Thursday, April 4, 2013

WATUHUMIWA 11 WA GHOROFA LILILOANGUKA DAR WAFIKISHWA MAHAKAMANI...

 Mtuhumiwa namba moja wa mashitaka 24 ya kuua bila kukusudia Raza Hussein Ladha (aliyevaa kanzu nyeupe) na watuhumiwa wenzake 10, wamepandishwa kizimbani leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

 HABARI  2  MUHIMU:

    Hakimu aagiza mtuhumiwa wa wa mauaji ya padre Evaristus Mushi

Hakimu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Isaac Sepetu, ameagiza mtuhumiwa Omar Yusuf Makame wa mauaji ya Padre Evaristus Mushi afikishwe mahakamani mara moja siku ya Jumatatu wiki ijayo, ikiwa ni pamoja na nyaraka zinazoeleza ni kwa nini hakupandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka ndani ya saa 24 kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 390 cha mwenendo wa makosa ya jinai, sura na. 7 ya mwaka 2004. Maombi ya kufikishwa mahaknani yametoka kwenye jopo la mawakili watetezi wa mtuhumiwa.

    Watuhumiwa wa jengo lililoporomoka mtaa wa Indira Gandhi, Dar, wafikishwa mahakamani



                                           Watuhukiwa wakiondoka mahakamani baada ya kusomewa mashitaka

11 KORTINI KWA MAUAJI YA KUANGUKA KWA GHOROFA
Imeandikwa na  Happiness Katabazi via blog

HATIMAYE mfanyabiashara Razah Hussein Ladha na wenzake 10 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam tarehe 3 Aprili 2013, wakikabiliwa na jumla ya makosa 24 ya kuua bila kukusudia.

Mbali na Razah washitakiwa wengine ni Godluck Mbaga, Wilbroad Mugabisyo, Ibrahim Kisoki, Mohamed Abdubakari, Charles Salu, Zonazea Anage,Vedasto Ferand, Michael Hemed  Hemed, Albert  Jones na Joseph  Ringo ambao waliletwa jana saa  nane mchana chini ya ulinzi mkali wa wanausalama ambao walikuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Ilala (RCO), Duwani Nyanda.

Mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka mawakili waandamizi wa serikali waliokuwa wakiongozwa na Bernad Kongora, Tumaini Kweka, Lasdlaus Komanya, Peter  Mahugo, Kinyeshi waliwasomea mashitaka hayo kwa kupokezana.

Wakili Kongora alidai mashitaka yote hayo 24 yanayowakabili washitakiwa wote yanafanana na kwamba wanakabiliwa na makosa ya kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa   mnano Machi 29 mwaka huu huko katika eneo la Mtaa wa Indira Gandhi waliwaua watu 24 bila kukusudia.

Hata hivyo wakili Kongora aliwataka washitakiwa hao wajibu chochote kwakuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ni Mahakama Kuu na kwamba upepelezi bado haujakamilika na kwamba wanaomba mahakama isiwapatie dhamana kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuwapatia dhamana.


Hata hivyo mawakili wa utetezi zaidi ya saba ambao Jerome Msemwa, Adronicus Byamungu ,John Mhozya waliomba mahakama hiyo iwapatie dhamana na washitakiwa wanao wadhamini wakuaminika kwasababu tayari kuna maamuzi mbalimbali yalishatolewa na mahakama ya Rufaa na mahakama Kuu katika kesi za makosa ya kujaribu kuua. Mahakama hizo zilisema mahakama za chini zina mamlaka ya kutoa dhamana kwa kesi ambazo zinafunguliwa kwanza mahakama ya chini na kisha zinakuja kuamishiwa mahakama kuu kwaajili ya usikilizwaji.

Hata hivyo mawakili wa Serikali walipinga maombi hayo kwa maelezo kuwa maamuzi hayo ya mahakama rufaa yalitolewa kwenye kesi ya kujaribu kuua wakati kesi inayowakabili washitakiwa hao ni kuua bila kukusudia na kusisitiza kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na hivyo haina mamlaka ya kuwapatia dhamana

“Mheshimiwa hakimu  sisi upande wa Jamhuri tunawasii mawakili wa washitakiwa wawe watulivu na wavumilivu kwani kesi hii ndiyo kwanza imefunguliwa leo, na upelelezi bado haujakamilika na sheria zilizotungwa na bunge zipo wazi kabisa zinasema ni Mahakama Kuu peke yake ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hii na si mahakama hii hivyo tunasisitiza kuwa mahakama hii haina mamlaka ya kutoa dhamana,” alidai wakili Kongora.

Itakumbukwa kuwa Machi 29 mwaka huu, ghorofa mmoja lililokuwa linajengwa katika mtaa wa Indira Gandhi lilianguka na kusababisha watu  idadi hiyo ya watu 36 kupoteza maisha.

No comments: