Tuesday, July 3, 2012

Mwanamke azikwa akiwa hai Mbeya


                   Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Malamba, Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

KUMEZUKA vitendo vya unyama mkoani Mbeya vya kuzika watu wanaotuhumiwa kuwa ni washirikina wakiwa hai ambapo hivi karibuni watu wawili akiwemo mwanamke mmoja wamefanyiwa unyama huo.
Mwanamke aliyezikwa akiwa hai kwa tuhuma za kujihusisha na ushirikina ni Rozina Mwadala (60) ambapo tukio hilo lilitokea Juni 2, mwaka huu.

Mwanamke huyo alichukuliwa hatua hiyo baada ya kifo cha mmoja wa ndugu yake ambaye alifariki muda mchache baada ya kulalamika kuwa alikuwa akiumwa sikio na kichwa. Hata hivyo, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa tayari kuhojiwa na mwandishi wetu kwa hofu ya kukamatwa na polisi.

Kufuatia vitendo hivyo kushika kasi mkoani Mbeya, Mwenyekiti wa Muungano wa Jamii Tanzania (Mujata), Chifu Soja Masoko, amewaonya wananchi wa Kijiji cha Malamba, Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kuacha mara moja tabia za kujichukulia sheria mikononi alipokuwa akiwahutubia katika mkutano wa hadhara Juni 15, mwaka huu.

“Hasara yake mnaona. Sasa kufuatia kitendo hicho cha kikatili baadhi ya wananchi wamehama kijijini hapa kukwepa mkono wa sheria na shughuli za kiuchumi zimezorota,” alisema.

Mbali na mwanamke huyo kuzikwa hai, hivi karibuni mwanaume mmoja, Nyerere Kombwee naye alizikwa hai baada ya kutokea kifo cha mdogo wake kisha yeye kutohudhuria msibani ndipo wananchi wakamsaka na walipompata wakampiga na yeye akatoa vitisho kuwa damu yake isingeweza kwenda bure ndipo wakaamua kumzika akiwa hai.

No comments: