Friday, April 12, 2013

TATIZO LA ELIMU TANZANIA SIYO VIBOKO.....BORESHENI MIUNDO MBINU KWANZA BADALA YA KUFIKIRIA KUTEMBEZA VIBOKO

 Taifa liko katika wakati mgumu juu mustakabali wa sekta ya elimu kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili.  Kuna mengi yanazungumzwa, yamependekezwa na mengine bado yanaendelea kutolewa juu ya njia sahihi ya kukoa elimu ya watu wa taifa hili.

Kuna hoja zinatolewa kwamba sekta ya elimu imeachwa kuporomoka hadi kufikia hali mbaya ya sasa kutokana na kuminywa kwa bajeti ya sekta hiyo, matokeo yake ni janga la kufeli kwa wananfunzi wengi katika mitihani yao kama ilivyodhihirika kwa wanafunzi wa kidato cha nne waliomaliza elimu ya sekondari mwaka jana kwa zaidi ya asilimia 60 kupata daraja sifuri.

Ukiacha suala la kufeli, kuna hoja za kweli na zenye mashiko zinazojengwa kwamba wanafunzi wengi wanaomaliza viwango mbalimbali vya elimu, kuanzia msingi, sekondari hadi vyuo vya elimu ya juu, hawafanani na matarajio ya watu kwa kuwa na uwezo wa kielimu kwa waliopita kwenye ngazi hizo za elimu.
Wapo wanafunzi wanamaliza darasa la saba bila kujua kusoma wala kuandika, lakini wanafaulu mtihani wa kuendelea na elimu ya sekondari; wapo wanaomaliza sekondari, lakini hawawezi hata kuandika sentensi moja iliyonyooka.

Kuna mgogoro mkubwa sana wa mitalaa ya elimu, mgorogo huu umejadiliwa kwa mapana yake na wadau wa elimu, ulifikishwa bungeni, lakini serikali kwa kutumia mlango wa nyuma iliikimbiza hoja hiyo kutoka bungeni kabla ya kupata mjadala wa kina ili ufumbuzi upatikane kwa nia ya kuokoa elimu ya nchi hii.

Katika harakati hizi na kizunguzungu katika sekta ya elimu, Waziri Mkuu ameunda Tume kuchunguza chanzo cha anguko kubwa la elimu kutokana na taifa kushtushwa na matokeo mabaya ya kidato cha nne kuliko mengine yote ambayo yamepata kuikumba nchi hii tangu uhuru.

Wakati hali ya elimu ikiwa katika mkanganyiko mkubwa, juzi Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliibuka na kusema kuna mpango wa kurudisha viboko pamoja na kupiga marufuku wanafunzi kumiliki simu shuleni kama njia ya kuokoa sekta ya elimu nchini.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam katika hafla ya utambulisho wa tovuti ya www.shuledirect.co.tz ambayo
imeanzishwa na aliyewahi kuwa Miss Tanzania 2004, Faraja Kotta, huku akisisitiza kuwa wanafunzi wasipopigwa viboko, mambo hayaendi, ndiyo maana mwanafunzi anaingia darasani saa tatu yaani muda anaoutaka yeye, lakini anaachwa tu bila kuadhibiwa, matokeo yake wakifeli wizara inalaumiwa.

Inawezekana Mulugo ana hoja, kwamba maisha ya binadamu bila utaratibu na makubaliano yanayojenga wajibu mambo hayaendi, kwa maana hiyo kuibua hoja ya kucharaza wanafunzi fimbo, kunaweza kutajwa kuwa ni sehemu mojawapo muhimu ya kujenga uwajibikaji kwa wanafunzi katika kutimiza wajibu wao. Hili linawezekana na linajadilika.

Naibu Waziri huyu hapana shaka anasukumwa na uzoefu wa alikotoka, kwamba zamani wanafunzi walikuwa wanacharazwa viboko ndiyo maana walikuwa na nidhamu, walikuwa wanasoma kwa bidii, walifaulu vizuri na kwa maana hiyo taifa halikuwa na aibu kama hii ya kufeli kwa wanafunzi kwa kiwango hicho.

Pamoja na hoja ya Naibu Waziri kuwa na msimamo huo, fimbo pekee hazikwezi kupandisha ubora wa elimu, fimbo haziwezi kuokoa elimu kama tabia ya nchi hii kuhusu uwekezaji finyu katika sekta ya elimu itaendelea kuwa kama ilivyo sasa.

Kabla ya serikali kufikiria habari ya fimbo tungefarijika kama ingetambua kuwa ina kazi nzito na ngumu kufanya katika kurejesha sekta ya elimu katika mstari wake.

Hali ya shule nyingi ni duni mno, hakuna walimu, hakuna vifaa vya mafunzo, walimu hawana motisha yoyote ya maana, ujira wao ni wa kijungu jiko mazingira ya kazi kama nyumba za kuishi hazipo, heshima kwa walimu kutoka kwa serikali yao na hata kwa jamii hakuna kabisa.

Kwa miaka mingi serikali imekuwa inaahirisha matatizo ya sekta ya elimu, malalamiko ya walimu yamepuuza kwa kitambo kirefu sasa, shule nyingi za umma zimegeuka kuwa mahame, siyo mahali panapompa mwanafunzi motisha ya kusoma na kujifunza kwa bidii.

Viongozi wengi ambao wamepewa jukumu la kusimamia sekta ya elimu wamegeuka kuwa waigizaji badala ya kuyakabili matatizo ya elimu kisayansi. Kwa kifupi hali ni mbaya katika sekta ya elimu.

Ni kwa kuangazi haya tunaamini kabla ya Mulugo kuanza kuzungumzia habari ya kurejesha viboko shuleni, angeangazia kwanza matatizo ya kumsingi ya sekta hii.

Wenzetu waliopiga hatua ni marufuku hata kumfokea mwanfanzi achilia mbali kucharazwa bakora, viwango vyao vya elimu viko juu. Shule nyingi za binafsi haziruhusu viboko hapa nchini, viwango vya ufaulu katika shule hizo uko juu mno kulinganisha na za umma ambako pamoja na bakora kuwa ruksa kwa utashi wa mwalimu, ziko chini kwa ubora.

Ni hali hii tunawaomba viongozi wa sekta ya elimu wajaribu kusumbua vichwa vyao zaidi kupata majibu ya maana kuhusu changamoto za elimu nchini.

---
Mhariri,
Nipashe.

No comments: