Thursday, August 30, 2012

Pinda Akwepa Kumjadili Lowassa

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amekwepa kujibu tamko lililotolewa na  Waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa la kuupinga mpango wa Serikali wa kuboresha sekta ya kilimo kupitia mkakati wake wa Kilimo Kwanza.

Wakati Pinda akionyesha kutotaka kulizungumzia suala hilo kwa maelezo kuwa yupo kijijini,  Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imepingana na maelezo ya Lowassa, kwa kueleza kuwa mpango huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba waziri huyo aliyejiuzulu ana sababu zake binafsi.

Mwanzoni mwa wiki wakati akizungumza katika kipindi cha Dakika 45, kinachorushwa na Televisheni ya ITV, Lowassa alisema mkakati huo umekosa mashiko na kwamba kuna haja ya kubadili dhana yake na kuwa, elimu kwanza.
Alisema ni vyema ieleweke kuwa, Serikali inapaswa kutoa elimu kwa wananchi ili  waweze kuboresha mkakati wa kilimo kwanza.

Alisema pamoja na Serikali kuwa na nia nzuri ya kumkomboa mtanzania  kwa kuboresha mazingira ya kilimo, jambo hilo litakuwa si chochote kama mwananchi hatapatiwa elimu itakayomuongoza kwenye mapinduzi hayo ya kijani.

Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri Pinda alisema, “Sijasikia kauli yake, siwezi kulizungumzia hilo kwa sababu sijui (concept) dhana nzima ya alichokisema.”

Hata alipoelezwa dhana ya alichokisema Lowassa Waziri Pinda alisema, “Kwanza nipo kijijini kwa kweli sijasikia na zaidi sijui kuhusu alichokizungumza.”

Wakati Pinda akieleza hayo Wizara ya Kilimo imepinga vikali, kauli ya Lowassa na kueleza kuwa mpango wa kilimo kwanza umefanikiwa kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana hata idadi ya wakulima nchini imeongezeka.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohamed Muya alisema kuwa hivi sasa wakulima wanatumia dhana za kisasa za kilimo na kwamba hali hiyo imepunguza gharama ya kununua chakula kutoka nje ya nchi.

“Mpaka sasa tumepunguza gharama ya kununua chakula kutoka nje ya nchi, hii inatokana na wananchi kuongeza juhudi katika shughuli nzima za kilimo,” alisema Muya na kuongeza:

“Hiyo ni pamoja na kutumia zana za kisasa kwenye kazi hiyo, jambo ambalo limesaidia kuboresha mkakati wa kilimo kwanza.”

Alisema kuwa Lowassa anapingana na mpango huo kwa sababu zake binafsi, “ sijui kwanini anashindwa kukubaliana na ukweli kwamba, sekta ya kilimo imeimarika  tofauti na miaka iliyopita.”

Huku akitolea mfano kilimo cha mahindi alisema, kwa zaidi ya miaka mitano Serikali inazalisha zao hilo, kwamba hali hiyo inatokana na wakulima kupewa elimu ya kutosha juu ya kilimo cha mahindi na mbegu bora.

“Sasa hivi tumeweza kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa, mpango huo unavuka malengo yaliyokusudiwa, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya kuboresha kilimo,” alisema Muya

Alisema Septemba mwaka huu, wanatarajia kufanya mkutano mkubwa wa sekta ya kilimo nchini, lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na wadau kutoka nchi mbalimbali.

“Jambo hili linaonyesha jinsi Serikali ilivyopiga hatua katika mpango mzima wa kilimo,” alisema Muya. CHANZO: MWANANCHI

No comments: