Sunday, December 9, 2012

Zaidi Ya Nyumba 50 Zaezuliwa Na Kimbunga

   Paa la nyumba lililoezuliwa
 Nguzo za umeme zilizoanguka
 Mkuu wa Wilaya ya Iringa Letisia Warioba akikabidhi mifuko ya unga wa ugali, kama ni moja ya msaada kwa waathirika wa mvua hizo.
Meneja wa Tanesco moa wa Iringa Donart Makingi akipita kati ya nguzo zilizodondoshwa na mvua za upepo, katika eneo la Migori.

MVUA kubwa zilizoambatana na upepo mkali, zimevunja nyumba zaidi ya 50 na kuezua paa katika Kata ya Migoli na Nyang’olo, katika Tarafa ya Isimani Wilaya ya Iringa, na kusababisha hasara kubwa kwa wananchi.

Wakizungumzia tukio hilo, wananchi walisema mvua hiyo ilianza kunyesha majira ya saa kumi jioni, ambapo baadhi yao walikuwa katika mkutano wa mkuu wa mkoa, ambapo mvua hiyo pia ilisambaratisha mkutano huo.

Maneno Kalinga mkazi wa Nyang’olo alisema mvua hizo ziliambatana na upepo mkali na hivyo kuezua paa la nyumba yake yote, na kudondosha kuta mbili za nyumba yake, huku watoto waliokuwemo ndani ya nyumba wakipata madhara.

Kalinga alisema kijana wake aitwaye Fadhili kalinga aliyekuwa amelala nadani ya nyumba hiyo, aliangukiwa na ukuta na kuumizwa maeneo ya mgongo na kumsaidia kumuondoa katika kifusi na kumuwahisha katika Zahanati ya Nyang’olo.

“Baada ya kupiga kelele majira walikuja kumusaidia kijana wangu, na walipofanikiwa kumtoa katika kifusi, tulimpeleka Zahanati kwa ajili ya kupata matibabu, na hasara nyingine nilizozipata ni kubwa kwani vitu vyote vimelowa na kuharibika, “ Alisema Kalinga.

Estwina Ngobola mkazi wa Migori alisema mali zake ziliharibiwa ikiwemo mifuko ya Sukari kilo 25, unga wa ugali, unga wa ngano, godolo, huku vitanda na kochi vikivunjika baada ya kuangukiwa na tofali

Alisema “Niliingia chumbani ili nifunge dirisha upepo usiingie, kwani mvua ilikuwa na upepo, nikawa ninahofu mji yataingilia dirishani, lakini nilipotaka kufunga dirisha ulikuja upepo mkali nikaona nyumba inatikisika, nikakimbilia nje na baadaye paa lote likatolewa na kutupwa pale, kuta zikadondoka, kama unavyoona hivi,” Alisema Estwina.

Estwina alisema kutokana na hali hiyo ameomba majirani wamuhifadhie vitu vyake, huku yeye akiwa anaishi katika nyumba ya wageni, licha ya kutokuwa na fedha ya kulipa kwani hana ndugu katika mkoa wa Iringa, kwani yeye ni mwenyeji wa Mbeya.

Lucia Magidanga (98) mkazi wa Migori alisema hana mahala pa kuishi baada ya nyumba yake kuezuliwa, huku akiwa hana msaada wowote wa kufanya ukatrabati wa nyumba yake, kutokana na watoto wake wote kufariki.

Naye Mwajuma Nzalamalenga alisema hasara aliyoipata kutokana na janga hilo ni kubwa kwani mali zake zote zimeharibiwa vibaya, yakiwemo Magodoro, unga, Sukari, Maharage, na nyumba ya mma yake ikiwa imeezuliwa yote.
Mwajuama alisema hana mahala pa kuishi yeye na afamilia yake, na hata mvua ikianza tena kunyesha haelewi hali halisi itakuwaje.

Aidha mvua hizo pia zimeangusha nguzo 19 za Tanesco na hivyo eneo hilo kukosa nishati ya umeme, ambapo meneja wa Tanesco mkoa wa Iringa Injinia Donart Makingi alisema eneo hilo halina umeme kutokana na kuanguka kwa nguzo hizo.

Injinia Makingi alisema tayari wanapeleka nguzo za umeme ili kurejesha nishati hiyo na kuwa bado hajapata thamani halisi ya hasara itokanayo na janga hilo la mvua zilizoambatana na upepo mkali.

Hatua hiyo iliulazimu uongozi wa Mkoa kufika katika eneo la tukio kufanya tathimini ya uharibifu uliotokea, huku waathjirika wakipatiwa baadhi ya misaada ya chakula ili kuwasaidia wananchi hao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Pudensiana Kisaka alisema wanafanya tathmini ili kutambua kiwango cha hasara kilichopatikana kwa lengo la kuwasaidia wananchi hao, huku akikabidhi Unga kilo 750 na Maharage kilo 300 kwa waathirika.

Kisaka aliwata wananchi hao kupanda miti kwa kiasi kikubwa msimu huu wa mvua ili kuepukana na upepo mkali unaosababisha madhara makubwa kama ya kuezuliwa nyumba zao na kupata hasara.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Letisia Warioba alisema mkoa kupitia mfuko wa maafa imeunda kamati ya muda ya kutathimini madhara hayo ili kuweza kuwafidia wananchi waliokumbwa na janga

 NA: OLIVER RICHARD - IRINGA

No comments: