Monday, June 17, 2013

DR. MARY NAGU ANUSURIKA KUCHOMWA MOTO NA WAFUASI WA CHADEMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu pamoja na Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni (CCM), wamenusurika kuchomwa moto na wafuasi wa Chadema usiku wa kuamkia jana.

Tukio hilo lilitokea usiku wa manane, baada ya wafuasi wa Chadema, wakiongozwa na Mbunge wa chama hicho Jimbo la Karatu, Mchungaji Israel Natse, kuvamia nyumba waliyokuwa wamefikia Nagu na Soni, katika Kata ya Bashnet, Babati Vijijini, mkoani Manyara.

Wafuasi hao wa Chadema wanawatuhumu Dk. Nagu na Soni kukutana katika nyumba hiyo kwa nia ya kupanga mipango ya kutoa rushwa ili kufanikisha uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata hiyo, unaotarajiwa kufanyika leo, ikiwa ni pamoja na maeneo mbalimbali nchini.

Chanzo cha MTANZANIA Jumapili kilichokuwa eneo la tukio kililidokeza gazeti hili kuwa Dk. Nagu na Soni

walikwenda kijijini hapo usiku, wakiwa na magari mawili, kila mmoja na lake na kufika nyumbani kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Petro Baha, kwa kile kilichodaiwa kuwa ulikuwa ni mpango wa kupita na kugawa fedha kwa wananchi usiku huo, ambapo pia inadaiwa ndani ya nyumba hiyo alikuwepo mgombea udiwani wa Kata hiyo, Nicodemus Gwandu (CCM).

Kitendo cha Nagu pamoja na Soni kuonekana katika nyumba hiyo kiliwashitua wafuasi wa Chadema, ambao baada ya muda mfupi walivamia nyumba hiyo wakiwa na Mbunge wao, Natse, madiwani na msafara wa pikipiki na kutishia kuichoma moto.

Mtoa habari wetu huyo alisema kuwa, wafuasi hao wa Chadema waliweka kambi katika nyumba hiyo kuhakikisha Nagu na Soni hawatoki kwenda kwa wananchi usiku huo.

Chanzo chetu kilisema kitendo cha kuzingirwa huku wakitishia nyumba kuchomwa moto kiliwashitua viongozi hao wa CCM na kuamua kupiga simu polisi, ambao walifika wakiwa sita muda mfupi baadaye kwa ajili ya kuimarisha ulinzi hadi walipotoka jana asubuhi.

Inaelezwa kuwa mgombea wa udiwani wa CCM, Nicodemus, ambaye naye alikuwemo ndani ya nyumba hiyo pamoja na akina Nagu, yeye alifanikiwa kutoroka mapema kwa kuruka ukuta na kukimbia.

Alipotafutwa Dk Nagu ili kupata ukweli kuhusu taarifa hizo, simu yake ya kiganjani iliita bila mafanikio na hata alipotumiwa ujumbe mfupi nao hakujibu.

Kwa upande Soni, alikiri kuzingirwa na wafuasi hao wa Chadema, lakini alikanusha madai ya mkakati wa kutoa rushwa.

“Ni wanachama wa Chadema wakiongozwa na Mbunge wa Karatu, Mchungaji Natse na madiwani karibia wa kata sita pamoja na msururu wa pikipiki, sisi tulikuja kulala, mimi siku zote huwa nalala kijijini, sasa walikuja wakaanza kupiga yowe, ndipo wananchi wakatoka. Tulikuwa wanne na magari mawili,” alisema Soni.

Akielezea sababu za kwenda kulala katika nyumba hiyo, Soni alisema walifikia hatua hiyo baada ya kuwapo kwa mpango wa Chadema kufanya fujo.

Alisema dalili hizo zilianza kuonekana mapema baada ya Dk. Nagu kuwekewa mawe kwenye daraja la Kambesh, kitendo ambacho kilimfanya ashindwe kuondoka na kwenda kulala alipoandaliwa Soni.

Akifafanua tuhuma kuwa walikwenda kwa ajili ya kutoa rushwa, Soni alisema kama wafuasi hao wana uhakika wathibitishe madai yao.

“Waje wathibitishe rushwa gani ya kuwapatia watu wanne, maana ndio waliokuwemo katika nyumba hiyo, hata mgombea wanayedai alikuwepo alikuja hapo mara baada ya kusikia yowe, wananchi wamesaidia kuwatawanya,” alisema Soni.

Mbunge wa Chadema, Natse alikiri kuwepo katika eneo hilo, baada ya kupatiwa taarifa kwa njia ya simu na wananchi ambao walimweleza juu ya kuwako kwa mpango wa kutoa rushwa uliokuwa ukiandaliwa na Nagu pamoja na Soni.

“Kilichotokea saa 7 usiku tulipigiwa simu na wananchi kuwa Waziri Nagu na Soni walikuwa eneo la Bashnet, ambalo ndiyo ngome yao ya rushwa na walikwenda kugawa huko, lakini walipoonekana tu yowe lilipigwa na watu walikusanyika wakitoka na silaha, ikiwemo mapanga na mikuki,” alisema.

Natse alisema kuwa baada ya taarifa hizo walikwenda eneo la tukio ili kuepusha madhara zaidi, kutokana na wananchi hao kudhamiria kuchoma moto nyumba walimokuwamo vigogo hao wa CCM.

“Tulipofika tuliwatuliza wananchi, lakini waligoma kuondoka, lakini wao (kina Nagu) walikuwa wameshapiga simu polisi. Askari walipofika eneo la tukio tuliwataka wawatoe nje wahusika, lakini walitusihi tukubali wawalinde mpaka asubuhi asitoke mtu, suala ambalo wananchi waliliafiki, huku wao wenyewe wakiendelea kuwepo eneo la tukio kuhakikisha kuwa hawatoki kwenda kugawa rushwa mpaka majira ya saa 11 nilipoondoka hapo,” alisema Natse.

Uchaguzi huo unaofanyika leo katika kata ya Bashnet, unawashirikisha wagombea watatu ambao ni Nicodemus Gwandu wa CCM, Alois Gwandu wa NCCR Mageuzi na Laurent Tara wa CHADEMA, ambaye kabla ya kuhamia chama hicho alikuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya NCCR Mageuz

No comments: