Wednesday, February 27, 2013

MAAJABU: KITANDA KIMOJA CHA HOSPITALI YA BUTIAMA HULAZA WATOTO WANNE....

HALI ya hospitali ya Butiama iliyopo wilayani Musoma mkoani hapa, iliyofunguliwa rasmi mwaka 1972 na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere imezidiwa na wagonjwa kutokana na kuachwa kama ilivyoziduliwa enzi za Mwalimu Nyerere. Tanzania Daima limebaini.

Hali hiyo imebainika jana baada ya jopo la waandishi wa habari za afya ya Mama, Baba na mtoto nchini kutembelea hospitali hiyo.

Waandishi hao walitembelea na kujionea hali halisi ya hospitali hiyo yakiwemo mawodi ya wagonjwa na vifaa vilivyopo ndai ya hospitali hiyo huku wakijionea mlundikano mkubwa wa wagonjwa.

Katika wodi ya watoto, walikutwa watoto wawili wawili na wakiwa na wazazi wao katika kitanda kimoja hali ambayo inaonesha jinsi hospitali hiyo inavyokimbiliwa na wananchi huku ikiwa na hali ambayo si salama.

Mbali na wodi hiyo ya watoto kulazimika kulaza wagonjwa wane wane, pia wodi ya wanaume inakabiliwa na udogo wa chumba ambapo kwa sasa wodi hiyo ina vitanda nane tu.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dr. Joseph Musagasa, alisema kuwa hali hiyo imekuwa kama kawaida kwa sasa ambapo inafikia hatua wagonjwa wanapokuwa wengi kitanda kimoja wanalazimika kulazwa watoto wanne.

‘’Kitanda kimoja wanalazwa watoto wanne na hii hali mliyoikuta leo ya watoto wawili wawili kwenye kitanda kimoja ni nafuu’’ alisema Dr. Musagasa.

Alisema kuwa mbali na wodi ya watoto, mpaka sasa kuna vitanda nane tu vya wagonjwa wa kiume ambapo vikijaa vitanda hivyo wagonjwa wengine hulazimika kulazwa sakafuni na kwamba umefika wakati hospitali hiyo inatakiwa kufanyiwa upanuzi wa majengo haraka na vifaa vikiwemo vitanda.

Chanzo: kalulunga blog

No comments: