Thursday, March 21, 2013

Meneja Fastjet akamatwa

                                           Wafanyakazi wa shirika la ndege, Fast Jet
Meneja wa wahudumu wa ndege za kampuni ya ndege ya Fastjet, Emma Donavan, amekamatwa na polisi, kuwekwa mahabusu na kuhojiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kumtolea lugha ya matusi mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Polisi walimshikilia na kumhoji Donavan kwa takribani saa tisa kuhusiana na tuhuma za kumtolea lugha ya matusi mfanyakazi huyo raia wa Tanzania.

Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba meneja huyo alikamatwa jana saa 2:00 asubuhi kwa tuhuma za kumtukana mfanyakazi mwenzake, Samson Isembe, ambaye ni Ofisa Mwendeshaji wa kampuni hiyo.

Nyerere, Karume watajwa kesi ya wafuasi wa Ponda

                                          Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere
Shahidi wa utetezi  na Mwanzilishi wa Baraza la Misikiti Tanganyika, Bilali Waikela (87), amedai mahakamani katika kesi inayomkabili Sheikh Issa Ponda na wenzake 49, kwamba  Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Shekhe Abeid Karume, walivunja Umoja wa Waislamu wa Afrika Mashiriki.

Waikela alidai kuwa umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuwatetea na kuwasaidia Waislamu na kwamba Tanzania ilipata kiwanja cha Chang’ombe Marcas kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Misri.

Waikela ambaye ni shahidi wa 48 wa upande wa utetezi katika kesi hiyo alidai kuwa, umoja huo ulifutwa baada ya Karume kudanganywa kuwa wana mpango wa kufanya mapinduzi na kuwarudisha Waarabu Zanzibar.

“Mwalimu Nyerere ndiye aliyemtuma Karume afanye hivyo na mwaka 1964 nilifungwa baada ya kukataa kupokea Shilingi 40,000 ili nikubali kuvunja umoja huo, na  Kassim bin Juma, Adam Simba na Salehe Masasi waliotumiwa kuhamasisha watu kuvunja umoja huo,” alidai.

Alidai kuwa ofisi za umoja huo zilifungwa hadi mwaka 1968 lilipoundwa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na kukabidhiwa ofisi pamoja na mali zote kikiwamo kiwanja cha Chang’ombe markazi kilichokuwa kimejengwa shule ya Waislamu.

CHANZO: NIPASHE

Gakondo wadhamiria kuupa nguvu muziki wa asili

 Katika kuhakikisha wanalinda asili ya nchi yao wasanii nguli  nane wa muziki wa asili nchini Rwanda wameungana na kufanya kazi pamoja kwa lengo la kulinda na kuheshimu kazi yao hiyo.

Wasanii hao wameungana na kujipa jina la ‘Gakondo’ambapo mwanamuziki nguli wa muziki huo nchini humo, Intore Massamba ndiye aliyetoa wazo hilo badala ya kuimba msanii mmoja mmoja.
Kundi hilo lina wasanii mahiri wa muziki huo, Jules Sentore, Daniel Ngarukiye, Michel Ngabo, Manu-teta Kamaliza and Didier Bass-tamfun.

Akizungumza kwenye umoja huo, Massamba alisema kufanya kazi pamoja ni vizuri lakini kwa muziki wa asili ni bora wakafanya pamoja ili kuunusuru muziki huo na kuufanya uwe imara ndani ya jamii.
Alisema wanachofanya kwa sasa baada ya muungano huo ni kuandaa nyimbo ambazo watazirekodi kabla ya kuziingiza sokoni”tunataka kuhakikisha tunaufanya muziki wa asili wa Rwanda uchezwe sehemu mbali mbali Barani Afrika na nje ya Afrika.

Chanzo: Mwananchi

WAFUASI 52 WA PONDA WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MWAKA MMOJA JELA

Washitakiwa 52 kati ya 54 katika kesi ya kula njama na kufanya maandamano isivyo halali wamehukumiwa kwenda jela kila mmoja baada ya kukutwa na makosa matatu huku mmoja akiachiwa huru baada ya kukutwa hana hatia na mwingine kufariki dunia kabla ya hukumu iliyotolewa leo na hakimu Sundi Fimbo wa Mahakama ya Hamimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. 
 
Washtakiwa hao walidaiwa kutenda kosa Februari 15 mwaka huu.

Baada ya pande zote kusikilizwa na washtakiwa kutoa hoja za utetezi, hatimaye hakimu Fimbo alitoa hukumu hiyo leo ambapo aliwatia hatiani washtakiwa 52 kwa makosa matatu kati ya manne na kila mmoja akamhukumu kwenda jela mwaka mmoja kwa kila kosa.