Tuesday, August 28, 2012

Ghasia Mombasa Baada Ya Aboud Rogo Kuuawa

Ghasia zimezuka mjini Mombasa baada ya mhubiri wa kiisilamu ambaye pia alikuwa mshukiwa wa kufadhili kundi la wanamgambo la Al shabaab nchini Somalia, Aboud Rogo, kuuawa kwa kupigwa risasi mjini Mombasa pwani mwa Kenya.

Mtu mmoja inaarifiwa ameuawa na wengine kujeruhiwa katika mtaa wa Mejengo kufuatia makabiliano kati ya polisi na mamia ya watu walioghadhabishwa na kitendo cha kuuawa kwa bwana Rogo ambaye alikuwa mhubiri wa kiisilamu mjini Mombasa

Hali ingali tete wenye maduka wakilazimika kuyafunga maduka yao na watu kukimbilia usalama wao katika mtaa wa Majengo katika maeneo ya kati ya mjini Mombasa.

Inaarifiwa Aboud Rogo,alipigwa risasi asubihi ya leo na kuaawa wakati alipokuwa akimpeleka mke wake hospitalini katika mtaa wa Bamburi mjini Mombasa.Watu wamechoma magari na hata kuvamia maduka huku hali ya wasiwasi ikitanda polisi nai wakifanya kila hali kuweza kutuliza mambo.

Duru zinaarifu kuwa huenda Rogo aliuawa na polisi ingawa ripotio hizi bado hazijathibitishwa.

Anasemekana alipigwa risasi akiwa ndani ya gari lake ambalo lilikuwa limewabeba watu wengine sita, alizikwa baadaye saa za mchana.

Vile vile Rogo alikuwa anakabiliwa ka kesi ya umiliki haramu wa silaha ambapo polisi walidai kuwa alikuwa na njama ya kushambulia kanisa moja la kikatoliki mjini humo.

Aboud Rogo Mohammed alikuwa kwenye orodha ya Marekani na ile ya Umoja wa mataifa ya watu wanaosaidia katika harakati za kundi la wanamgambo wa kiisilamu nchini Somalia la al-Shabab

Kulingana na ripoti ya umoja wa mataifa, Rogo alisaidia kundi la al-Shabab kusajili makurutu wapya. Pia alikuwa anakabiliwa na madai ya njama ya mashambulizi dhidi ya kanisa moja mjini Mombasa.

Kwa mujibu wa taarifa, bwana Rogo alipigwa risasi wakati akiendesha gari lake katika mtaa a Bamburi mjini humo.

Chanzo:  http://www.bbc.co.uk/swahili/habari

No comments: