Tuesday, January 8, 2013

EDWARD LOWASSA AVIPIGA JEKI VIKUNDI SABA VYA VIKOBA MONDULI MJINI

 Mh. Lowassa akikabidhiwa zawadi na mwenyekiti wa Vikoba Kijiji cha Monduli Juu, Dawson Kaaya
wakati viongozi wa vikundi hivyo walipomtembelea nyumbani kwake Monduli.
 Mmoja wa viongozi wa vikundi vya vikoba Kijiji cha Monduli Mjini akisoma risala mbele ya Mh. Lowassa.
 Baadhi ya wanavikoba wa Monduli Mjini wakimsikiliza Mh. Lowassa (hayupo pichani).
Mhe Edward Lowassa akipewa zawadi na Bi Arafa Ismail kutoka katika vikundi vya Vikoba Monduli mjini ambao walikwenda kumtembelea nyumbani kwake. Kushoto kwa Mhe ni Bw. Dawson Kaaya ambaye ni Mwenyekiti wa Vikoba Monduli Mjini.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa amevipatia vukundi saba vya Vikoba vilivyopo Wilayani Monduli, kiasi cha shilingi milioni nane kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao. Lowassa amesema yeye ni mkereketwa mkubwa wa Vikoba huku akisisitiza kuwa ni chachu ya maendeleo na kumkwamua Mtanzania kutoka katika umasikini. Kila kikundi kimepata shilingi millioni moja ambapo kikundi kilichofanya vizuri kimeongezewa shilingi milioni moja zaidi.

SANII WA MNANDA OMAR OMAR AFARIKI DUNIA

MSANII  nyota wa miondoko ya Mnanda 'Mchiriku', Omar Omar, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Habari zilizotufikia ni kwamba, Omar Omar aliyetamba na nyimbo mbalimbali ukiwemo ule maarufu wa 'Kupata ni Majaliwa' alifariki nyumbani kwao Temeke, saa chache baada ya kurejeshwa kutoka Hospitali ya Temeke alipokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.
Taarifa hizo zinasema kuwa mara baada ya kurejea nyumbani, msanii huyo alizidiwa na hatimaye kufariki na msiba wake upo nyumbani kwao Temeke Mikoroshini.
Mwenyezi Mungu Ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi. Amen!

LIONEL MESSI ATWAA TUZO YA BALLON D'OR

                            Lionel Messi akiwa na tuzo yake ya Ballon d'Or.
                       Fabio Cannavaro, akionyesha jina la mshindi wa Ballon d'Or, Lionel Messi.

MSHAMBULIAJI wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, ameshinda tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka wa nne mfululizo.
Messi (25) alifunga jumla ya mabao 91 mwaka jana na aliwashinda wachezaji wengine Andres Iniesta wa Barcelona na Christiano Ronaldo wa Real Madrid.

Messi alitangazwa mshindi wa tuzo hiyo ya the Ballon d'Or, tuzo ambayo hukabidhiwa mchezaji bora wa mwaka katika sherehe iliyofanyika mjini Zurich.
Mesi sasa ni mchezaji wa kwanza kuwahi kushinda tuzo hiyo ya Ballons d'Or kwa miaka minne mfululizo na kuvunja rekodi ya aliyekuwa mchezaji wa Ufaransa na rais wa UEFA kwa sasa, Michel Platini, ambaye alitwaa tuzo hiyo mara tatu mfululizo mwaka 1983, 1984 na 1985.

Hapa chini ni orodha ya kikosi cha wachezaji bora wa mwaka 2012
•Iker Casillas (Real Madrid)
•Dani Alves (Barcelona)
•Gerard Pique (Barcelona)
•Sergio Ramos (Real Madrid)
•Marcelo Vieira (Real Madrid)
•Andres Iniesta (Barcelona)
•Xabi Alonso (Real Madrid)
•Xavi Hernández (Barcelona)
•Cristiano Ronaldo (Real Madrid)
•Radamel Falcao (Atletico Madrid)
•Lionel Messi (Barcelona)


WASTARA; MKE MWEMA ALIYEPIGANIA ROHO YA MUMEWE HADI DAKIKA ZA MWISHO

     Siku ambayo wapendanao hao walifunga ndoa  lakini wastara akawa na kilio cha kupoteza mguu


                                         Siku ambayo walisimamia harusi ya msanii mwenzao
SAFU ya Kali Wiki hii inakuja na tukio lililotikisa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam ambapo tasnia ya filamu kwa mara nyingine ilimpoteza muigizaji wake maarufu, Juma Kilowoko almaarufu kama Sajuki.

Kifo cha Sajuki ni pigo katika tasnia hiyo lakini zaidi kwa mkewe, Wastara Juma ambaye alifanya kila juhudi kupigania uhai wa mumewe hadi dakika za mwisho lakini Mungu akampenda zaidi na kumchukua Januari 2, mwaka huu akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa kwa matibabu.
Hatuwezi kusema mengi sana kuhusu kifo hicho kwani mnajimu maarufu nchini, marehemu Sheikh Yahya Hussein aliwahi kusema kwamba kupinga kifo ni kumkufuru Mungu kwa sababu hiyo ni amri yake.

Lakini ukweli unabaki palepale kwamba Sajuki na Wastara walikuwa ni wanandoa waliopendana sana katika maisha ya ndoa yao ambayo ni mafupi sana kwani walioona Juni 6, 2009 na baada ya hapo mikosi kedekede ikawa inawaandama.
Mateso ndani ya ndoa yao yalikuwa kama ni kupokezana kijiti na kuwafanya kutokwa na machozi ya huzuni. Sajuki ameugua kwa muda mrefu maradhi ya uvimbe tumboni ndiyo chanzo cha matatizo yake yote.

Katika maisha yao ya ndoa, wawili hao wamekuwa wakipokezana mateso huku likiibuka jipya la kuwatoa machozi mara kwa mara na sasa Sajuki ndiye anayewaliza watu kufuatia kusumbuliwa na maradhi ya uvimbe tumboni.

Leo tuwape historia fupi ya maisha yao ya mashaka na huzuni tukianzia Machi 12, 2009 wakati huo wakiwa wachumba tu,  Wastara na Sajuki walipata ajali mbaya ya pikipiki maeneo ya karibu wanapoishi, Tabata, Dar es Salaam ambapo mwanadada huyo alikatika mguu, hapo ndipo huzuni ya wapendanao hao ilipoanza kuwafuata. Walisikitishwa sana na tukio hilo baya katika maisha yao.
Wapendanao hao walifunga ndoa  lakini Wastara akawa na kilio cha kupoteza mguu na kutaka wa bandia ambao ulikuwa na gharama kubwa. Mungu si Athmani kwani walifanikiwa kupata shilingi milioni 7 zilizomfanya mwana mama huyo kwenda Nairobi Kenya na kupata

Historia ya maisha yao inaonesha kuwa Agosti 29, mwaka juzi Wastara alikimbizwa hospitalini na kulazwa kutokana na maradhi ya nimonia ambayo yalimjia ghafla. Lakini uchunguzi ulipofanywa alionekana pia kuwa alikuwa mjamzito, japokuwa mwenyewe alifanya siri.

Habari kwamba Sajuki ni mgonjwa zilivuma Oktoba 29, mwaka 2011 na ikagundulika kuwa alikuwa na uvimbe tumboni na saratani ya ngozi. Baya zaidi gharama za tiba zilikuwa kubwa kwani zilikuwa zikihitajika shilingi milioni sita, na wao kwa kuwa walikuwa hawana, furaha ya maisha ikadidimia
Lakini Mungu naye ana mambo yake kwani Machi 7, mwaka jana wakati fedha za matibabu India zikiwa zimepatikana kwa michango mbalimbal ndoa yao ilipata Baraka za Mungu kwa kupata mtoto. Ni bahati mbaya kwamba furaha yao haikukamilika kutokana na Sajuki kuugua.

Sajuki alifanikiwa kwenda India kutibiwa na Aprili 2, 2012 akarejea nchini kutoka katika Hospitali ya Apollo alikopelekwa kupata matibabu ambapo alisema alikuwa amepata nafuu kidogo kabla ya hivi karibuni hali kuwa mbaya zaidi na kuibua vilio upya kutoka kwa marafiki zake na hasa mkewe Wastara.
Zilisambazwa habari kwa Watanzania kuombwa kumchangia ili arudishwe India kwa matibabu lakini kabla ya mipango hiyo kukamilika Mungu akamchukua alfajiri ya Januari 2, mwaka huu na akazikwa Ijumaa iliyopita katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, mazishi ambayo yaliongozwa na Rais Jakaya Kiwete. Hakika Wastara alipigania roho ya mumewe kwa nguvu zake zote na ameonyesha upendo wa hali ya juu, anafaa kuigwa na wanandoa wengine!


Jackson makala hajafukuzwa bavicha wala chadema

 KAMANDA mpambanaji wa Chadema kutokea Babati Jackson Wilson Makala (pichani juu), amekanusha vikali habari zilizosambaa kwa watu tofauti waliokaribu nae zikimhusisha na sekeseke la kuwavua uanachama wa Baraza la Vijana Chadema ambalo limeleta sintofahamu dhidi yake baada ya  gazeti moja la kila siku kumuandika jana kuwa nae ni miongoni mwa vijana waliosimamishwa kwa muda katika baraza hilo (BAVICHA kwa makosa tofauti ya utovu wa nidhamu.

Katika mawasiliano yake na Blog hii, jioni ya leo Makala ameeleza kusikitishwa na upotoshwaji huo ambao anadai kwa kiasi fulani umemuathiri kwa kuzingatia uaminifu ambao amejijengea miongoni mwa viongozi na wanachama wengine wa chama chake, na watanzania kwa ujumla.

“Napenda kutoa maelezo mafupi kuhusu habari iliyoandikwa na gazeti la jana (jina linahifadhiwa). Mimi Jackson Wilson Makala sijasimamishwa uanachama na Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) kama ilivyotaarifiwa na gazeti hilo. Nimewasiliana na Mhariri wa habari wa gazeti… na amekiri kuwa walifanya makosa makubwa katika habari ile.

Ukweli ni kwamba Baraza la vijana CHADEMA taifa jana mchana limetoa tamko la ufafanuzi kuhusu maamuzi ya Kamati Tendaji ya BAVICHA na hakuna popote lilipotaja jina la Jackson Wilson Makala kuwa amesimamishwa uanachama.

NAPENDA KUKANUSHA KUWA HABARI ZILE NI ZA UONGO NA HAZINA UKWELI WOWOTE!
CHADEMA IS MY LIFE STYLE!” anamaliza kutoa ufafanuzi wake.

Sehemu ya habari hiyo iliyoleta utata kwa kumtaja Bw Makala kimakosa kuwa miongoni mwa vijana waliosimamishwa Chadema ilisomeka hivi ikirejea kikao cha Kamati Tendaji iliyoketi Januari 5, 2013 “Kikao hicho pia kilichukua uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uanachama kwa muda wa mwaka mmoja, Gwakisa Mwakisando (Mbeya), Wilson Makala (Babati) na Joseph Kasambala (Mbeya)”

TAARIFA RASMI YA BAVICHA

Magazeti ya Leo Jumanne 8th January 2013