Wednesday, October 10, 2012

MGOMBEA UDIWANI CHADEMA ADAIWA KUPIGWA

POLISI mkoani Arusha imeingia katika kashfa nyingine, baada ya kudaiwa kumpiga mgombea wa udiwani Kata ya Daraja mbili, Prosper Msofe (Chadema).

Msofe anadaiwa kuwa, amepata maumivu ya uti wa mgongo, kutokana na kipigo hicho, ingawa awali kulikuwa na taarifa za polisi kukataa kumpeleka hospitalini.

Hata hivyo baada ya kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu, mgombea huyo alijikuta akipitishwa njia za panya na kufikishwa Mahakama ya Mwanzo, Maromboso na kusomewa mashitaka.

Msofe alifikishwa jana mchana katika Hospitali ya Mount Meru, ambapo alipelekwa moja moja wodi ya majeruhi namba 1, ambapo baada ya kupimwa ilibainika kupata madhara katika mfumo wa uti wa mgongo.

Msofe alipata kipigo hicho siku moja baada ya kulumbana na Wakala wa Matangazo wa Halmashauri ya Jiji la Arusha juzi, akiwa katika eneo la Friends Corner jijini hapa.

Wakala huyo aliyetajwa kwa jina la Ramadhan Karamba (56), alikuwa akiwataka wafanyabiashara ndogo ndogo (machinga), kuondoka katika eneo hilo huku akiamuru mgambo kuwachukulia bidhaa zao.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kwa nyakati tofauti kwamba, wakala huyo hakushambuliwa kama ambavyo imedaiwa na askari polisi.

“Wakati mgombea huyo akijibizana naye, ilikuwa ni saa 1.30 jioni muda ambao tayari ofisi za Manispaa ya Arusha zilikuwa zimekwisha kufungwa, hivyo bidhaa walizokuwa wakichukua walikuwa wanataka kuzipeleka wapi?.

“Huyu wakala wa matangazo ni kwamba, amepata mahali pa kutokea kwa vile yeye ni kada wa CCM na amejua huyu Msofe ni mgombea wa udiwani, ndio maana ameamua kumuuzia kesi kuwa amemjeruhi sisi tulikuwepo hakuna mtu aliyepigwa,” alisema shuhuda mmoja Juma Nassoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas, alithibitisha mgombea huyo kufikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Sabas mgombea huyo alikamatwa jana usiku kwa kosa la kudaiwa kumshambulia wakala wa matangazo wa manispaa, aliyekuwa akiwatangazia wamachinga kuondoka eneo la Friends Corner.

“Msofe alikuwa akimzuia na kisha kuanza kumshambulia, mlalamikaji alifungua jalada namba AR/RB/12648/2012 la shambulio la mwili la kawaida.

“Askari polisi walikwenda eneo la tukio na kumkamata mtuhumiwa, hata hivyo baada ya kufikishwa hapa alikataa dhamana kwa madai anawasilisha ujumbe kwa umma,” alisema.

Jana asubuhi baadhi ya viongozi wa wafuasi wa Chadema na baadhi ya viongozi wa chama hicho walimiminika Makao Mkuu ya Polisi mkoani hapa kwa lengo la kujua hatima ya mgombea huyo wa udiwani.

Hata hivyo katika hali iliyowashangaza wengi badala ya kupelekwa hospitalini, askari polisi hao walimpeleka mahakamani kusomewa shitaka.

Pamoja na kufikishwa mahakamani mgombea huyo, hakuweza kusomewa mashitaka yake kutokana na kudai kuwa, alikuwa anasikia maumivu makali ya mgongo.

Kampeni katika kata hiyo, tayari zimekwishaanza ambapo mchuano mkali ni baina ya Msofe na Philip Mushi wa CCM.

Chanzo: Mtanzania

No comments: