Friday, October 5, 2012

Ukiamua, hata kwa kubeba zege unaweza kufanikiwa!

WAKATI nasoma sekondari nilitamani sana kufanya kazi ya uandishi licha ya kwamba pia niliamini biashara ingeweza kunifanya nikafika pale ambapo nilitamani kuwepo katika maisha yangu. Kutokana na utashi wangu huo nilijikuta nikiamua kuchagua  kuwa mwandishi na wakati huo huo mfanyabiashara huku nikiamini kwamba kazi hizi zitanipatia mafanikio makubwa.

Mafanikio ni mafanikio licha ya kwamba viwango vya kufanikiwa vinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Kwa mantiki hiyo basi naweza kusema nimefanikiwa kwa kiasi fulani licha ya kwamba nahitaji mafanikio makubwa zaidi.
Labda nikuulize wewe msomaji, ukiulizwa umeamua kuwa nani na kufanya nini katika maisha yako utajibu nini? Naamini kwa swali hilo kila mtu atakuwa na jibu lake. Usishangae ukamsikia mtu akisema ameamua kuwa kahaba na mwingine akakueleza kwamba ameamua kuwa mwizi katika maisha yake.

Lakini pia unaweza kumsikia mtu akisema, ameamua kuwa daktari ama mfanyabiashara katika maisha yake. Kimsingi kila mtu ana chaguo lake. Unachotakiwa kujiuliza ni kwamba je kwa kuwa mwizi au kahaba unaweza kuwa na mafanikio ya kudumu katika maisha yako? Hilo ndilo swali la msingi.

Wakati mwingine inakuwa ni rahisi sana kwa mtu aliyeamua kufanya kazi ya kubeba zege ama kuzibua mtaro kufanikiwa katika maisha yake kuliko yule ambaye hajaamua afanye nini, yaani yupoyupo tu. Hawa ni wale wanaoishi kibubusa ilimradi tu siku zinakwenda.

Ninavyoona ni kwamba, karne hii si ya kuishi kibubusa na kushukuru Mungu kwa kuiona siku nyingine bali unatakiwa kujiuliza baada ya Mungu kukujalia kuiona siku hiyo nyingine utaitumia vipi? Kitu cha msingi ni kujiwekea mikakati madhubuti ya vipi utaendesha maisha yako katika kila siku ya Mungu.

Umefika wakati sasa wa kuamua ufanye nini na uwe nani katika maisha yako la sivyo utabaki kuwa si chochote wala si lolote na mwishowe Mungu ataona hana sababu ya kukubakiza ulimwenguni wakati huna chochote unachokifanya.

Tufahamu kabisa kwamba kama tutashindwa kuamua kuwa nani na kufanya nini hakika tutakuwa hatuna uhakika wa nini tunatafuta katika maisha yetu.

Kimsingi tutakuwa ni watu wa kubahatisha na kufanya kila tutakachoona kinaweza kutuingizia pesa na wakati mwingine kufanya mambo mengine ambayo hayawezi kutupa mafanikio ya kudumu na furaha ya kweli katika maisha.

Hebu anza kujiuliza leo hii bila kujali elimu uliyonayo, jinsi wala umri wako kwamba ni kitu gani ambacho ukikifanya utafurahi na kuona kwamba umetimiza lengo lako la kuletwa hapa ulimwenguni na hatimaye kupata mafanikio?

Katika maisha ukijaribu kuchunguza kwa makini utakuta wengi waliofanikiwa ni wale waliochagua mafanikio. Waliamua kufa na kupona kuhakikisha kwamba wanafika pale ambapo walitaka kufika kwa kufanya kazi mbalimbali.

Hii inadhibitisha kwamba katika maisha kila kitu ni uamuzi na ndiyo maana nadiriki kusema wale ambao wana nguvu za kutosha na afya njema lakini ni maskini, naamini wameamua kuwa maskini katika maisha yao. Watu hao wakiamua kuwa matajiri pia wanaweza.
Kwa kumalizia niseme tu kwamba hakuna hata mmoja wetu ambaye ameletwa hapa ulimwenguni ili awe si lolote wala si chochote. kila mtu ana nafasi yake ambayo akiitumia vizuri ana uwezo wa kuwa na maisha bora na yenye furaha.

Unachotakiwa kufanya ni kuamua ufanye nini katika maisha yako ili uweze kupata mafanikio.

No comments: