Saturday, June 16, 2012

SHULE YA SEKONDARI NAURA YADORORA KIELIMU MKOANI ARUSHA.


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Naura, Ndugu Sunday G. Mshobozi ambaye pia ndiye mwalimu pekee wa somo la Fizikia kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari ya Naura, Ndugu Mary Shirima akifanya mahojiano na mwandishi kufahamu changamoto zinazoikabili shule hiyo
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo wakiwa katika muda wa mapumziko

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la HakiElimu umegundua kuwa Shule ya Sekondari ya Naura iliyoko katika kata ya Lemara , eneo la Njiro ni miongoni mwa shule zenye maendeleo hafifu ya kielimu ukilinganisha na shule nyingine za serikali na kata zilizoko katika Manispaa ya Wilaya ya Arusha. 

Shule hii iliyoanzishwa mwaka 2008 , inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu kwani kuna masomo hayajawahi kuwa na walimu toka shule hiyo ianzishwe  mfano masomo ya Chemistry, Mathematics na  Book- Keeping . Pia kuna masomo ambayo yana mwalimu mmoja mmoja mfano English, Commerce,  Literature, na Civics toka kidato cha kwanza mpaka cha nne. 

Tofauti na shule nyingine ambazo hukimbiwa na walimu kutokana na kuwa mazingira magumu shule hii iko eneo zuri na maarufu waishio watu wenye kipato cha juu mkoani Arusha lijulikanalo kama Njiro na kuacha maswali kuwa kama kuna tatizo la uongozi wa shule au kuna tatizo la upangaji wa walimu unaofanywa na serikali , hili hali shule nyingine zikiwa na walimu lukuki. 

Akielezea sababu nyingine za kudorora kitaaluma shuleni hapa Mwalimu Mshobozi alisema kuna mrundikano mkubwa wa wanafunzi kushinda uwezo wa shule akitolea mfano wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza  kwa mwaka huu kufikia 307. Tofauti na malengo ya shule ya kata kusomesha wanafunzi wa maeneo ya karibu ,  wanafunzi wa shule hii wanatoka katika kata zote zilizoko manispaa hii kukiwa na umbali mrefu na kukabiliwa na shida kubwa ya usafiri jambo ambalo pia alilielezea  kuwa ni moja ya sababu za kudorora kitaaluma kwa wanafunzi wa shuleni hapo. 

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi Bi Mary Shirima alisema sababu za kudodora kitaaluma kwa shule yake ni mwako mdogo wa kielimu kwa wazazi pamoja na watoto wenyewe akisema wengi wa wanafunzi ni kama wamelazimishwa kuja kusoma shuleni hapo na wazazi wao hawajishughulishi na maendeleo ya watoto wao.  “ Historia ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne ni tata kwani kuna waliokuwa wameolewa na wafanyabiashara mara baada ya kumaliza darasa la saba ,ghafla wakasikia wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na kulazimika kuja shuleni, sasa katika hali hiyo unatarajia nini” aliuliza Mwalimu Shirima.

Katika mtihani wa kidato cha nne wa taifa wa mwaka jana 2011 jumla ya wanafunzi 164 walifanya mtihani  huo ambapo hakuna aliyepata daraja la kwanza wala la pili, wanafunzi 2 walipata daraja la tatu , 24 wakapata daraja la nne na 138 walifeli kwa kupata zero. Shule hii ilishika nafasi ya mwisho kati ya shule 137 zilizofanya mtihani huo katika mkoa wa Arusha. Kitaifa ilishika nafasi ya 2994 kati ya 3108 zilizofanya mtihani huo.

HakiElimu inatoa wito kwa Serikali kupitia mamlaka husika kuangalia upangaji wa walimu na uchaguzi wa wanafunzi shuleni hapo. Wazazi na wakazi wa Njiro nao wanatikiwa kuchukua jitihada za ziada kuhakikisha wanafunzi walioko shuleni hapa wanapata elimu bora na kuelimika .Uongozi wa shule nao ni siri ya mafanikio au kushindwa kufanya vema , hivyo uongozi wa Shule ya Sekondari Naura uongeze jitihada kuhakikisha shule hii inafanya vema kama shule za Kaloleni, Ngarenaro na Arusha Day . 

No comments: