Saturday, June 8, 2013

Magazeti ya leo ijumaa 8th June 2013





CHADEMA WAUNGA MKONO RASIMU YA KATIBA MPYA

 Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe amesema chama chake kinaunga mkono rasimu ya Katiba mpya iliyotolewa na Jaji Joseph Warioba.

Mwenyekiti huyo alikuwa akihutubia maelfu kwa maelfu ya wananchi wa jiji la Mbeya katika mkutano wa kumnadi mgombea udiwani wa kata ya Iyela kwa tiketi ya Chadema Charles Nkelwa.Kiongozi huyo wa upinzani bungeni amesema sababu kubwa ya kuunga mkono rasimu hiyo ni kwamba mambo mengi yaliyoorodheshwa na chama hicho yamekubaliwa.

Mbowe amesema jambo kubwa lililofanyiwa kazi ni kurejeshwa kwa serikali ya Tanganyika. Mbowe amesema amesikitika kuona baadhi ya wanaCCM wakiipinga serikali ya Tanganyika na kung'ang'ania serikali mbili na kudai watu hao ni wanafiki wanaopaswa kupuuzwa na wananchi.

Kauli ya Mbowe imekuja wakati ambapo mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Dr Kitila Mkumbo alinukuliwa kusema rasimu mpya ya Katiba iliyotolewa na Warioba ni bora mara mia mbili akilinganisha na katiba ya sasa.Mara baada ya mkutano huo maelfu ya watu walitanda barabarani kumsindikiza kiongozi huyo anayependwa sana jijini Mbeya.

MFULULIZO WA VIFO VYA WASANII WAMFANYA DOKII AFUNGUKE KUWA NI MUNGU ANAWAADHIBU

MWIGIZAJI Bongo, Ummy Wenslaus ‘Dokii’ ameibuka na kusema kuwa vifo vya wasanii vimetokea kutokana na kujisahau hivyo Mungu ameamua kuwaadhibu.

Akiongea na mwandishi wetu katika Viwanja vya Leaders Club, Juni 5, mwaka huu ambapo mwili wa Mangwea ulikuwa ukiagwa, Dokii alisema matukio ya vifo vya wasanii mbalimbali yaliyotokea miaka miwili mfululizo ni pigo kubwa kwani wengi ni vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa kitu ambacho anakiona ni ishara kuwa Mungu anataka kujidhihirisha kwa wasanii.
“Wasanii tulijisahau sana na kuona Mungu hayupo kwani kipindi bado hatujatoka na tunatafuta kutoka kisanaa, tulikuwa tunamuomba kila wakati lakini baada ya kutoka na kuwa mastaa tumemsahau kabisa.

“Hatukumbuki kwenda ibadani tunabaki kuendekeza starehe za dunia tu, hivyo tubadilike kwani Mungu ameanza kujionesha kwetu kwamba yupo,” alisema Dokii.

NAIBU WAZIRI WA JINSIA NA WATOTO AIBUA KASHIFA YA RUSHWA YA NGONO KATIKA CHUO KIKUU CHA DODOMA

Suala la uwepo wa rushwa ya ngono kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) limetinga bungeni.

Suala  hilo Lilijitokeza jana wakati Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), alipomaliza kujieleza bungeni akiomba kura kwa wabunge wamchague awe mjumbe kwenye taasisi hiyo.

Baada ya Mbunge huyo kumaliza kujieleza, alisimama Mbunge wa Viti Maalumu, Naibu Waziri wa Jinsia na Watoto, Ummy Ally Mwalimu aliyemhoji atatoa mchango gani katika kupambana na changamoto kwenye chuo hicho, ikiwamo rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia, ili kusaidia watoto wa kike wasome vizuri.

Kabla ya Mangungu kujibu swali hilo, Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo (CUF), aliomba Mwongozo wa Spika kutaka muuliza swali afute kauli yake kwani ni ya udhalilishaji na inaweza kuleta matatizo.

 Hata hivyo, Spika Anne Makinda aliingilia kati na kusema hakuna haja ya kufuta kauli hiyo kwa vile ndiyo hali halisi iliyopo.