Thursday, May 30, 2013

NAIBU SPIKA AAPA KUTOMWADHIBU MBUNGE YEYOTE KWA MADAI KWAMBA AMECHOKA KUITWA ZEZETA

Naibu Spika wa Bunge,Ndugu Job Ndugai amesema kuwa kuanzia sasa hatamwadhibu Mbunge yeyote anayeleta vurugu Bungeni kwakuwa amechoka lawama.

 Akihojiwa na Redio One Stereo katika kipindi cha Kumepambazuka leo asubuhi ,Ndugai amesema kuwa yeye amechoka kuitwa mzembe,zezeta na goigoi na vyombo vya habari.

Ndugai amesema kuwa hata kwa Wabunge waliosababisha tafrani Bungeni jana kiasi cha kuchana Nyaraka za Bunge,hawatachukuliwa hatua yoyote.

 "Kila Mbunge anayeadhibiwa na Kiti cha Spika anaonekana Shujaa. Sisi tunamuona mtovu wa nidhamu,wananchi wanamuona shujaa.Siko tayari tena kwa hilo".alisema Ndugai

Kuhusu uandalizi wa Bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kama hupitiwa kabla ya kusomwa Bungeni,Ndugai amesema kuwa Bajeti hizo zinapaswa kujadili mafungu ya Bajeti husika ya Serikali na si vinginevyo.

"Kwanza hawa wenzetu wanatoka na Bajeti zao nyumbani moja kwa moja na kuja kuzisoma pale.Hawapaswi kutunga za kwao.Wanatakiwa kujadili mafungu ya Bajeti ya Wizara husika tu. Wakati mwingine mtu mmoja anajiandikia tu Bajeti ya Upinzani wenzake hawawezi kumkana Bungeni" alisema kwa hasira Ndugai.

Alipoulizwa kuhusu kutenda haki kwa kuwaadhibu na Wabunge waCCM,Ndugai alikwepa na kuanza kufoka kuhusu Wabunge wa CHADEMA kuwa hawana nidhamu na hatowagusa tena. ‘Watanzania si ndivyo watakavyo….sawa,na sisi tutawaacha ili wasiwe mashujaa!’ alisisitiza Ndugai.

Credit: JF

No comments: