Tuesday, December 11, 2012

POLISI MWINGINE AUA KWA RISASI

JESHI la polisi nchini limeendelea kuandamwa na mzimu wa mauaji ya raia wasiokuwa na hatia baada askari mmoja kutuhumiwa kumpiga risasi mwananchi na kusababisha kifo.

 Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni katika Kituo cha Polisi cha Ushirimbo Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ambapo askari polisi alimpiga risasi na kumuua kijana aliyefahamika kwa jina la Rashidi Juma (23).

Tukio hilo lilisababisha tafrani kubwa baina ya polisi na wananchi wenye hasira kali kwa kuvamia kituo hicho kwa lengo la kulipiza kisasi kwa kukichoma moto na kutaka askari aliyehusika na mauaji hayo naye auawe.

Hata hivyo, askari walilazimika kutumia nguvu nyingi kwa kurusha mabomu ya machozi, risasi za moto na baridi kwa ajili ya kuwatawanya wananchi hao ambao walikuwa wakirusha mawe kwa lengo la kuwajeruhi askari na  kuharibu mali za kituo hicho.

Chanzo chetu kilidai kuwa tukio hilo lilitokana na askari waliokwenda kumkamata mtu ambaye anadaiwa kuwa ni jambazi, aliyesadikiwa alikuwa amejificha katika nyumba ambayo ipo mtaa wa Kilimahewa mjini Ushirombo na wakafanikiwa kumtia mbaroni.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi walilizingira gari hilo huku wakitaka mtuhumiwa huyo ashushwe ili auawe ndipo polisi walilazimika kufyatua risasi kuwatawanya na moja ikampata kijana Rashidi aliyekufa papohapo.

Vurugu hizo zilitulizwa na Mbunge wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi aliyekuwa na Diwani wa Kata ya Igulwa, Soud Ntanyagalla baada ya kuwasihi kutulia wananchi na ndugu wa marehemu akiwemo mama yake mzazi, Justina Francis  kwa maelezo kwamba watalishughulikia suala hilo.

Mbunge na diwani walifika katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe na kukutana na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk. Archard Rwezahura ambaye alithibitisha kuwa kijana huyo aliyepigwa risasi na polisi alifia mikononi mwa polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, (RPC) Lenard Paul alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri kupata taarifa ya kijana huyo kupigwa risasi na kufa, akaahidi kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya askari aliyehusika.

Na Mwandishi Wetu, Bukombe

No comments: