Thursday, November 22, 2012

DKT. Bilal Afungua Maadhimisho Ya Siku Ya Takwimu Afrika

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wananchi wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu waliohudhuria ufunguzi wa maadhimisho hayo baada ya ufunguzi rasmi uliofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam leo.

Picha na OMR

Japani Yaahidi Makubwa Kwa Tanzania

                                         Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada
Serikali ya Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta mbalimbali hasa sekta ya afya na kilimo.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada alipotembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika ziara iliyolenga kusaini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya Tosamaganga iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.

Balozi Okada amesema kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuhakikisha uchumi unakuwa kwa kasi zaidi kwa kukuza biashara baina ya nchi mbili hizo.

 Amesema kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo, ni lazima kipato chao kiongezeke ili waweze kunufaika na kilimo hicho kama shughuli yao kuu ya kiuchumi.

Amesema kuwa Serikali yake inao mpango wa kuisaidia sekta ya kilimo nchili ili kuhakikisha kilimo cha mpunga kinaongezeka mara dufu kwa kuwa nchi ya Japan inasifika kwa uzalishaji wa mpunga duniani.
Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na kuahidi kuziunga mkono juhudi hizo kwa karibu.

Awali katika salamu za Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesifu juhudi za Serikali ya Japan katika kusaidia maendeleo kwa mkoa wa Iringa na kusema ni juhudi za kupongezwa sana.
Amesema kupitia misaada ya Japan, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeweza kupata ufadhili katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, kilimo, maji na umwagiliaji.

Akiongelea maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa kwa kujibu wa utafiti wa mwaka 2008, mkoa wa Iringa ulikuwa na takribani asilimia 16 ya maambukizi, kiwango ambacho ni karibu mara tatu ya kiwango cha maambukizi kitaifa.

Amesema kuwa hali hiyo haikubaliki na zinaihitajika juhudi za pamoja kati ya Tanzania na Japan katika kuendeleza mapambano hayo.
 Aidha, amezipongeza juhudi za Serikali ya Japan za kuisaidia Tanzania katika sekta ya afya na ustawi wa jamii kupitia miradi mbalimbali kwa lengo la kuboresha afya ya mama na familia katika  mkoa wa Iringa.

Balozi wa Japan nchini Tanzania yupo mkoani Iringa kwa ajili ya utiaji saini mkataba wa ukarabati wa hospitali ya Tosamaganga unaogharimu dola za kimarekani 123,339 kwa lengo la kuongeza ubora wa huduma za afya na kupunguza vifo vya wanawake na watoto mkoani Iringa.

 Na. Dennis Gondwe, IRINGA

Anglikana Yateua Askofu Wa Kwanza Mwanamke

 ELLINAH Wamukoya ameteuliwa kuwa Askofu wa Kwanza wa Kike wa Kanisa la Kianglikana barani Afrika. Akiongea muda mfupi baada ya kuteuliwa, Bi. Ellinah Wamukoya amesema uamuzi huo ni heshima kwa kina mama. Ellinah Wamukoya, 61, sasa atahudumu kama askofu mpya wa kanisa hilo katika ufakme wa Swaziland, moja wapo ya nchi zinazokisiwa kufuata siasa za kihafidina. Kutawazwa kwake kumejiri huku Kanisa la Kianglikana, likitarajiwa kujadili ikiwa kina mama wataruhusiwa kuapishwa kuwa maaskofu wa kanisa hilo.
Ellinah Wamukoya ameteuliwa kuwa askofu wa kwanza wa kike wa kanisa la Kianglikana barani Afrika.

Askofu wa jimbo la Capte Town, nchini Afrika Kusini, amesema kuwa wamechukua uamuzi huo ili wawe mfano kwa wengine na pia kuwatakia, viongozi wa kanisa hilo, faraja na hekima ili kujadilia sauala hilo kwa haraka. Kwa mujibu wa ripoti aliyotuma kwa vyombo vya habari, askofu huyo wa Jimbo la Cape Town, Revd. Thabo Makgoba, amesema wimbi kwa sasa linavuma na kuwa wameshuhudia tukio la kihistoria ambao ni sawa na bingu kufunguka.

David Dinkebogile aliongoza sherehe hizo na kukariri kuwa nia yao kuwa ilikuwa kumuapisha askofu na wale sio mtu mweusi, muafrika na raia wa Swaziland. Askofu Wamukoya ni meya wa zamani wa Mji Mkuu wa Swaziland Manzini.

-BBC/SWAHILI.

Magazeti ya leo Alhamisi 22nd November 2012

Askari 10 JWTZ Mbaroni Kwa Mauaji


                                                 Kamanda wa Polisi mkoani wa Mbeya, Diwani Athuman

JESHI la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia  watu 10 wanaodhaniwa kuwa ni askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha 44 KJ  Kambi ya mji mdogo wa Mbalizi  kwa tuhuma za mauaji ya mkazi wa mji huo, Petro Sanga (25).

Askari hao wanadaiwa kumuua Sanga kwa kumchoma kisu shingoni na mdomoni, kisha kuwajeruhi watu wengine sita kwenye Baa iitwayo Power Night, ambako walikwenda kwa lengo la kulipiza kisasi cha kupigwa kwa askari mwenzao, Geodfery Matete (30).

Hata hivyo, Matete anadaiwa kwamba alikuwa amepigwa na walinzi wa kilabu cha pombe cha DDC kilichopo katika mji huo wa Mbalizi, Novemba 18 mwaka huu saa 3 usiku.

Mauaji hayo yamekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar  es Salaam  kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa askari  watatu wa JWTZ na JKT, baada ya kupatikana  na hatia ya kumuua, Swetu Fundikira.

Hata hivyo, askari hao waliohukumiwa kunyongwa, jana waliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika  Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kamanda wa Polisi mkoani wa Mbeya, Diwani Athuman alithibitisha mauaji hayo mapya yaliyotokea katika Mji wa Mbalizi na kwamba marehemu Sanga alikutwa na mauti akiwa anakunywa pombe kwenye baa iitwayo Power Night.

“Marehemu na wenzake walivamiwa na askari hao na kuanza kuwashambulia. Askari hao waliwashambulia wananchi waliokuwapo kwenye baa hiyo na Sanga alifariki dunia baada kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa mateke, mikanda, marungu, sime na mapanga,” alisema Kamanda Athuman na kuongeza:

“Baada ya kumpiga walimchoma  kisu mdomoni. Katika jitihada zake za kujiokoa, marehemu alikimbilia katika baa nyingine ya  Vavenemwe.”

Kwa mujibu wa Kamanda Athuman, baada ya marehemu kufika katika baa hiyo alipoteza fahamu na wasamaria wema walimbeba na kumkimbiza katika Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo katika mji huo mdogo.

“Alifariki wakati akipatiwa matibabu na hiyo ilitokana na kuvuja damu nyingi,” alisema.

 Chanzo cha vurugu

Kamanda Athuman alisema chanzo  cha vurugu hizo, ni askari wa JWTZ, Matete (30)  kushambuliwa na walinzi wa kilabu cha pombe za kienyeji  kilichojulikana kwa jina la DDC Novemba 17 mwaka huu.

Alisema kuwa  kutokana na tukio hilo, Polisi wanawashikilia  walinzi wanne kwa mahojiano zaidi ambao ni Frank Mtasimwa (25), Mure Julius (26), Omari Charles (28) na Regnad Mwampete, wote wakazi wa Kijiji cha Izumbwe Wilaya ya Mbeya.

Kamanda Athuman alisema majina ya askari waliokamatwa kwa tuhuma hizo yatatajwa baadaye kwani bado uchunguzi unaendelea huku akivitaka vyombo vya dola kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Uchunguzi wa tukio hili ukikamilika waliokamatwa watafikishwa mahakamani” alisema.

Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa hana taarifa za wanajeshi hao kufanya mauaji huku akisisitiza kuwa kama wanashikiliwa na Jeshi la Polisi ni wazi kuwa watakuwa wanahusika na tukio hilo.

“Bado sijapata taarifa rasmi kuhusu tukio hilo kwa kuwa hivi sasa sipo katika eneo la kazi, polisi ndio wanaweza kusema lolote na kama kweli wanawashikilia basi watakuwa wamehusika,” alisema Mgawe.

Walioua na rufaa
Wakati huohuo, askari  watatu wa JWTZ, waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana  na hatia ya kumuua Swetu Fundikira, jana wamewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika  Mahakama Kuu ya Tanzania.

Wakili wa askari hao, Mluge Karoli alisema wamewasilisha kusudio hilo la taarifa ya kukata rufaa kwa sababu hawajaridhishwa na uamuzi uliotolewa na Jaji Zainabu Muruke wa   kuwatia hatiani wanajeshi hao kwa kosa la kumuua kwa makusudi Fundikira, kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu.

Karoli akitoa sababu za kuwasilisha kusudio hilo la kukata rufaa alidai kuwa kesi yoyote ya ugomvi  haiwezi  kuwa na kusudio la kutaka kuua na kwamba hakuna shahidi aliyefika mahakamani hapo na kueleza kuwa wateja wake ndio wamemuua Swetu Fundikira.

Pia alienda mbali zaidi na kudai kuwa wateja wake ambao ni MT 1900 Sajini Roda Robert (42), MT 85067 Koplo Mohamed Rashid  wa JKT Mbweni na MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa kikosi cha JWTZ Kunduchi hawakuwa na wajibu wa kuthibitisha mauaji hayo.

“Waliomuua marehemu Swetu siyo wateja wangu na ninaamini  Mahakama ya Rufani itaangalia upya ushahidi na kutenda haki,” alidai Karoli.

Aliongeza kudai kuwa aliyepambana na wateja wake ni Swetu Fundikira na uchunguzi wa daktari unaonyesha jina la Swetu Ramadhani Fundikira hivyo ni watu wawili tofauti na kwamba hakuna hata shahidi mmoja  aliyesema aliwahi kuona mwili wa marehemu ama kuhudhuria kwenye msiba.

Askari hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka huu  saa 7:30 usiku wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki dunia usiku huohuo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Mruke, ilifufua upya msiba wa Swetu, baada ya ndugu zake kuangua vilio, huku chumba cha Mahakama kikigeuka kwa muda kuwa sehemu ya msiba.

Sambamba na vilio hivyo, ndugu wawili wa marehemu Swetu walianguka chini na kuzirai kwa muda, kabla ya kupewa huduma ya kwanza na kurejea katika hali ya kawaida.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Muruke alisema ingwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndio waliomuua Fundikira, ushahidi uliotolewa na  upande wa mashtaka (Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza kuthibitisha mashtaka hayo.

Alisema kuwa anakubaliana na mtiririko wa ushahidi wa upande wa mashtaka kama ulivyoelezwa na mashahidi wake sita akiwamo daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, askari polisi wawili ambao washtakiwa katika utetezi wao walishindwa kuuvunja.

“Sheria iko wazi ukiondoka na mtu au ukionekana naye kwa mara ya mwisho na baadaye mtu huyo akapatikana na madhara, wewe ndio unawajibika kutoa maelezo ya kina kuhusu yaliyompata mtu huyo” alisema Jaji Muruke na kuongeza;

“Kisheria ukitoa maelezo ambayo hayajakidhi haja na yana utata ni faida kwa upande wa mashtaka ambao hutegemea ushahidi wa mazingira. Maelezo ya kina hayajatolewa na washtakiwa wote.”

Aliendelea,  “Ushahidi wa Jamhuri japokuwa ni wa mazingira, umejengwa thabiti na upande wa utetezi haukuweza kujenga matundu, ama kuuvunja mnyororo huo,  kidole kinawaelekea wao.”

Jaji Muruke alisisitiza kuwa katika kesi hiyo licha ya kuwa kuna ushahidi wa kimazingira, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.

“Hivyo kosa wanaloshtakiwa nalo limethibitishwa na Mahakama imewaona washtakiwa kuwa wana hatia ya kumuua Swetu Abdallah Fundikira” alisema Jaji Muruke.

Chanzo:  http://www.mwananchi.co.tz