Monday, July 9, 2012

Mgomo Wa Madaktari: Hakuna Cha kujadili. Asiyeweza Aache Kazi. Umeisha. - IKULU.

Ikulu imesema kwamba mgomo wa Madaktari umeisha na walioamua kuendelea na kazi ya kutibu binadamu, wamerejea kazini.


Aidha, imesema kwamba sasa siyo wakati wa kulumbana tena, bali ni wakati wa kusonga mbele badala ya kurudi nyuma kwa sababu hakuna mgomo tena wa kujadiliwa.

Taarifa ya maandishi ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilieleza hayo jana baada ya kutakiwa kutoa kauli kuhusu ombi la baadhi ya viongozi wa dini kutaka Rais Kikwete akutane nao, wanaharakati na madaktari kujadili mgomo wa Madaktari.

Juzi, baadhi ya viongozi wa dini nchini waliingilia kati mgomo huo wa madaktari wakimwomba Rais Kikwete aitishe kikao nao ili kufanya mazungumzo yatakayowashirikisha madaktari na wanaharakati kwa lengo la kuondoa tatizo hilo.

Aidha, wametaka wanaharakati na wanasiasa waache kushabikia na kuchochea mgomo na badala yake washiriki kutafuta suluhu ya kweli kwa faida ya Watanzania wote.

Mambo ya msingi

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu kujibu swali aliloulizwa  kuhusu ombi hilo la viongozi wa dini, alisema mambo ya msingi kwa sasa ni manne.

“Kwamba mgomo wa madaktari umeisha na walioamua kuendelea na kazi hii muhimu sana ya kutibu binadamu wamerudi kazini. Hili ni jambo jema sana. Sasa siyo wakati wa kulumbana tena bali ni wakati wa kusonga mbele badala ya kurudi nyuma kwa sababu hakuna mgomo tena wa kujadiliwa.

“Kwamba tokea madaktari walipoanza kudai maslahi zaidi, Serikali ilifanya jitihada kubwa za kukutana na madaktari hao.

Mbali na Kamati ya Majadiliano ya Serikali, Madaktari pia wamekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda. Kamwe, Serikali haijapata kukataa kukutana na viongozi wa madaktari,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Alieleza kuwa mara ya mwisho madaktari hao walipoitwa kukutana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi walikataa wakidai kuwa Waziri hakuwa na jambo jipya la kuwaambia.

“Huu ni ushahidi mwingine kuwa kamwe Serikali haijapata kukataa kukutana na kuzungumza na madaktari,” alieleza.

“Kwamba mara zote walipoomba kukutana na viongozi wa Serikali, akiwemo Rais, hawakupitia kwa mtu yeyote isipokuwa waliomba moja kwa moja na wakakubaliwa. Hivyo, hawana sababu ya kupitia kwa watu wengine kuomba kukutana na viongozi wa Serikali,” Mkurugenzi huyo aliutaja msingi mwingine.

Moja ya hoja za madaktari hao waliogoma ni kutaka kulipwa mshahara zaidi na Serikali na katika mapendekezo yao walitaka kulipwa Sh. milioni 3.5 kwa mwezi kwa daktari anayeanza kazi; kiwango ambacho ukijumuisha na madai mengine ya posho kinafikia Sh. milioni 7.7.

Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho ya mwezi Juni, aliwaeleza madaktari hao kwamba Serikali haina uwezo wa kulipa kiwango hicho, na kwamba wako huru kutafuta mwajiri mwingine anayeweza kuwalipa, na hivyo hawana sababu ya kugoma.

“Kama daktari anaona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo (Sh. milioni 7.7) awe huru kuacha kazi na kwenda kwa mwajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho,” alisema Rais Kikwete.

Kutokana na ukweli huo, aliwatakia kila la heri wasioweza kufanya kazi serikalini, lakini akaongeza kuwa “hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo.” “Isitoshe, hana sababu ya kuendelea kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka. Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24?,” alihoji.

Rais Kikwete pia aliwaonya Madaktari hao kwa kuingia katika mgogoro na Mahakama ambayo iliwapa amri kurudi kazini wakaikataa na mgogoro mwingine na waajiri wao isivyostahili.

No comments: