Tuesday, May 14, 2013

IKULU YAMJIBU DR. SLAA KUHUSU KASHFA YA UDINI WA RAISI KIKWETE ALIZOZITOA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Wilbroad Slaa, leo, Jumatatu, Mei 13, 2013, amekaririwa na gazeti moja akidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na timu yake ya kampeni, “ilikuwa ikisaka kura kwenye nyumba za ibada na kumwaga sumu mbaya ya udini ambayo sasa inaitesa Serikali nataifa” kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Aidha, katika habari hiyo iliyoandikwa chini ya kichwa cha habari, “Dk. Slaa amlipua JK” kwenye gazeti linalounga mkono CHADEMA la Tanzania Daima,Mheshimiwa Slaa anadai kuwa migogoro ya sasa ya kidini “inajengwa au kutengenezwa na Serikali iliyojikita kusambaza sumu ya udini katika misikiti wakati wa kampeni za Urais mwaka 2010”.

Kwa hakika, hakuna namna nyingine ama namna bora zaidi ya kuielezea kauli hii ya Mheshimiwa Slaa isipokuwa kwamba kauli hiyo ni riwaya nyingine isiyokuwa na mshiko. Ni uongo mtupu. Yake Mheshimiwa Slaa ni maneno yasiyokuwa na ukweli wowote.

Ni uzushi na santuri ambayo imezoeleka sasa kwa wananchi. Kauli ya Mheshimiwa Slaa ni mwendelezo wa mtiririko usiokuwa na mwisho wa ghiriba ambazo kamwe hazitafanikiwa za Mheshimiwa Slaa kuwahadaa wananchi ukweli wa mambo ulivyo katika nchi yetu.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete na timu yake ya kampeni kamwe hawakufanya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, ama wa mwaka mwingine wowote, katika nyumba yoyote ya ibada iwe msikitini ama kanisani ama hekaluni ama nyumba nyingine yoyote ya ibada mahali popote katika nchi yetu.

Mheshimiwa Rais Kikwete hajawahi hata kufikiria kuchanganya dini na siasa. Hana sababu ya kufanya hivyo. Anaelewa fika madhara ya udini kwa mustakabali wa nchi yetu, kwa umoja wa taifa letu na kwa mshikamno wa wananchi wake.

 Yoyote anayejaribu kumbebesha Rais Kikwete msalaba wa udini ana lake jambo na ni vyema atuambie fika Rais alitumia Msikiti upi, ama Kanisa lipi, mahali gani na kwa nyakati gani kufanya kampeni.

Vinginevyo, kauli ya Mheshimiwa Slaa itabakia ni kauli tu inayostahili kupuuzwa na wananchi, itabakia ni kauli ya mtu mzima anayetapatapa na kufanya jitihada kubwa kujivunjia mwenye heshima kwa kutunga na kusambaza uongo.

Tunanapenda kumshauri Mheshimiwa Slaa kuwa kama  hana jambo la maana lakuwaambia wananchi ama ameishiwa na hoja ni vyema  anyamaze, awaachie wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo, kuliko kuendeleza riwaya zake zisizokuwa na mshiko.Yake ni santuri iliyowachosha wananchi.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Raisi Ikulu.
Dar es Salaam.
13 Mei, 2013

No comments: