Tuesday, February 19, 2013

JOHN MNYIKA (MBUNGE) AWAJIBU NAPE NA RIDHIWANI KIKWETE JUU YA ELIMU YAKE

 UTANGULIZI

- Amesoma S/Msingi Mbuyuni (Dar) | Alichaguliwa kwenda Ilboru lakini hakwenda, akaenda Maua Seminary na alipata A tisa | Alisoma A-Level Tambaza | Ana BBA toka UDSM

- Amtaka Ridhiwan aongee na 'mshua' juu ya tatizo la maji Dar!

SASA  ENDELEA>>>>>>>

Nilikuwa katikati ya kazi jimboni nikaambiwa kwamba kuna mwito humu wa Nape na Ridhwan kutaka nieleze elimu yangu. WanaCCM walianza suala hili kwa ari, nguvu na kasi mpya niliposema kwamba nchi imefika hapa ilipo kwa sababu ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na upuuzi wa CCM.

Nikapuuza, naona sasa limeibuka tena kwa ari, nguvu na kasi zaidi baada ya yaliyojiri bungeni kuhusu hoja binafsi niliyowasilisha bungeni kuhusu maji na mkutano wa hadhara wa tarehe 10 Februari 2013 na masuala ambayo niliipa Serikali wiki mbili kuyatolea majibu ama sivyo nitaongoza maandamano ya wananchi kwenda Wizara ya Maji kutaka uwajibikaji na hatua za haraka.

Kwa mara nyingine tena zinafanyika jitihada za kuhamisha wananchi kwenye mjadala kwa kumshambulia mtoa hoja badala ya hoja, sasa ili turejee kwenye mijadala ya msingi ni muhimu niweke kumbukumbu sawa kuhusu masuala kadhaa kama yalivyoombwa.

Elimu yangu sio siri, nimegombea ubunge mara mbili mwaka 2005 na 2010 na mara zote nimeeleza kuhusu suala hili; Nape na Ridhwan wangetumia tu elimu yao wangetafuta kwenye mitandao na kukuta majibu wanayoyatafuta. Nieleze kwa muktasari tu; nimesoma shule ya msingi Mbuyuni Dar Es Salaam (nilikuwa mwanafunzi wa kwanza kwa mkoa wa Dar es Salaam).

Nilichaguliwa kwenda Shule ya Sekondari ya Ilboru wakati huo ikiwa ya vipaji maalum, sikwenda; wito ulinituma kwenda Seminarini. Nilisoma Franciscan Seminary Maua (FRASEMA) mpaka kidato cha nne; nilipata daraja la kwanza; nikiwa na alama A katika masomo tisa.

Ningeweza kwenda shule yoyote ya Serikali ya kidato cha tano na sita yenye mchepeo ambapo ningeutaka; lakini niliamua kubaki Dar es Salaam shule ya Tambaza kwa sababu nilitaka kusoma huku nikiendelea na harakati ambazo nilizianza kabla.

Hapa ndio ilikuwa chanzo cha mimi kuingia kwenye kazi ya kuhamasisha mabadiliko kwenye mimbari nje ya utumishi wa madhabahuni. Tukio lililobadili mwelekeo wa maisha yangu, mwaka 1998 nikiwa kidato cha nne; nimesoma na tumeanza mitihani tukatangaziwa kwamba mitahani yote imefutwa baada ya kuvujishwa.Tukarudishwa nyumbani kipindi hicho nikaenda kwenye mafungo kujitafakari kwenye mkoa mmoja nikarejea Dar es Salaam nikakutana na wanaharakati kadhaa wa asasi zisizo za kiserikali; maelezo kuhusu ufisadi yalinifanya nione nina wajibu kwa nchi yangu, nikarejea Seminarini kufanya mitihani nikiwa na fikra tofauti.

Matokeo yakatoka nimefanya vizuri, kwa mifumo yetu mibovu ya wakati huo kwa mara ya pili tena Serikali hii inayoongozwa na CCM haikutambua vipaji na nikapaswa niendelee kujilipia ada mwenyewe kama ilivyokuwa kwa ngazi nyingine za elimu zilizotangulia; hapa nikakata shauri kwamba nitatumia uwezo na uadilifu wote ambao Mwenyezi Mungu amenijalia kuwezesha mabadiliko katika taifa letu.

Nikaamua kuacha kwenda kwenye shule za bweni mikoani na kubaki Dar es salaam nisome Tambaza huku nikiendelea na kazi za harakati; wakati huo nikihamasisha masuala ya ukombozi wa vijana nchini. Pamoja na kusoma kutwa huku nikifanya kazi nilipata daraja la pili katika kidato cha sita.

Taasisi nilizoanzisha au nilizoongoza katika kipindi hicho na kazi nilizofanya sio siri na zinapaswa kujieleza zenyewe kwa matendo badala ya maneno. Katika kipindi hicho, wakati huo kukiwa hakuna Mfuko wa Elimu wala Bodi ya Mikopo nikashiriki katika ushawishi wa mabadiliko ya kimfumo; nilikwenda Dodoma, tukakutana na wabunge na mawaziri nikawasilisha mada “Towards a more functional education in Tanzania”, wakati huo nikiwa mwanafunzi wa Sekondari.

Kati ya wabunge waliosikiliza mada niliyoiwaisilisha wakati huo sasa ni Rais Jakaya Kikwete ( Ridhwan ukiwa nyumbani unaweza kumwuliza maoni yake aliyotoa siku hiyo kuhusu ugharamiaji wa elimu na suala la mauaji ya mwanafunzi wa Iyunga Michael Sikupya). Nilipotoka kwenye mkutano ule Dodoma mwishoni wa miaka ya tisini, nilikata shauri kwamba mwaka 2005 nitagombea Ubunge hii ni baada ya kushudia aina ya wabunge waliokuwepo.

Mwaka 2002 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Es Salaam kusomea “Bachelor in Business Administration (BBA) kwenye programu ya jioni; nilifanya hivyo kwa kuamua kwa kuwa nilitaka nisome huku nikiendelea na kazi. Mkuu wa Programu hiyo wakati huo alishangaa sana kwa umri wangu (wakati huo shahada hiyo walikuwa wakisoma wazee watu wazima wafanyakazi) na matokeo yangu (kwa kuwa yaliniruhusu kwenda kuingia kusoma katika mfumo wa kawaida). Nikamweleza akanielewa kwamba sitaki kusoma kama wanachuo wengine wa kawaida, uamuzi wangu huo ulikuwa na gharama kwa kuwatafsiri yake ni kuwa nilipaswa kujisomesha binafsi.

Kwa hiyo mimi ni kati ya wale ambao hatudaiwi na nchi hii kwa maana ya kwamba sijawahi kuchukua ruzuku wala kusomeshwa na Serikali hii inayoongozwa na CCM; nimesoma kwa jasho la wazazi wangu na langu binafsi. Kwa hiyo, nijibu tu kuhusu elimu yangu ya juu kwamba nimesoma miaka mitatu Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (mtu aliyosoma kwa kiwango hicho kwenye baadhi ya vyuo duniani hupewa associate degree).

Mwaka 2004 ikaanza misukosuko mbalimbali, mwaka huo ulikuwa ndio unatungwa muswada wa Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, haya matatizo yanayotokea leo niliyatabiri wakati huo. Niliwasilisha mada kwa wanachuo kwenye ukumbi wa Nkurumah kuchambua udhaifu wa muswada huo na kupata maoni ya wanafunzi kuhusu marekebisho yanayohitajika; wanachuo wakapitisha azimio la kwamba muswada huo upingwe.

Kesho yake nikiwa Morogoro kikazi kukafanyika mgomo hatimaye wanafunzi wakapigwa na kukamatwa.Nakumbuka nilikatiza kazi niliyokuwa nafanya nikarejea kwa kuwa Chuo kiliweka sharti kwamba lazima wanachuo waache mgomo ndio waliokamatwa waachiwe. Wakati huo Serikali ya wanafunzi ilikuwa haisikilizwi, mimi na wengine wachache tukajitolea kuzunguka kampasi na hosteli zote kushawishi wanafunzi kurejea masomoni na wakafanya hivyo.

Serikali ya CCM ikatoa maelekezo kwamba kama tumeweza kuwafanya wanafunzi warudi, hata kama sikushiriki mgomo na sihusiki na masuala ya mikopo kwa kuwa ni mwanafunzi ninayejilipia mwenyewe lazima nisimamishwe; nikiwa mwanafunzi pekee wa BBA niliyesimamishwa wakati huo.

Nikarejea baada ya muda tayari kukiwa na mvutano kati yangu na utawala, mwaka 2005 nikaamua kugombea Ubunge wakati huo nikiwa mwanafunzi; mvutano ukaongezeka zaidi. Na utawala wa Chuo ukawa unapata mashinikizo mengi kutoka kwa Serikali na CCM; wengine wakipendekeza nifukuzwe, wengine nifelishwe na wengine nisiruhusiwe kuingia katika maeneo ya Chuo jioni masomoni kwa kuwa nitakuwa nafanya kampeni.

Nikawa katika mtanziko(dilemma) wa kuchagua ama kuendelea na masomo na kujitoa au kupunguza nguvu kwenye kampeni (mbinu nyingi zilitumika wakati huo, sio sehemu ya majibu yangu ya leo) au niendelee na kampeni. Nafsi yangu ikanituma kuamua kuandika barua yakuahirisha masomo, baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005 mazingira yalikuwa yamebadilika sana kuweza kurejea kumalizia mwaka au miezi michache iliyokuwa imebaki.

Mwaka 2006 nikiwa Marekani nilitafakari sana na kufikia uamuzi wa kuendelea na kazi hii ya kusimamia mabadiliko na kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2010. Mwaka 2010 niligombea tena na kushinda wakati huo huo nikiongoza kazi za kitaifa za kampeni makao makuu pamoja na Profesa Baregu na wengine; hakuna mahali popote nilipowadanganya wananchi kuhusu elimu yangu, kama nilivyoeleza hapo juu.

Naamini wananchi wa Jimbo la Ubungo walinichagua kwa uwezo na uadilifu wangu, na walijua pia kwamba nilikuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa miaka mitatu. Naamini elimu ni kitu muhimu sana kwa kiongozi, lakini wapo wenye elimu kubwa ya vyeti lakini hawajaelimika na wapo wenye elimu ndogo sana ya vyeti lakini wanaelewa mkubwa wa kutimiza majukumu yao ya uongozi.

Tangu mwaka 2012 na 2013, nimekuwa kwenye mtanziko mwingine na viongozi wangu ndani ya chama wanafahamu; niliomba kuachia majukumu mengine yote katika chama ili nibaki na ubunge peke yake niweze kuwatumikia wananchi wakati huo huo niendelee na masomo zaidi ya elimu ya juu katika fani inayoendana na kazi ninayoifanya ya sasa na matarajio yangu ya baadaye.

Hata hivyo, kwa mwelekeo huu wa Serikali na CCM leo nieleze tu kwamba nikifanya hivyo itakuwa faida zaidi kwa watawala tunapoelekea mwaka 2015; hivyo, nimeamua kama nilivyoamua mwaka 2005; kwamba nitarejea masomoni baada ya CCM kuondoka madarakani na Tanzania kupata Serikali mpya itakayoongozwa na CHADEMA. Kwa sasa nitaendelea kujisomea kila siku ninapopata wasaa kwa kuwa elimu haina mwisho.

Wakili Ridhwan katika maandiko yake amefanya rejea ya suala Kihiyo wa CCM Temeke, nashauri arejee kwenye hukumu ya kesi ile na marekebisho ya sheria yaliyofanywa na Serikali yaCCM kuwalinda wabunge wake vihiyo baada ya hukumu.

Mifano hailingani kwa sababu mimi sijatoa maelezo ya uongo popote. Lakini hata kwa wabunge wa CCM wanaotoa maelezo ya uongo wa wapiga kura, marekebisho hayo yamewawekea wigo wa mianya yakutokea mahakamani. 

Zamani fomu zakuogembea zilikuwa na mahali pa kujaza elimu ya mgombea, sasa kipengele hicho kimeondolewa. Hivyo, suala la kughushi na kutoa taarifa za uongo haliko kama ilivyokuwa awali, isipokuwa kesi inaweza kufunguliwa ya ukiukwaji wa kawaida wataratibu za kampeni kwa kuwashawishi wapiga kura kwa taarifa za uongo (ndani ya ule muda wa kisheria wa kesi kufunguliwa ambao ulishapita).

Halafu ni jukumu la mlalamikaji sio tu kuthibitisha kwamba uongo ulitolewa bali uongo umeathiri vipi matokeo. Ndio maana leo kuna vihiyo wengi tu wa CCM ndani ya Bunge lakini ni vigumu kuwabana kwa mfumo wetu wa sasa.

 Baada ya majibu hayo marefu, naamini sasa Nape unaweza sasa kurejea kwenye kujibu; Elimu ya Mnyika ina uhusiano gani na CCM kuahidi kwenye ilani yake na kushindwa kutekeleza kwamba ifikapo mwaka 2010 asilimia 90 ya wananchi wa mijini ikiwemo Dar essalaam watakuwa wanapata maji safi na salama? Ridhwan kwa kuwa umeweza kufanya rejea unaweza pia kueleza ni kwanini Rais Kikwete mwaka 2011 aliahidi kuwa tatizo la maji Dar es Salaam litakuwa historia mwezi Februari 2013 lakini mwezi huo umefika na matatizo bado ni makubwa?

No comments: