Friday, August 3, 2012

JEMBE MRISHO NGASA ATUA CHAMA KUBWA SIMBA

Aliyekuwa mchezaji wa Azam,Mrisho Ngassa akiwa ameegemea gari yake aliyokabidhiwa jana mara baada ya kuwasili katika ufukwe wa Coco Beach kwa kuungana na wachezaji wenzake wa Simba baada ya maridhiano ya Azam,Simba na yeye kumalizika

HAKIELIMU WAISHAURI SERIKALI, CWT KUHUSU MGOMO WA WALIMU

 Meneja wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiElimu, Nyanda Shuli (kushoto) akijibu maswali anuai ya wanahabari katika mkutano huo..
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (kulia) akitoa tamko kwa wanahabari kuhusiana na mgomo mchana huu jijini Dar es Salaam. Wa pili kutoka kulia ni Meneja wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiE.
---
Na Joachim Mushi, Thehabari.com

TAASISI ya HakiElimu nchini imeishauri Serikali pamoja na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, ili kumaliza mgomo uliopo kwani waathirika zaidi na mgomo huo si wao bali ni ni wanafunzi.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na mgomo wa walimu unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa, kitu ambacho hawakipati kwa sasa kutokana na mgomo wa walimu wanaoshinikiza Serikali iwaongeze mishahara pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kazi zao.

Mkurugenzi huyo alisema kauli ya Serikali kudai haina uwezo wa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya  watumishi wake haileti unafuu wa maisha kwa watumishi wa umma hivyo kushauri iangalie namna ya kufanya kumaliza mgogoro huo.

“HakiElimu inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu  na kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu walio hoi,” alisema Missokia.

Aidha amewataka walimu kuhakikisha wanadai haki zao huku wakiendelea kuwajibika kwa kufundisha na kuendeleza elimu yetu, kwani wanamgogoro na Serikali na wala si wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“HakiElimu inawakumbusha walimu kuwajibika. Wadai haki zao, huku wakitimiza wajibu wao wa kufundisha na kuendeleza elimu yetu. Wafundishe kwa bidii bila kinyongo, kwa kuwa wasipowajibika watakuwa wanawaumiza wanafunzi na jamii kwa ujumla. Mgogoro uliopo ni baina yao na Serikali, na si wanafunzi,” alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji.

“Viongozi wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa. Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli,” alisema.

Pamoja na hayo ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati mgogoro huo na kutenga muda kujadili suala hilo kwa kina ikiwa ni pamoja na kuishauri serikali, hasa kuhusu tahadhari za kuchukua ili tatizo kama hili lisitokee tena.

“Bunge lina wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu sera, utendaji na usimamizi wa elimu nchini. Inasikitisha kwamba Bunge linakwepa kujadili tatizo hili kwa maelezo kwamba liko mahakamani. Tunaamini kwamba mahakama italiangalia suala hili na kutenda haki, lakini wajibu wa Bunge uko pale pale…” alisema Bi. Missokia.

Amekiri kwamba ni kweli gharama za maisha zinazidi kupanda, huku mfumuko wa bei nao unaendelea kuwaumiza watumishi kila siku, hivyo kuishauri Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kuweza kuwaboreshea mapato watumishi wake.

“Serikali ijijengee utaratibu wa kuboresha mazingira ya watumishi wake, na si kusubiri kwenda mahakamani kuzuia watumishi kugoma. Watumishi wa umma watafanya kazi kwa ari endapo tu wameridhika na mazingira ya kazi na maslahi yao; na si kwa kutumia uamuzi wa mahakama peke yake.”

Picha Mbalimbali za Matukio ya Jana Wilaya Monduli

 Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mh. Edward Lowassa akipatiwa maelezo ya Mifugo hiyo kabla Rais Kikwete hajafika na kuigawa kwa wananchi wa wilaya tatu za Mkoa wa Arusha kama kifuta jasho cha kupoteza kiasi cha mifugo 800,000 kutokana na ukame na athari zake uliozikumba wilaya hizo mwaka 2008/2009.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akiwa katika Mazungumzo na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Mh. Christopher Ole Sendeka.
     
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akisalimiana na kina mama wa Kimasai katika kijiji cha MakuyuniRais Jakaya Kikwete akisalimiana na Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa alipowasili katika kijiji cha Makuyuni,Wilayani Monduli kwa ajili ya kuzindua mpango wa kugawa ng'ombe 1500 kila mwezi kwa wananchi wa wilaya tatu za Mkoa wa Arusha kama kifuta jasho cha kupoteza kiasi cha mifugo 800,000 kutokana na ukame na athari zake mwaka 2008/2009.

Magazeti Ya Leo Ijumaa 3rd August 2012

LISA JENSEN AANZA KUPETA MISS WORLD 2012

MWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Miss World, Lisa Jensen ameanza kufanya kweli katika michuano hiyo baada ya kufanikiwa kuingia kumi bora ya shindano la Top Model, hivyo kumuongezea pointi zaidi kabla ya fainali za kinyang’anyiro hicho.

Habari zilizopatikana kutopka Mongolia ambako shindano la Miss World litafanyika, zimepasha kuwa Lisa alikuwa mwiba mchungu kwa washiriki wengine kutokana na uwezo wake mkubwa, huku akionesha kipaji cha aina yake katika shindano hilo lililofanyika juzi usiku nchini humo. Akithibitisha habari hizi, Afisa Habari wa Kamati ya Miss Tanzania, Haidan Ricco alisema Lisa ni mmoja kati ya wawakilishi watatu kutoka Bara la Afrika ambao wamefanikiwa kupenya na kuingia katika nafasi hiyo muhimu.

Waafrika wengine waliofanikiwa kupenya katika kumi bora ya shindano hilo kabla ya siku ya fainali ya Miss World ni mrembo wa Afrika Kusini na Shelisheli. Lisa amefanikiwa kufanya kweli na kuwatoa kimasomaso Watanzania ambao kwa sasa wanajikuta katika hali mbaya kutokana na wanamichezo wake waliopo katika Michuano ya Olimpiki wakifanya vibaya.

Kutokana na kuingia kumi bora, Lisa bado ana kazi kubwa ya kuhakikisha anapambana ndani ya wiki hii wakati mshindi wa Top Model atakaposakwa rasmi. “Kwetu sisi ni faraja kubwa mno, kwani tunaamini Lisa ataiwakilisha vema Tanzania na huu ni mwanzo mzuri kwake,” alisema Ricco, huku akitaka Watanzania wamuombee kabla ya kufanyika shindano la Miss World hapo Agosti 18, ili aweze kufanya kweli.

Shindano la Miss Tanzania kwa sasa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s, ambacho kinazalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania.

Wanaharakati Waendelea Kupinga Kufungiwa Mwanahalisi, Wengine Waomba Msaada UN.

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDs), wamepinga kufungiwa kwa gazeti laMwanahalisi huku wakiitaka Serikali kuacha kutumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 kwa lengo la kuvifunga mdomo vyombo vya habari.

Mtandao huo unajumiisha wadau 22 ambao ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Haki madini Arusha, Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla (Sahringon), Kituo cha Msaada wa Sheria Zanzibar (ZLSC), Taasisi ya vyombo vya Habari vya Kusini mwa Afrika (MISA), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela).

Wengine ni Jukwaa la Jamii ya wafugaji (TPCF), Waandishi wa Habari wa Haki za Binadamu, (Paicodeo)-Morogoro, (Tufae)- Songea, (Mvuha)-Shinynga, (Chaumta)-Geita, (Mfuma)-Shinyanga, (Jawawavi)-Rukwa, (SNDF)-Shinyanga.

Pamoja na Jukwa la Wahariri (TEF), Chama cha Maalbino Tanzania (TAS), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuia ya Elimu ya Haki za Binadamu na Amani- Mbeya, na PINGOS Forum-Arusha.

Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam ,Mratibu wa mtandao huo, Onesmo Olengurumwa alisema ni wazi kwamba kulifungia gazeti la Mwanahalisi ni lengo la Serikali kutaka kuleta hofu na kuwanyamazisha wapigania haki za binadamu.

“Tunapinga kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi na kwamba tunaitaka Serikali kulifungulia gazeti hilo kwani hiyo ni njama ya kutaka kuwanyamazisha watetezi wa haki za binadamu,” alisema Olengurumwa na kuongeza:

“Tunawataka maofisa wa Serikali ambao wapo kwenye vyombo nyeti vya Serikali kufuata maadili ya kazi na kwamba wasikubali kutumiwa kwa lengo la kutaka kuwanyamazisha watetezi wa haki za binadamu,”alisema.

Olengurumwa alifafanua kwamba THRDs wameamua kuingilia suala hilo kwani wameona nia ya Serikali ni kuvizua vyombo vingine vya habari kutozungumzia masuala nyeti yenye maslahi ya umma.

“Ukiachilia mbali kuwapo kwa Mikataba ya Kimataifa, Katiba ya nchi yetu inatoa uhuru wa kutoa maoni ila bado Serikali yetu imejifanya haioni jambo hilo kwani sheria ya 1976 ni kandamizi na inaondoa Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa kumpa waziri mamlaka ya kufungia gazeti lolote jambo ambalo sio haki kwa vyombo vya habari,” alisema.
Kuchukua hatua. Akizungumzia hatua ambazo zitachukuiwa na Mtandao huo , alisema wao kama watetezi wa haki za binadamu wataendelea kudai haki mpaka pale gazeti hilo litakapofunguliwa.

“Hatuwezi kusema kwamba tutaenda Mahakamani au vipi kwani bado hatujashindwa kudai haki ya msingi ya kufunguliwa kwa gazeti hili na kwamba tutaendelea kupiga kelele kupitia watetezi wa haki za binadamu mpaka pale Serikali itakapolifungua,”alisema.

Waomba msaada UN.
Mtandao huo uliutaka Umoja wa Mataifa (UN), na Mawakala wake ikiwa pamoja na Balozi mbalimbali Tanzania na asasi za kikanda na Kimataifa kuchukua hatua katika suala hilo.

Akizungumizia msaada huo alisema ni wakati kwa Umoja wa Mataifa kuliona jambo hilo kuwa ni la msingi na wanatakiwa kuchukua hatua kwani hiyo ni moja ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kuwanyiwa watanzania uhuru wa kupata habari.

“Tunaamini kwamba UN itachukua hatua dhidi ya jambo hili kwani kumnyima Mtanzania uhuru wa kupata habari ni kinyume na haki za binadamu,” alisema.

Taasisi za Dini
Alisema kwa upande wa Taasisi za dini, wanahabari, watetezi wa haki za binadamu, asasi za kiraia wanapingana na rushwa, ukiukwaji wa haki na utendaji mbovu wa Serikali.

“Tunaomba Taasisi za dini kuungana pamoja kuwatetea watetezi wa haki za binadamu kwani jambo la kulifungia gazeti la Mwanahalisi kwa madai ya kuandika habari za uchochezi sio za kweli,” alisema.
Kubenea anena
Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa kama miongoni wa wadau wa Mtandao wa haki za binadamu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali halisi , inayochapisha Gazeti la Mwana Halisi, Saed Kubenea, alisema siyo vyema kulifungia gazeti hilo kwani habari zinazoandikwa zinafuata maadili na taaluma ya uandishi wa habari.

“Mimi sioni kama gazeti la Mwanahalisi linaandika habari za uchochezi kama zinavyo daiwa lakini hiyo ni njama ya mtu ambaye analengo la kutaka kuwafunga mdomo waandishi wa habari ili wasieleze mambo ya kweli jambo ambalo halikubaliki,” alisema na kuongeza:

“Nipo tayari kufa lakini nitaendelea kutetea haki za watanzania mpaka mwisho wangu,”

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz