Friday, September 21, 2012

Matatizo yetu tuyachukulie kama changamoto kimaisha!

NDUGU zangu, matatizo katika maisha ni kitu cha kawaida sana. Hakuna anayeweza kuyaepuka kwani yapo kwa ajili ya binadamu na ndiyo maana hakuna anayeweza kupitisha siku bila kukumbwa na tatizo aidha dogo ama kubwa. Lakini, utafiti unaonesha kuwa miongoni mwetu wapo watu wanapokumbwa na matatizo hushindwa kuyachukulia kuwa ni kitu cha kawaida, badala yake wanaishia kwenye kuvunjika mioyo na kukata tamaa kabisa ya maisha.

Ni wazi binadamu tunatofautiana katika namna tunavyoyapokea matatizo pale yanapotukabili, lakini baadhi ya watu wanapitiliza katika namna wanavyoyapokea kwani inafikia wakati mtu anapopatwa na tatizo huingia katika hali fulani ya kuona dunia ni mbaya na maisha ni yenye upendeleo.

Anashindwa kuyaangalia matatizo hayo kwa umakini na kuyakubali kisha kuangalia namna ya kuyatatua, hali ambayo huweza kusababisha tatizo kuzidi kuwa kubwa na kumuathiri zaidi.

Katika maisha tunapoingia katika hali kama hiyo ni sawa na kujizuia kusonga mbele katika kupata ama kutafuta kile ambacho tunakitaka katika maisha yetu ya kila siku.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, hali ya kukata tamaa inapopiga hodi katika nafsi zetu huwa tunashindwa kufanya yale ambayo ni ya muhimu kwetu na kuishia kwenye kusononeka.

Wengine wanapopatwa na matatizo badala ya kuyatafutia ufumbuzi, hupandwa na hasira na wakati mwingine kuchukua maamuzi ambayo hayastahili.

Kwa mfano umekuwa katika uhusiano na mtu ambaye ulitokea kumpenda sana lakini ikafikia kipindi ukamkosa aidha baada ya kufariki ama kuachana. Au fikiria umepata barua ya kuachishwa kazi au kama ni mwanafunzi umefeli katika masomo yako yote, hivi utajisikiaje?

Wapo ambao wamefikia hatua ya kukatisha maisha yao kwa kukumbwa na matatizo kama hayo. Lakini je, huo ndiyo ufumbuzi sahihi? Hatuoni kwamba kwa kufanya hivyo ni sawa na kukufuru? Ukweli ni kwamba, matatizo hayachagui mtu, humtokea kila mtu na wakati wowote lakini pia yana ufumbuzi wake. Hivyo basi unapokumbwa na matatizo si vizuri kuanza kunung’unika bali fanya kila uwezalo kutafuta ufumbuzi tena kwa kutumia mbinu sahihi.

Ninachopenda kushauri ni kwamba, kama unasumbuliwa na tatizo fulani si wakati wa kukata tamaa na kuona kwamba huna haki ya kuendelea kuishi.

Fahamu unayo nafasi ya kukabiliana vilivyo na matatizo hayo. Elewa unapokabiliwa na tatizo fulani kisha ukashindwa kutafuta ufumbuzi, unaweza kulifanya tatizo likawa kubwa zaidi ama kuzua tatizo lingine.

Epukana sana na mrundikano wa matatizo ambayo hayakutafutiwa ufumbuzi kwani kwa kufanya hivyo unahatarisha maisha yako lakini pia chukulia kwamba kila tatizo linalokupata ni changamoto tu za kimaisha.

No comments: