Thursday, December 13, 2012

TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA MADOLA

TANZANIA itakuwa mwenyeji wa mkutano wa   Vijana wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya ya Madola kuanzia Januari 28 hadi Februari Mosi mwaka huu.

 Hayo yamesemwa (leo)  na  Mkurugenzi  wa Kanda ya Afrika ya Mpango wa Vijana wa  Jumuia ya Madola, James Odit  wakati akizungumza na  Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuhusu  maandalizi ya mkutano  huo.

 Mkurugenzi huyo alisema mkutano utahusisha nchi 22 ambazo ni   wanachama na jumla ya washiriki 60 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo kutoka katika  wizara zinazohusiana na masuala ya vijana, viogozi wa vijana, viongozi wawakilishi wa Baraza la Vijana, wawakilishi wa kimataifa, viongozi wa kikanda wa maendeleo ya vijana na Jumuiya ya Madola.

Miongoni mwa mambo mengine waliyojadiliana ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Vijana na jinsi ya kuunda Katiba ya  Baraza la Vijana la Jumuiya ya Madola.

“Mkutano huu utajadili namna ya kuunda Barazala Vijana la Jumuiya ya Madola(CYC) na program za maendeleo ya vijana na jinsi ya kuwawezesha katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo,” alisema Odit.

 Kwa Upande wake Waziri wa wizara hiyo, Dk. Mukangara alisema  anaishukuru jumuiya hiyo kwa kuichagua Tanzania kuwa mwejeji wa mkutano huo. Huku akisema suala la uundaji wa Baraza la Taifa la Vijana hivi sasa liko katika hatua ya ngazi za juu.

Waziri huyo alizitaja changamoto za kuendeleza mipago mbalimbali ya maendedeleo ya vijana kuwa ni kukosefu wa fedha za kutosha   mfano vile kuwawezesha vijana katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo, kuwajengea uwezo,  kuwapatia ajira, ujuzi na elimu.

 Akifafanua kuhusu suala hilo  Mkurugenzi huyo alisema atalifikisha  suala hilo  kwa wenzake ili waweze kungalia namna ya kuweza kushirikiana.

Waziri Mukangara alishauri  jumuiya hiyo kuangalia namna ya kuweza kushirikiana katika maeneo mengine  ambayo ni sekta ya Michezo, Utamaduni na Habari.

No comments: