Friday, November 30, 2012

ACHA KUJIKATISHA TAMAA, UNA THAMANI KUBWA KWENYE MAPENZI!

NI Ijumaa nyingine tena tunakutana katika Let’s Talk About Love, lengo likiwa ni lilelile; kupeana elimu zaidi juu ya mambo ya uhusiano na mapenzi. Sina shaka marafiki zangu wote mtakuwa wazima wa afya njema.

Kuna baadhi ya wanawake au wanaume wanakaa kipindi kirefu bila ya kutamkiwa kuwa wanapendwa, kutokana na hali hiyo wanakuwa wapweke na wakati mwingine kufikiria kuwa wao ni wabaya na wasiostahili kabisa kuwa na wapenzi.
Wengine huanza kujiona hawafai kutokana na sababu ambazo wenyewe wanaziweka ambazo kwa kiasi kikubwa huwa za kujikosoa.

Wakati mwingine huanza kufikiria kuwa huenda kwa sababu yupo katika hali fulani ndiyo maana hapati mtu wa kumpenda na fikra nyingine mbaya juu yake ambazo huwa ni za kujikatisha tamaa.

Tambua kitu kimoja, kuna wasichana warembo na wavulana watanashati wengi ambao hawajapata pumziko la kweli katika mioyo yao kwa muda mrefu sasa, wamekuwa wakitafuta watu wenye mapenzi ya dhati kwa muda mrefu bila mafanikio na sasa wamekata tamaa ya kupata wapenzi wa kweli na badala yake wamegeuka vyombo vya starehe.

Wavulana watanashati au wasichana warembo mara nyingi watu wa upande wa pili huwatamani zaidi kuliko kuwa na mapenzi ya kweli, kwa maana hiyo baada ya kushiriki naye ngono mara kadhaa huamua kuachana naye na kumuacha muhusika akiwa na sononeko katika moyo wake.

Watu wa aina hii huachwa na dhiki ya moyo na wakati mwingine hukata tamaa na kuamua kutokuwa na uhusiano mwingine kabisa na wapenzi wapya. Jaribu kufikiri kama kuna mtu wa aina hii ambaye amekuwa akitoneshwa mara kadhaa na wapenzi na wewe ambaye una miezi karibu sita sasa hujapata akupendaye nani mwenye matatizo zaidi? Nadhani jibu yakinifu utakuwa nalo.

Inawezekana wewe ni mmoja kati ya hao ambao wana sononeko la moyo kwa kutopata faraja ya kweli kwa wapenzi wao. Hakika hizi ni mada mbili tofauti lakini leo nitaanza na hili la kutopata mpenzi kwa muda mrefu na sasa umekata tamaa ya kupedwa, kuoa au kuolewa katika siku zote za maisha yako.

Wakati mwingine inawezekana hujafahamu chanzo cha wewe kutopata mpenzi, lakini kuna mambo mengi ya kuzingatia ili uweze kupata mpenzi na hivyo kuepuka upweke katika moyo wako.

JAMBO LA KWANZA
Jiulize mwenyewe, unajijali? Inawezekana ukawa na maswali lukuki kutokana na ninavyouliza swali hilo? Nataka utambue kitu kimoja, kuwa kuna baadhi ya watu hawajipendi! Hivi unadhani kama wewe mwenyewe hujipendi, hujithamini nani atakupenda?

Ninaposema ujipende namaanisha ujipe upendo ule wa kawaida wewe mwenyewe kabla ya kuhitaji upendo wa mtu mwingine. Mwingine anaweza akawa anavaa nguo chafu, hapigi pasi, nywele zipo timtim nani atakupenda kwa muonekano huo?
Hakuna anayependa kuwa na mtu ambaye hana desturi ya usafi kwanza hata kama ni mzuri kiasi gani unapokuwa upo rafu hakuna mtu atakayeusumbua moyo wake kuanza eti kukufikiria wewe usiyejipenda.

Siyo lazima wakati wote uwe ‘smart’, kwa kuwa inawezekana wengine wanafanya kazi ngumu ambazo mazingira yake lazima anakuwa mchafu, lakini baada ya kazi unapaswa kuwa msafi kabisa mbele za watu.

Upande wa wasichana siyo lazima uweke nywele zako dawa au usuke rasta wakati vitu hivyo huna uwezo navyo, unaweza ukasuka nywele zako vizuri au wakati mwingine ukanyoa mtindo mzuri unaokubalika ambao hautakutafsirisha vibaya kwa jamii.

Anza kujipenda kabla ya kuhitaji upendo kutoka kwa mtu mwingine, hiyo itakusaidia kuwa na mvuto na mwonekano mzuri kiasi cha kuweza kumpagawisha mtu mwingine kuanza kuhisi cheche za moto wa mapenzi katika moyo wake.
Nina mengi ya kuzungumza nanyi kuhusu mada hii,lakini kutokana na changamoto ya nafasi finyu, vuta subira hadi wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE! kusoma globalpublishers

No comments: