Wednesday, May 22, 2013

Washirika sita wa ‘polisi wa bangi’ wakamatwa wakiwa na magunia 30

                 Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Leberatus Sabas akionyesha bangi iliyokamatwa 

“Siku za karibuni tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna mtandao wa wahalifu wanaoshirikiana na baadhi ya polisi wasiyo waaminifu,” alisema Kamanda Sabas.

Arusha. Polisi mkoani Arusha, imekamata magunia mengine 30 ya dawa za kulevya aina ya bangi kwa watu sita ambao inadaiwa ni washirika wa polisi wawili, waliokamatwa na magunia 18 ya bangi katika maeneo ya Himo mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema watuhumiwa hao, walikamatwa Mei 19 saa 10 jioni katika Kijiji cha Kisimiri juu, Kata ya Ngaramtoni wilayani Arumeru.

“Wakati askari hao, waliokamatwa mkoani Kilimanjaro, polisi mkoani Arusha pia tulikuwa katika msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaoshirikiana na polisi hao, katika biashara ya kusafirisha bangi kutoka Arumeru kupeleka nchini Kenya,” alisema Sabas.

“Siku za karibuni tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna mtandao wa wahalifu wanaoshirikiana na baadhi ya polisi wasiyo waaminifu,” alisema Kamanda Sabas.

“Watuhumiwa hawa walifanikiwa kukimbia kabla ya kukamatwa na kutelekeza bangi hiyo kwenye nyumba zao”alisema Sabas.

Kamanda Sabas alisema uchunguzi wa tukio hilo, ukikamilika watuhumiwa hao, watafikishwa mahakamani.

Habari zilizopatikana baadaye jana kutoka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz kuwa askari wawili waliokamatwa juzi na magunia 18 ya bangi, watashtakiwa katika mahakama za kiraia kama wakosefu wengine.

Wakati huo huo, Kamanda Sabas jana alikiri kuwapo taarifa ya kuuawa Watanzania watatu nchini Kenya kwa tuhuma za ujambazi na kupatikana na bunduki ya polisi aina ya Sub Mashine Gun (SMG).

Watanzania hao,Tigiki Pasto,Steven Webo na mmoja ametambulika kwa jina moja la Kadogoo, waliuawa Mei2, mwaka huu baada ya kuvamia wafanyabiasha na kuwapora na kuwaua wawili.

Hata hivyo, baadaye walizingirwa na wananchi hao na kuuawa na ndipo waliipata bunduki hiyo mali ya polisi.

“Ni kweli tukio hilo lipo, ila sasa kwa kuwa linahusisha nchi mbili, linashughulikiwa kwa taratibu nyingine za nchi na nchi”alisema Kamanda Sabas.

Hata hivyo, alikiri pia kushikiliwa kwa polisi wawili kwa uchunguzi kutokana na kupotea kwa silaha hiyo, kwenye ghala la polisi Wilaya ya Ngorongoro.

No comments: