Wednesday, June 19, 2013

NAPE , GODBLESS LEMA NA MBOWE WATAKIWA KUPELEKA ASHAHIDI WAO POLISI, VINGINEVYO SHERIA ITACHUKUA MKONDO WAKE

Jeshi la Polisi limetishia kuwakamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na limesema litamhoji Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye baada ya wanasiasa hao kudai kufahamu watu waliohusika na tukio la kurushwa bomu mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja aliwataka wanasiasa hao kuwasilisha ushahidi wa kile wanachofahamu kuhusu kulipuliwa kwa bomu hilo.

Juzi, Mbowe akiwa na Lema, alisema wana ushahidi wa picha za video zikiwahusisha polisi na kulipuliwa kwa bomu hilo katika Uwanja wa Soweto wakati wa mkutano wa kuhitimisha kampeni za udiwani kwa Chadema, Jumamosi iliyopita.

Mkwara wa Chagonja
Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kupeleka ushahidi ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.

“Tunamtaka Mbowe na Lema kutoa ushahidi wa askari wetu kuhusika na tukio la bomu pale Soweto. Wasipofanya hivyo tutatumia sheria kuwalazimisha kufanya hivyo kwani yeyote mwenye ushahidi unaoweza kusaidia upelelezi wa kosa la jinai akikataa kuuwasilisha kwa vyombo husika anaweza kuchukuliwa hatua,” alisema.

Nape naye kuhojiwa
Kwa upande wake, polisi limesema litamhoji Nape ambaye alikaririwa jana akidai kuwa Chadema ndiyo waliohusika na urushaji wa bomu kwenye mkutano wao baada ya kuhisi kushindwa kwenye uchaguzi wa kata nne za Jiji la Arusha.

Kamishna Chagonja alisema watamhoji ili kusaidia kazi yao ya upelelezi. Nape aliihusisha Chadema kwa kauli alizoita za kutishia amani zilizowahi kutolewa siku za nyuma kabla ya uchaguzi wa kata za Arusha.

Watatu wakamatwa
Kamishna Chagonja alisema watu watatu wamekamatwa wakihusishwa na tukio la kulipuliwa kwa bomu mkoani Arusha.

Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa na polisi na watafikishwa mahakamani muda wowote ushahidi wa kutosha utakapopatikana au kuachiwa huru wakigundulika kutokuhusika.

Kamishna Chagonja alikataa kutaja majina ya watuhumiwa akidai kwa kufanya hivyo kunaweza kuharibu upelelezi.
Polisi wajitetea kurusha risasi

Akizungumzia madai ya polisi kutumia risasi za moto katika tukio hilo, Kamishna Chagonja alisema walilazimika kupiga mabomu na kurusha risasi hizo ili kuwadhibiti wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiwazuia kumkamata mtuhumiwa.

Hata hivyo, Mtoto Abubakar Adam, mwenye umri wa miaka kumi na moja, ambaye ni mmoja wa majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Selian alikaririwa  jana akiwatuhumu polisi kumpiga risasi.

Kamishna Chagonja alisema: “Baada ya bomu kurushwa na kulipuka, polisi walianza kukimbilia eneo la tukio lakini vijana wa Chadema wakaanza kuwashambulia polisi ambao walilazimika kujihami.”

Tendwa awaonya Mbowe na Nape
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa amewataka viongozi wa Chadema na CCM kuwasilisha ushahidi wa taarifa zao za madai ya kuwafahamu watu waliohusika na tukio hilo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kauli ya Tendwa imekuja baada ya Nape kudai kumkariri Lema akisema kuwa uchaguzi hauwezi kufanyika, huku Mbowe akidai kuwa wana ushahidi wa CD ambao umemwonyesha askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuhusika na tukio la urushaji wa bomu kwenye mkutano huo wa chama chake na kusababisha watu watatu kufariki dunia na wengine kujeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Tendwa alisema kauli za viongozi hao zinawachanganya wananchi.

Alisema kitendo cha kunyoosheana vidole bila ya kutoa ushahidi ni kutafuta umaarufu usio na faida, jambo ambalo linaweza kuongeza chuki na hasira.

Mwananchi

No comments: