Tuesday, February 26, 2013

LOWASSA: CCM ITASHINDA 2015

 Waziri mkuu mstaafu na mbunge wa Monduli Moh Edward Lowassa amesema kuwa iwaposerikali zote mbili ile Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na ya visiwani, zitatekeleza  kwa usahihi maelekezo ya mkutano mkuu wa CCM juu ya suala la ajira basi chama hicho kitashinda kiurahisi katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano na Radio Uhuru jijini Dar es Salaam, jana juu ya uchaguzi wa Kenya Mh Lowassa  amesema amefurahishwa kuwa suala la tatizo la ajira kwa vijana limekuwa ni moja ya ajenda muhimu katika uchaguzi huo wa wiki ijayo.

 `Nimefurahi kuwa wenzetu wameliona hili kuwa ni tatizo kubwa nan i ajenda muhimu katika uchaguzi wao.Nimefurahi Waziri Mkuu Odinga alielezea jinsi serikali yao ilivyojaribu kulishughulikia suala hili’’ alisema Lowassa na kuongeza kuwa  ni muhimu kwa nchi za Afrika Mashahriki kutambua rasmi juu ya tatizo hilo.

 Amesema kuwa chama chake cha CCM kimepiga hatua kubwa ya kukiri kuwepo kwa tatizo hilo la ajira kwa vijana, na kimetoa maelekezo kwa serikali zote mbili kulishughulikia.

``Moja ya maazimio ya mkutano mkuu wa CCM ni juu ya suala la ajira na katika kika cha halmashauri kuu hivi karibuni, tulilijadili kwa kina tatizo hili, na kwakweli kama serikali zetu hizi zitatekeleza maelekezo yake, sina shaka yoyote CCM tutashinda kiurahisi 2015’’ alisema .

 Mh Lowassa ambaye amekuwa msemaji mkuu wa suala la ajira kwa vijana akiliita ni bomu linalosubiri kulipuka, aliongeza kuwa , maamuzi ya vikao hivyo yakitekelezwa vizuri vitaifanya CCM iingie kwenye uchaguzi mkuu ikiwanamajibu sahihi yaliyokwishajibiwa juu ya tatizo la ajira kwa vijana.

 `CCM imeanza kulishughulikia ili tusiulizwe na vijana 2015, tuangalie uchaguzi wa Kenya hii ni moja ya ajenda muhimu katika kujinadi’’alitanabaisha.

Amesema kuwa kilimo ni moja ya eneo ambalo linaweza kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo hilo.’’pamoja na kwamba  bado naamini kuwa elimu kabla kilimo kwanza, lakini sekta hii nakubaliana kabisa kuwa inaweza kusaidia kukabiliana na tatizo hili’’ alisema .

 Aidha amesema kuwa  viwanda vikubwa vya nguo ni eneo jingine ambalo linaweza kwa kiasi kikubwa kusaidia upatikanaji wa jira kwa vijana.`` Mkutano mkuu ulizielekeza serikali zetu kujikita katika uanzishwaji wa viwanda vya nguo,hapa tunaweza kukopa kutokana na rasilimali ya gesi tuliyonayo ili kujenga viwanda vya nguo katika maeneo yanayolimwa  pamba’’alishauri na kutolea mfano wan chi ya Ghana ambayo baada ya kubaini kuwa na nishati ya mafuta iliamua kukopa kabla ya kuanza kuyachimba na fedha hizo zikasaidia katika sekta nyingine za kimaendeleo.

 `Hii inawezekana kabisa,  viwanda vya nguo ndiyo vyenye kutoa ajira kubwa,tusingoje mpaka vijana waje kutuuliza 2015’’ alionya Lowassa ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa watu wanaotaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujayo.

 Kauli hiyo ya Lowassa imekuja siku moja tu baada ya  Shirika la utafiti la Synovate kutoa matokeo ya uchaguzi wake yanaoonesha kuwa chama  tawala CCM kimeongezeka umaarufu ambapo asilimia 52 ya wananchi waliyohojiwa wamesema kuwa wangependa kujiunga nacho.Ama kwa upande wake Mh Lowassa kwa mujibu wa utafiti huo umaarufu wake kuelekea 2015 umepanda kwa asilimia sita  na kufikia asilimia 7 akiwa miongoni mwa vigogo watano wa juu wanaopewa nafasi ya kushinda urais iwapo uchaguzi ungefanyika leo.

 Lowassa kwa mujibu wa utaifi huo anataguliwa na Waziri wa Ujenzi John Pombe Magufuli mwenye asilimia 8, Zitto Kabwe wa Chadema na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wenye asilimia 9 na Katibu Mkuu wa Chadema Dr Wilbroad Slah mwenye asilimia 17 akiporomoka kutoka asilimia 42 aliyokuwa nayo miaka miwili iliyopita.

No comments: