Thursday, August 30, 2012

CHADEMA- Yapata Pigo Makete

Jumla ya vijana 47 waliokuwa wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) katika kata ya Tandala wilayani Makete wamekihama chama hicho na kujiunga na chama cha mapinduzi (CCM) katika mkutano wa hadhara uliofanyika katani hapo

Mmoja wa vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la Nahom Dovisiana Sanga amesema alijiunga na Chadema mwaka 2011 lakini ahadi alizoahidiwa ikiwa ni pamoja na kusaidiwa kiuchumi haijatekelezwa na ndio maana ameamua kutoka kwenye chama hicho

Naye Imani Nyamike ambaye ni mkazi wa kata hiyo naye amesema kwa upande wake amejiona kama amepotea kutokana na kukosa ushirikiano kwa viongozi wa chama hicho hivyo kujiona mpweke tangu alipojiunga na chama hicho

“Mimi napenda kuwaasa vijana wenzangu ambao mmmedanganyika na CHADEMA ndugu zangu huu ni muda wa kurudi CCM, bibi na babu yangu wapo CCM, baba na mama yangu wapo CCM na mimi nimerudi CCM na nitakufa ndani ya CCM” alisema Nyamike

Akizungumza mkutanoni hapo Katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu amesema chama chake kimefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na vijana hao ya kujiunga na CCM na kusema wao kama chama cha mapinduzi wako tayari kuwasaidia vijana hao na kuwataka kujiunga na kuwa kikundi kimoja ili waweze kupatiwa mikopo ya riba nafuu ili wakuze mitaji ya bishara zao

Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya vijana kujiunga na vyama vyenye sera za uongo pasipo kujua madhara yanayokuja kuwapata mbele na huku akisistiza wananchi waliofika kenye mkutano huo kubakia chama cha mapinduzi ambacho kimepewa dhamana na wananchi kutekeleza sera zake ndani ya wilaya hiyo

“Ndugu zangu naomba niseme CHADEMA hawana adabu, hivi hakuna ambayo jema lililofanywa na CCM hata mkapongeza? Ninyi kila siku ni matusi tu majukwaani, hata kitendo cha wao kuishi kwa uhuru hadi sasa ni jitihada za serikali ya CCM, bado nalo si jema kwenu?” alisema Mtaturu

Mtaturu alitoa bendera za CCM kwa vijana hao na kusema kuwa kwa kuwa tukio hilo la kuhamia CCM limetokea ghafla, atajipanga ndani ya chama chake kufanya sherehe ya kuwakabidhi rasmi kadi za CCM na kuongeza kuwa zoezi hilo litafanywa na uongozi wa mkoa ama taifa

Katika hatua nyingine Mtaturu aliwataka wananchi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa wanaoendelea na zoezi la kuhesabu watu katani humo kwani zoezi hilo bado linaendelea kwa siku saba mfululizo pamoja na wananchi hao kujiandaa kutoa maoni ya katiba mpya pindi tume ya kukusanya maoni itakapofika katani hapo

Naye diwani wa kata ya Tandala Mh. Egnatio Mtawa amewashukuru wananchi wa kata yake kwa ushirikiano wanaompa pamoja na kumuomba katibu wa CCm kusaidia kushughulikia suala la umeme wa gridi ya taifa kufika katani Tandala

Amesema huo ni mpango wa siku nyingi wa serikali kuhakikisha umeme unawaka Tandala hivyo anaombwa kusaidia kuimkumbusha serikali ili mpango huo ukamilike mapema

Chanzo: www.francisgodwin.blogspot.com

No comments: