Sunday, October 14, 2012

Madabida Ambwaga Guninita Dar

PATASHIKA ya uchaguzi imeendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuchagua wenyeviti wa mikoa, huku baadhi ya wenyeviti wa zamani wakiangushwa, sura mpya kuibuka na wengine wakitetea nafasi zao. Jijini Dar es Salaam, kada wa siku nyingi wa chama hicho, Ramadhani Madabida ameibuka mshindi wa nafasi ya uenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kumbwaga John Guninita aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo.

 Madabida ameshinda kwa kupata kura 310 akimng'oa John Guninita aliyekuwa mwenyekiti, ambaye alipata kura 214 huku Madison Chizii akipata kura 52. Katika uchaguzi huo wajumbe walianza kuingia ukumbini hapo saa 2.00 asubuhi na kuanza kupiga kura saa sita mchana. Awali Madabida alijikuta katika wakati mgumu wakati akijinadi baada ya mjumbe mmoja kumuuliza swali kuhusiana na kiwanda chake kudaiwa kutengeneza dawa bandia za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi za ARV.

 Hata hivyo, Msimamizi wa uchaguzi huo, Assa Simba alimzuia Madabida kujibu swali hilo akisema kwamba haukuwa wakati wake. Awali, akifungua mkutano wa uchaguzi huo, Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal alisema kuwa chama hicho kimelenga kurudisha majimbo yake yote yaliyochukuliwa na wapinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Natumaini uchaguzi utakuwa wa haki bila vurugu zozote, nawaomba msiwe na wasiwasi kwani chama chenu kipo imara kuwakabili wapinzani,” alisema Dk Bilal. Kambi ya Sitta yapeta Habari kutoka mkoani Tabora, zinaeleza kuwa kambi ya Samuel Sitta imeibuka mshindi mkoani humo baada ya mtu anayetajwa kuwa mgombea wake katika nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoani humo, Hassan Wakasuvi kuchaguliwa kukiongoza chama hicho.

 Wakasuvi alichaguliwa katika nafasi hiyo kwa mara ya pili, alipata kura 921 kati ya kura 1012 zilizopigwa, huku Mwamba Z mwamba akiambulia kura 75, ambapo kura 16 ziliharibika. Kimbisa ambwaga Kusila Mzizi wa fitina ndani ya CCM, mkoani Dodoma ulikatwa juzi baada ya Mbunge wa Afrika Mashariki, Alhaj Adam Kimbisa kushinda kiti cha uenyekiti wa chama hicho mkoani humo kwa kumbwaga Mwenyekiti wa zamani, William Kusila.

Baada ya kutangazwa mshindi wa kiti hicho, Kimbisa alisema kuwa bado kuna watu wanaoendeleza siasa za ukabila na kuongeza kuwa jambo hilo ni hatari kwa siasa hasa mkoani Dodoma. Wagombea watatu waliwania kiti hicho, ambapo Kimbisa aliibuka na ushindi wa kimbunga kwa kupata kura 948 katika kura 1198 zilizopigwa akiwaacha Kusila aliyepata kura 216 na Denis Bendera aliyeambulia kura 30.

Ushindi wa Kimbisa ulianza kuonekana mapema juzi asubuhi, baada ya mkutano huo kuanza ambapo wajumbe kutoka wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma walipokuwa wakiingia walikuwa wakiimba wimbo wa kumsifu Kimbisa. Baada ya aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi kumtangaza Kimbisa kuwa ndiye mshindi ukumbi mzima ulilipuka kwa nderemo na shangwe.

Baada ya kutangaza matokeo hayo, Dk Nchimbi aliwaita wagombea walioshindwa, ambapo wote walikubali matokeo na kueleza kuwa uchaguzi ulikuwa ni wa haki, huku Kusila akieleza kuwa ushindi wa Kimbisa ulikuwa ni wa kimbunga. Kimbisa aliwashukuru waliomchagua na kueleza kuwa ubishi wa ukabila kwa mkoa wa Dodoma sasa umekwisha. Hata hivyo, alisema kuwa Mkoa wa Dodoma bado una watu watatu ambao bado wanaendekeza suala la ukabila na kueleza kuwa hao wamefilisika kisiasa.

“Haiwezekani kuendeleza siasa za ukabila katika kipindi hiki cha mitandao, Dodoma bado kuna watu watatu ambao wanaendekeza ukabila, mimi nasema wamefilisika kisiasa na ningeomba muwapuuze kabisa,” alisema Kimbisa bila ya kuwataja kwa majina. Aliwataka viongozi wa CCM ngazi zote mkoani humo, kutengeneza mipango kazi yao na kuiweka wazi kwa ajili ya utekelezaji kuliko kutegemea misaada kwa kila kitu. Mbunge aukwaa uenyekiti Mkoani Morogoro Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Innocent Kalogeris amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa baada ya kumpiga mwereka Injinia Petrol Kingu aliyeshikilia nafasi hiyo kwa awamu mbili.

Uchaguzi huo ulifanyika Oktoba 12 ambapo wajumbe halali waliopiga kura walikuwa 1160 na Kalogeris alipata kura 778, Kingu kura 291 na Hinaya Dimoso alipata kura 86 huku kura zilizoharibika zikiwa 14.

 Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi huo, Zakhia Megid alisema kuwa uchaguzi huo umefanyika kihalali kwa kuzingatia Katiba ya CCM na kuwataka wanachama wa chama hicho kuwaamini waliowachagua. Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Kalogeris aliwataka wanachama na viongozi wengine waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali kuvunja makundi na kuhakikisha kuwa mshikamano unadumishwa ndani ya chama.

Kalogeris alisema kuwa, kazi iliyopo mbele ya viongozi wa CCM ni kuhakikisha Ilani ya CCM inasimamiwa na kutekelezwa ili kukiimarisha chama na hatimaye kiweze kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Aliongeza kuwa kwa nafasi yake ya ubunge na uenyekiti wa CCM, hatakubali kuona mtu ama kikundi cha watu kikipanga mbinu au kufanya mambo yanayoweza kukiweka pabaya chama hicho.

 Alisema kuwa katika kutambua mchango wa viongozi wenzake wakiwamo aliogombea nao nafasi ya uenyekiti, ameamua kumteua Injinia Kingu, Hinaya Dimoso, Said Ally Abdulatif Twalib kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa ili waweze kutoa mchango wao katika chama. Kwa upande wake Injinia Kingu alisema amekubali matokeo na hana kinyongo na WanaCCM kwa kuwa wametimiza haki yao ya kidemokrasia.

Mtopa atetea kiti Lindi Mkoani Lindi, Alli Mohamedi Mtopa amefanikiwa kutetea nafasi yake baada ya kumshinda Ali Hassan Gwaja kwenye uchaguzi uliofanyika jana katika Ukumbi wa Yongolo, wilayani Ruangwa.

 Mtopa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM wa mikoa, ameshinda tena nafasi hiyo katika uchaguzi unaodaiwa kukithiri kwa vitendo vya rushwa na makundi ya wagombea urais wa mwaka 2015. Msimamizi wa uchaguzi huo, Bernald Membe alimtangaza Alli Mtopa kuwa mwenyekiti baada ya kupata kura 523 na kumshinda mpinzani wake pekee Ali Gwaja, aliyepata kura 314.

Hata hivyo, Gwaja hakuwapo ndani ya ukumbi wakati matokeo hayo yakitangazwa huku ikielezwa kuwa alijua mapema kuwa ameshindwa. Mgombea pekee wa nafasi ya Katibu Uenezi wa Mkoa, Ibrahimu Said Mpwapwa alipita bila kupingwa kwa kura za ‘ndiyo’ na nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha ilichukuliwa na Frank Raphael Magali aliyewashinda Mohamed Lidume Lihumbo na Rashidi Hasani Nakumbya.

Mkutano huo uliwachagua wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa ambapo kwa Wilaya ya Nachingwea waliochaguliwa ni Sada Yunus Makota na Maua Mussa Millanzi. Wilaya ya Liwale ni Haji Rajabu Mwenyeji na Fatuma Kilola huku Wilaya ya Ruangwa ni Theodora Elias Mbila na Rashidi Ismail Lipea.

 Wajumbe wa Wilaya ya Kilwa ni Adjut Alli Adjut na Hamisi Omari Ligweje, huku Wilaya ya Lindi Vijijini akiwa ni Ahmad Mussa Mbonde na Hawa Selemeni Nameta ambapo Wilaya ya Lindi Mjini waliochaguliwa ni Aisha Alli Issa na Hamida Abdalah Mohamed. Habari hii imeandikwa na Bakari Kiango, Dar, Hamida Shariff, Morogoro, Christopher Lilai, Ruangwa-Lindi, Habel Chidawali,Dodoma, Tausi Mbowe, Tabora.

              Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz

No comments: