasmi zilizopatikana jana zilidai hata mtoto wa Mbunge huyo, Lucy Owenya aliondoka nchini hivi karibuni kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya kumuuguza baba yake na bado yuko nchini humo.


Habari zilizomkariri mmoja wa ndugu wa karibu wa familia ya Ndesamburo zilidai mbunge huyo ni mgonjwa, lakini kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kutibiwa Uingereza.

“Ni kweli mzee anaumwa, lakini sasa hivi anaendelea vizuri, huo uvumi kuwa hali yake ni mbaya sijui unaanzia wapi,”alisema mwanafamilia huyo aliyekataa jina lake lisitajwe.

Hata hivyo, Owenya ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema alipoulizwa kwa simu na gazeti hili juzi kutoka nchini Uingereza alikanusha baba yake kuugua.

“Nini? Eti unasema?” aliuliza Owenya kwenye simu na baada ya kuelezwa kuna taarifa zimezagaa baba yake ni mgonjwa alijibu kwa kifupi, "Hakuna kitu kama hicho.”

Habari zaidi zilidai kuwa mbunge huyo anatarajiwa kurejea nchini leo na yuko salama tofauti na taarifa zilizozagaa jimboni kwake kuwa ni mgonjwa.

Katibu wa wabunge wa Chadema, David Silinde alisema kuwa ni kweli Ndesamburo anaumwa na yuko nchini Uingereza kwa matibabu.

"Ni kweli yuko Uingereza anaumwa na anaendelea na matibabu ila anaendelea vizuri."

Silinde ambaye pia ni mbunge wa Mbozi Magharibi alisema, Ndesamburo alikuwa nchini Uingereza kwa mapumziko na kuumwa kwake kulitokea huko huko na si kwamba alikwenda kwa matibabu.

"Alikuwa Uingereza kwenye mapumziko na huko huko hali ya ugonjwa ikamtokea," alisema Silinde na kuongeza: "Nitafuatilia nijue anarudi lini kwa kuwa sasa hivi sina taarifa kamili za kurudi kwake."

Na :  Daniel Mjema,Moshi na Boniface Meena, Dar