Tuesday, September 11, 2012

Simba Mabingwa wachukua kombe 3-2


MAADHIMISHO YA MIAKA 11 YA TUKIO LA UGAIDI NCHINI MAREKANI 'SEPT 11, 2001'

 Mwanamama Rosario Tejada wa Columbia (kulia) akitafuta jina la mpwa wake aliyefariki katika tukio la kigaidi Septemba 11, 2001 leo katika Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTO) jijini New York . Pichani ni waombolezaji wengine waliohudhuria tukio hilo.
 Maria Rodriguez akiomboleza pembeni ya picha za marehemu mkwe wake, Emilio Ortiz aliyefariki katika tukio la ugaidi la Septemba 11, jijini New York.
Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTO) kikiwaka moto baada ya kulipuliwa Septemba 11, 2001.

MAMIA ya Wamarekani leo wameungana tena katika maadhimisho ya kumbukumbu za tukio la ugaidi lililotekea Septemba 11, 2001 katika majiji ya New York na Washington nchini Marekani.
Umati huo ulikusanyika katika maeneo ya Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTO) jijini New York na Makao Makuu ya Kijeshi ya Marekani, Pentagon kusoma majina ya watu zaidi ya 3,000 waliouawawa katika mashambulizi hayo.

Angalia video ya Maandamano ya waandishi wa habari jijini dar leo


Wanahabari Waliondamana Leo Mjini Iringa Kulaani Mauaji Ya Mwangosi







Waandishi wa Mkoa wa Singida Waandamana

 Askari wa usalama barabarani akiongoza maandamano ya wanahabari wa Singida walioandamana kupinga mauaji ya mwenzao
 Baadhi ya waandishi wa habari mkoa Singida-SINGPRESS wakiwa ofisi za klabu wakimsikiliza Mwenyekiti waoo, Seif Takaza
 Mwenyekiti wa SINGPRESS, Seif Takaza(katikati), mratibu wa klabu hiyo Evarista Lucas(kushoto) na Shabani Msangi
Wanahabari wa mkoa wa Singida wakiwa kwenye maandamano kwenye moja ya barabara za manispaa Singida kupinga mauaji ya mwandishi


WANAHABARI Mkoani Singida wameungana na wenzao nchini kwa maandamano ya kulaani na kupinga kitendo cha jeshi la polisi kuhusika na mauaji ya mwandishi wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa Daudi Mwangosi, wakati akiwa kazini.

Kupitia umoja wa klabu yao ya habari mkoa Singida(SINGPRESS),  maandamano hayo yakisindikizwa na askari polisi yalianzia eneo la Benki ya NBC na kuendelea barabara ya Kawawa hadi kituo cha mafuta Esso.

Baadaye yaliingia barabara ya Soko kuu, msikitini, Mghandi, Ipembe, Karume, Kinyeto na kumalizikia kwenye ofisi ya klabu, kabla ya kupokelewa na Mwenyekiti wa SINGPRESS, Seif Takaza.

Akizungumza na waandishi 19 wa mkoa Singida walioshiriki maandamano hayo, Takaza alisema kitendo cha polisi kuhusika na mauaji hayo kimedhalilisha chombo hicho, pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu, kulingana na mafunzo yao ya kijeshi.

“Mauaji ya mwangosi ni ya makusudi, hasa ikizingatiwa alikuwa chini ya mikono ya polisi, lakini mwisho wa siku akafia mikononi mwao….jambo hili lazima lipingwe kwa nguvu zote na watetesi wa haki za binadamu,”alisema.

Alisema mauaji hayo ni ya uonevu, kikatili na yanalifedhehesha taifa ambalo tangu lipate uhuru mwaka 1961 limejipatia sifa kubwa ya kudumu katika hali ya amani na utulivu kiasi cha kuitwa jina la kisiwa cha amani.

Aidha wanahabari hao wameomba kudumishwa kwa mahusiano ya jeshi la polisi na waandishi wa wa habari ili kuondoa uwezekano wa kutokea mauaji mengine kama hayo.

Hata hivyo wananchi wengi, waliyaunga mkono maandamano hayo na kuwakipunga mikono waandishi huku wakitamka neno la ‘Poleni’, kila ambako wanahabari walipita katika barabara mbalimbali za mjini Singida.
Singida
Septemba 11,2012.

Dkt Bilal Akutana Na Wajumbe Wa IPU

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na ujumbe wa Kamati ya ‘Interparliamentary Unity’ (IPU), wakati ujumbe huo ulipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Sept 11, 2012 kwa mazungumzo.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Kamati ya Interparliamentary unity (IPU) baada ya mazungumzo wakati ujumbe huo ulipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo. Sept 11, 2012
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Akiagana na Mbunge wa Bunge la Zimbabwe na Mjumbe wa Kamati ya Interparliamentary unity (IPU), Thabitha Khumalo, wakati akiagana na ujumbe wa IPU baada ya mzungumzo na ujumbe huo, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Sept 11, 2012. Picha na OMR

Endelea Kupata Picha za Maandamano Jijini Dar



                   Wanahabari hawa wakijaribu kukufikishia ujumbe (TAFAKARI)tunaelekea wapi?

Damu Ya Mwangosi Kutegua Unafiki Wa Waandishi?

NIMELIA. Nikalia na kulia tena na tena, kila napoona picha ama kusikia wengine wakimlilia mwandishi mwenzetu.

Nalia zaidi nikiona waandishi waliokuwa karibu zaidi na Daudi Mwangosi, yule mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel 10, aliyekuwa akiripoti kutoka Iringa.

Napata uchungu zaidi napolazimishwa kutazama damu, matumbo, moyo, maini na mapafu ya Mwangosi, binadamu aliyezaliwa, akalelewa, akasoma, akaanza kazi zake, akaoa, akapata watoto wane kupitia tumbo la mkewe, Itika.

Mimi sio daktari, sikuwa na lazima kuyaona maungo ya ndani ya Mwangosi, lakini nimelazimishwa na watu, binadamu kama yeye ambao, wamezaliwa na labda wamezaa ama kuzalisha. Hawa ni kama hayawani, wasiokuwa na chembe ya utu.

Hata daktari, mwenyewe hana ulazima wa kuona matumbo ya mtu, hadi kwa sababu maalum ya upasuaji, tena kwenye tumbo labda.

Wao, kwa tukio hili, wanaonekana wamesomea (sema wamejifunza) kuua. Tena siyo kuua mbwa, wala farasi ama kuku. Hata hivyo, katika kuua huko, hawaelezwi, kuua hovyo hovyo tu wanyama, au kuua yeyote; raia mwema.

Hawakufundishwa kuua waandishi, lakini sijui nini kimewakumba. Sasa wameamua kuanza kuua waandishi. Wameua mjumbe. Hawakuwa hata na huruma, wakakusanyika, wakampiga, tena kama gaidi. Walikuja kama tai, wakamvamia, wakagawana kumshambulia, wengi wakiwa na silaha za kuua.

Kumpiga ngwala, kumshambulia kwa vikalio vya bunduki, haikutosha. Mmoja wao akafyatua…paaaaa. Hiyo paaaa, ikawa chanzo cha kufumua tumbo la Mwangosi na uhai wake ukakoma papo hapo.

Hakika kifo cha mwangosi, kama ilivyo kwa binadamu awaye yote, kinaleta simanzi. Kinasikitisha na zaidi sana kinapotokea kwa kulazimishwa. Tena hiki chake, kimelazimishwa na walinzi wa amani, wenye jukumu la kulinda uhai wake, sasa wao wamekuwa chanzo cha kuuondoa kwa nguvu za ziada na haraka mno.

Nimewaona waandishi wakikusanyika, wakiliaani mauaji hayo. Kila mmoja, hata aliyekuwa adui yake amesimama kulaani mauaji ya Mwangosi. Nimefarijika zaidi kuona makundi mbalimbali ya umoja wa waandishi (hata kama bado, katika maeneo mengi haujaimarika) yakisimama na kulaani mauaji hayo ya kinyama.

Makundi na jumuia nyingi za nje ya Tanzania, zimeibuka na kumlilia Mwangosi. Habari zikasambaa kama moto wa nyika, dunia nzima ikajua na hakuna kilichofichama kwa sasa. Tumsubiri huyo atakayekuja na uongo wake. Tutamsuta, tutamjua siyo mwenzetu. Hakika dunia nzima itamcheka.

Matumaini yangu ni kwamba, pamoja na kumlilia Mwangosi, huenda kifo chake kikaanzisha chachu ya kuwepo kwa umoja zaidi kwa waandishi, kazi zao kuthaminiwa zaidi na kuheshimika.

Kifo hiki kinaweza kuwa njia ya kujitambua kwa waandishi huku kikijenga wigo utakaowapa nafasi ya kuthaminiana zaidi na kuvunja misambaratiko na minyukano isiyokuwa na tija kwao.

Waandishi tumeshuhudia wakinyanyaswa, tena na wenzao; baadhi ya wakubwa katika vyumba vya habari wakishindwa hata kupigania maslahi ya waandishi wanaowajazia habari kwenye vyombo vyao.

Tumeshuhudia waandishi wa mikoani (nje ya Dar es Salaam) wakifiwa na wazazi wao, watoto wao hata wake zao, na vyumba vyao vya habari vikishindwa kuwasaidia hata vipande vya sabuni kusaficha mikono ya wachimba ‘vyumba vya milele’.

Mbaya zaidi Tanzania imeshuhudia vyombo vya habari vikiwakana waandishi wao, hasa –correspondents, wale wa mikoani wanapopatwa na madhila, licha ya kuwafanyia kazi kwa muda mrefu, bila hata kuwaajiri rasmi.

Wanawakana, mara nyingi wanapopata matatizo, ingawa, nina uhakika ikiwa waandishi hao hao wanaowakana, kama wakishinda tuzo za kimataifa za tasnia ya habari, watasimama hata juu ya mapaa wakipaza sauti za kumpongeza na kujipiga kifua kwamba huyo ni mwandishi wao. Poor Bongo journalists.

Wakati wa kubadilika ni sasa. Wakati wa kujenga umoja wenye nguvu ni sasa na wakati wa kuthaminiana ni sasa. Hivi kama wananchi wasiokuwa waandishi wanaonekana kutulilia, iweje sisi tushindwe?

Tuvunje makundi ya ubaguzi ya wahariri kuthamini zaidi wahariri. Waandishi kuthamini zaidi waandishi wenzao, huku pia wakilazimishwa kuwathamini zaidi wahariri wao.
Ulale salama Mwangosi.

Chanzo: http://blog.simonmkina.com

Maandamano ya Wanahabari Leo Hii Jijini Dar




Waandishi wa habari leo wameandamana kwa ajili ya kifo cha Mwangozi. kufuatia maandamano hayo Waziri wa Mambo ya ndani EmanuelNchombi alifika Jangwani kuongea na waandishi wa habari lakini alisomewa sana ikabidi aondoke uwanjani hapo.

Magazeti ya Leo Jumanne 11th September 2012