Friday, August 31, 2012

HEKALU LA MCHUNGAJI GETRUDE RWAKATARE

                                                            Kitanda chake cha kulala



Nimeamini kuwa ukifanya kazi ya Mungu kwa uaminifu naye atakulipa hapa hapa dunia, na utakuwa ushuhuda kwa watu wengine. Mama Getrude Rwakatare siku ya Jumapili alikuwa anahamia rasmi katika nyumba yake mpya iliyoko Mbezi Beach jijini Dar es Salaam pembezoni mwa bahari ya Hindi. Waumini wa kanisa hilo wapatao takribani 300 walifika mahali hapo kwa kushuhudia nyumba ya kifahali.

Mch. Mh. Getrude Pangalile Rwakatare kabla ya kuhamia kwenye hekalu lake jipya alikuwa akiishi Mikocheni B katika nyumba ya kifahali pia. Alizidi kukaa katika uwepo wa Mungu na kufanya kazi yake kwa bidii na kujituma. Katika mahubiri yake kwa waumini wake amekuwa akiwatabiria watu mafanikio na watu wamefanikiwa kutokana na utabiri wake. Leo hii imekuwa zamu kwake ambapo Mungu hakutaka kumuabisha kma mtumishi wake, akamshangaza kwa muujiza wa kumuwezesha kujenga jumba la kifahari kwa gharama kubwa sana

Mwandishi: Rulea Sanga

KAMA WEWE NI SHABIKI WA CHELSEA PATA RAHA.






HAWA NDIO WACHEZAJI WA TANZANIA WALIOWEKEWA PINGAMIZI KUCHEZA LIGI KUU.

Klabu mbalimbali zimewasilisha pingamizi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga usajili wa wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu.
Toto Africans imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.

Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.

Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.

Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani. Nayo Simba inapinga Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
Vilevile Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.

Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.

Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.
Redondo, Luhende, Christopher Edward, Kiggy Makasi na Yondani wawekewa pingamizi kucheza ligi kuu. (Stori imeandikwa na Shaffih Dauda wa shaffihdauda.com )

CHAMA CHA WALIMU IMESEMA HAYA KUHUSU SERIKALI.

Chama cha walimu (CWT) kimesema pamoja na bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na Mahakama kuagiza chama hicho na serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi madai ya walimu, bado serikali haijaonyesha utayari wowote wa kufanya hivyo.

Rais wa CWT Gratian Mukoba amesema chama kimechukua hatua mbalimbali ikiwemo kumwandikia barua katibu mkuu kiongozi zaidi ya mara moja kuonyesha utayari wa CWT kukutana na Serikali kwa majadiliano lakini hadi sasa hakuna taarifa yoyote kutoka serikalini.

Amesema kitendo cha serikali kukaa kimya kwa muda wa siku 27 bila kuonyesha kujali kutekelezwa kwa amri ya Mahakama, kinatafsiriwa na CWT kama ni kukosekana kwa nia njema ya serikali kusikiliza madai ya walimu.

Kwenye line nyingine, CWT kimeitaka serikali kuwaachia huru baadhi ya viongozi wa CWT na walimu wote waliofunguliwa mashtaka ikiwa ni pamoja na kuwarejeshea madaraka walimu 15 waliovuliwa vyeo vyao kutokana na mgomo wa walimu.

Dkt Bilal Ahutubia Mkutano Wa Nchi Zisizofungamana Na Upande Wowote Iran

Makamu wa Rais Dk.Mohammed Gharib Bilal akihutubia Mkutano wa Kumi na Sita wa Wakuu wa Nchi za Siasa ya Kutofungamana na Siasa ya Upande wowote  unaomalizika leo  mjini Teheran, Iran. Katika hotuba yake, pamoja na mambo mengine alisisitiza msimamo wa Tanzania kuendelea kupigania haki, kutetea wanyonge, kupinga ubeberu na ukandamizaji  kote duniani, pia aliiasa Jumuiya ya Kimataifa  kutatua migogoro yote kwa njia ya amani.

 Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais

Sitta: Tishio Chadema Ni Dk Slaa Tu

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM, Samuel Sitta amekiponda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akidai kuwa muda wake wa kutawala nchi bado, kwa kuwa hakina viongozi wa kutosha wa kufanya kazi za Serikali ukimwondoa Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa.

Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya Karagwe, Kagera, alikokuwa katika ziara ya kutembelea ofisi za CCM.

Alisema kuna upungufu mwingi katika safu ya uongozi wa chama hicho, kutokana na kutokuwa na watu wenye uzoefu wa kufanya kazi za Serikali, badala yake akidai kuwa kina baadhi ya viongozi wenye uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki... “Wote hapa mnasikia kwamba Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ni mjuzi wa disko za usiku, sasa huwezi kulinganisha na CCM hata akitoka mtu mmoja chama chetu hakiwezi kuyumba.”

Dk Slaa na Mbowe hawakupatikana jana kuzungumzia kauli hiyo ya Sitta baada ya taarifa kueleza kuwa Mbowe yuko nje ya nchi na alikuwa hapatikani kupitia simu yake ya mkononi kama ilivyokuwa kwa Dk Slaa.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alipinga kauli hiyo akimtaka Sitta aachane na chama hicho kikuu cha upinzani na atumie muda wake kukijenga chama chake ambacho alidai kuwa kina makundi zaidi ya sita.
“Mwaka 2005 tuliweka mgombea Mbowe, mwaka 2010 tukamweka Dk Slaa, mwaka 2015 anaweza akarudi Mbowe, Dk Slaa au mwanachama yeyote wa Chadema,” alisema Zitto.

Alisema Chadema ni taasisi na si chama cha makundi kama ilivyo kwa CCM hivyo hakiwezi kumtegemea mtu mmoja... “Sitta asigombane na Chadema, ajenge chama chake ili tukutane mwaka 2015.”

Akizungumza na viongozi hao wa CCM Karagwe, Sitta alisema hakuna kiongozi mwingine anayeweza kufanya kazi ya kukiongoza Chadema na kukifanya chama kikubalike kwa umma.

“Hawa jamaa hawana hazina ya viongozi kama tulionayo CCM, ambapo tunaweza kusimamisha wagombea 20 wa urais wenye sifa zinazofanana tofauti na wao wanaye Dk Slaa tu ambaye inasemekana aliukimbia upadri.”

Kuhusu CCM
Akizungumzia chama chake, Sitta aliwataka viongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kutokaa kimya na badala yake wajitoe na kujibu hoja za upinzani wanazozitoa kuikosoa Serikali iliyopo madarakani ili ionekane haijafanya mambo ya maendeleo tangu kupatikana kwa uhuru.

“Serikali ya CCM imefanikiwa katika maeneo mengi ya huduma za jamii kama elimu, barabara, afya na mawasiliano, sasa inashangaza kuona viongozi wa chama mnashindwa kufanya mikutano ya kuwaeleza wananchi mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera na ilani ya chama chetu.”

Sitta aliwataka viongozi chama hicho nchini kuepuka mapambano na chuki miongoni mwao lakini akasisitiza kwamba kinaendelea na mkakati wake wa kuwaondoa viongozi wanaodaiwa kuwa ni mafisadi maarufu kwa jina la “magamba”.
Alisema chuki na mapambano yanayoendelea ndani ya chama hicho ndiyo yanayochangia kukidhoofisha na kuwapa la kusema wapinzani na hata kusababisha baadhi ya wanachama kukihama.

“Mapambano ndani ya CCM ndiyo chanzo cha migogoro na mitafaruku inayosababisha viongozi na wanachama wetu kuombeana mambo mabaya na kutoa mwanya kwa watu wetu kuhamia upinzani.”
Sitta yupo katika ziara ya siku tano ya kiserikali mkoani Kagera kukagua miradi mbalimbali inayohusiana na mwingiliano wa uchumi na kijamii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz

Wanafunzi UDSM Waachiwa Huru Na Mahakama


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imewaachia huru wanafunzi 51 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri halali ya askari wa Jeshi la Polisi iliyowataka watawanyike.

Akiwaachia huru wanafunzi hao jana, Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alisema anawaachia huru washtakiwa hao, kwa mujibu wa kifungu cha 225 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), sura ya 20 kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuliendesha shtaka hilo.

Wanafunzi hao waliachiwa huru baada ya Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila kudai kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa na kubainisha kuwa mahakama ilikwisha toa ahirisho la mwisho Agosti 13, mwaka huu.
Mwangamila alidai kuwa waliwasiliana na mashahidi wao ambao ni askari kupitia kwa RCO wa Wilaya ya Kinondoni ,lakini aliwaambiwa kuwa askari hao ni moja kati ya askari waliopo kwenye Sensa ambayo ni muhimu kama kesi hiyo.
Hivyo Wakili huyo wa Serikali aliiomba mahakama itoe ahirisho lingine la mwisho hadi Jumatatu kwa sababu askari hao bado wapo kwenye Sensa ambayo inaisha Jumapili.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Wakili wa Utetezi, Regnal Martin alipinga ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo na kuutaka upande wa mashtaka kuheshimu amri ya mahakama.

Wakili Martin alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa kwa sababu tofauti ikiwemo ya askari hao kuwepo kwenye mgomo wa madaktari wa Julai 12, mwaka huu.

Akitoa uamuzi juu ya hoja hizo, Hakimu Lema alisema baada ya kupitia mwenendo mzima wa kesi , mahakama inajiuliza swali kuwa mashahidi pekee ni hao hao maaskari na kama ni hao upande wa mashtaka ulipaswa kuwasilisha hati chini ya kifungu cha sheria cha 225 (4) cha CPA ambacho kinaeleza tarabu kama shahidi hayupo nini kifuatwe.
Hakimu Lema alisema sababu zilizotolewa na upande wa mashtaka ni za msingi lakini hazikubaliki na kwamba walichokifanya wameidharau mahakama kwa kutofuata taratibu zilizopo.

Aliongeza kuw ana wasiwasi hata kutoa ahirisho lingine la mwisho kwa upande wa mashtaka kwa sababu akitoa ahirisho hadi Jumatatu wanaweza kwenda na sababu nyingine kuwa askari hao wapo kwenye matukio yaliyotokea baada ya Sensa.

Baada ya kuangalia mwenendo mzima wa kesi hiyo, Hakimu aliliondoa shauri hilo kwa mujibu wa kifungu cha 225 (5) sura ya 20 kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuliendesha shtaka hilo.

Wanafunzi walioachiwa huru ni Mwambapa Elias,Evalist Elias, Baraka Monesi, Hellen Mushi, Alphonce Lusako, Matrona Babu, Rolana Wilfred, Godfrey Deogratius , Munisi Denis,Evanos Gumbi pamoja na wenzao 40.

Awali Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya alidai kuwa mnamo Novemba 11 mwaka huu, eneo la Mlimani la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio halali na kusababisha uvunjifu wa amani eneo hilo.

Komanya alidai kuwa washtakiwa hao wakiwa kwenye mkusanyiko huo haramu kwa lengo la kufanya mgomo, askari wa Jeshi la Polisi waliwataka watawanyike, lakini hata hivyo wanafunzi hao walikaidi amri hiyo na kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Hata hivyo washtakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi, walikana mashtaka hayo na waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika ambaye alisaini bondi ya Sh1milioni
www.mwananchi.co.tz

Magazeti ya leo Ijumaa 31th August 2012