Monday, August 13, 2012

Prof: Sheriff Na Jenerali Ulimwengu Wakutana Na Tume Ya Mabadiliko Ya Katiba

Mtaalamu wa historia na mwanaharakati wa siku nyingi kutoka Zanzibar, Profesa Abdul Sheriff (kushoto) akifafanua jambo katika mkutano wa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam (Jumatatu, Agosti 13, 2012). Wengine ni Mwenyekiti wa Tume Jaji Mstaafu Joseph Warioba, Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid (kulia).
              
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wameendelea kukutana na kubadilishana mawazo na uzoefu na Wataalam mbalimbali kuhusu Katiba Mpya kwa lengo la kuongeza uelewa wao na leo (Jumatatu, Agosti 13, 2012), kwa nyakati tofauti, Wajumbe wamekutana na Prof. Abdul Sheriff na Ndg. Jenerali Ulimwengu.

Tayari Tume hiyo imeshawaalika na kukutana na kwa nyakati tofauti na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kwanza mzalendo Jaji Mark Bomani, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndg. Pius Msekwa na Mhadhiri wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Issa Shivji.

Prof. Sheriff ni mtaalam wa historia na mwanaharakati wa siku nyingi kutoka Zanzibar na kwa muda mrefu amekuwa akishiriki na kutoa mada katika makongamano mbalimbali yanayohusu Katiba. Ndg.Ulimwengu ni Mwanasheria na Mwandishi wa Habari wa siku nyingi ambaye pia ameshiriki na kutoa mada katika makongamano mbalimbali yanayohusu Katiba Mpya.

Akizungumza wakati akiwakaribisha, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatambua kuwa Tanzania ina wataalam wanaoweza kutoa mchango mkubwa katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba na kuwasihi wanapopata nafasi wasisite kuwasilisha maoni yao kwa Tume.

“Tukipata nafasi, huwa tunawaomba wataalam kama ninyi kuja kubadilishana mawazo na Wajumbe wa Tume. Ni matumaini yangu kuwa Wajumbe wa Tume watafaidika sana na utaalam wako katika kupanua mawazo,” alisema Jaji Warioba katika mkutano uliohudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani, Wajumbe wengine wa Tume na Sekretarieti ya Tume.

Jaji Warioba aliongeza kuwa Tume imejiwekea utaratibu wa kukutana na makundi mengine mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kubadilishana mawazo na kupokea maoni yao kuhusu Katiba Mpya.

Akiongea katika mkutano huo leo (Jumatatu, Agosti 13, 2012), Prof. Sheriff pamoja na kushukuru kwa kualikwa na Tyume, alizungumzia uzoefu wake katika mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea na kutoa maoni yake katika masuala mbalimbali yakiwemo Muungano na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Kwa upande wake, Ndg. Ulimwengu ambaye amekutana na Tume hiyo leo (Jumatatu, Agosti 13, 2012) mchana, pamoja na mambo mengine, alizungumzia umuhimu wa kuandika Katiba Mpya itakayotumiwa na Watanzania kwa miaka mingi ijayo katika kuwaletea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
                                  
                       Picha na Tume ya Katiba

No comments: