Sunday, January 13, 2013

Baruti zauzwa jirani na Ikulu Dar

BARUTI zilizotengenezwa maalumu kwa ajili ya kulipua miamba, sasa zimezagaa katika Soko la Samaki la Kimataifa, lililopo Feri jijini Dar es Salaam, jirani na Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete, zikiuzwa kwa ajili ya kutekeleza uvuvi haramu wa samaki katika Bahari ya Hindi.

Biashara hiyo inadaiwa kufanywa na baadhi ya askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wanaowatumia mawakala, ambao huziuza kwa watu wanaofanya uvuvi haramu sokoni hapo na kutoka maeneo mengine.

Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa biashara hiyo haramu imekuwa ikifanyika zaidi nyakati za usiku na alfajiri kwa takriban mwaka mmoja sasa.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, baruti hizo huuzwa kati ya Sh20,000 hadi 30,000 pamoja na nyaya zake, ambazo huuzwa Sh5,000.

Kitaalamu baruti hutumika katika miradi ya ujenzi wa barabara, migodi ya madini pamoja na jeshini kwa ajili ya kulipulia miamba ya mawe.

Akizungumza na gazeti hili, mfanyabiashara wa soko hilo ambaye alisita kutaja jina lake, alisema kuwa baruti hizo mara nyingi hupatikana asubuhi kwa kuwa usiku wahusika wanakuwa wameondoka.

“Kaka unataka baruti, usijali hiyo kitu umepata, lakini unaweza kuja asubuhi ili kufanikisha dili hilo,” alisema mtu huyo na kuongeza:

“Sikiliza nikwambie, sisi tunauza kwa siri kubwa, ukiona hapa baruti hazipatikani, unatakiwa uende eneo linaloitwa Mjimwema (Kigamboni) na  ukienda huko ujipange vizuri (uje na fedha ya kutosha).”

Kauli ya JWTZ
Akizungumzia madai ya askari wa jeshi hilo kujihusisha katika biashara hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa ni vyema watu hao kama wanafanya hivyo wakawekewa mtego na Jeshi la Polisi ili wakamatwe kwani ni kinyume cha sheria.

Alisema kwamba hawezi kusema kama wanajeshi hawahusiki kufanya biashara hiyo, lakini ni vyema Jeshi la Polisi likaweka mitego ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa, kwani biashara hiyo ni kinyume cha sheria na hairuhusiwi kufanywa.

“Sisi kama wanajeshi, silaha aina ya baruti siyo ambayo tunaitumia sana, lakini, kwa wanajeshi kufanya biashara hiyo ni kinyume cha sheria, hata kama wanazo. Tunaomba kama kuna wanajeshi wanafanya hivyo, polisi waweke mtego ili wakamatwe na wao waache kufanya hivyo,” alisema Mgawe na kuongeza:

“Siwezi kukataa moja kwa moja kama hawawezi kufanya hivyo, sasa ili kukomesha vitendo hivyo, lazima polisi waweke mitego wawakamate, waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.”

No comments: