Tuesday, January 1, 2013

IPO HAJA YA MFUMO WA UONGOZI KUTUNGIWA SHERIA KATIKA KATIBA MPYA

                                    Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe.

HAKIKA Mungu ni mwema kwani ametufanya tukutane tena leo katika safu hii lakini pia tumshukuru kwa kuweza kutuwezesha kuuona mwaka 2013.
Baada ya kusema hayo nizungumzie kwa ufupi kuhusu  ushauri uliowahi kutolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiishauri serikali kuandaa mfumo na utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaoiwezesha nchi kuepuka machafuko na vurugu iwapo chama chochote hasa cha upinzani kitachaguliwa na wananchi kuongoza nchi baada ya  kile kinachotawala kuondolewa madarakani.

Ushauri huo wa Chadema ulitolewa na Mbowe alipokuwa akihutubia mikutano ya wilayani Mbozi, mkoani Mbeya mwishoni mwa mwaka jana.
Alisema kutokana na vuguvugu la siasa za mabadiliko zinazoendelea hapa nchini, ni fursa nzuri na wakati muafaka nchi yetu ikawa na mfumo mzuri wa kikatiba na kisheria kwa ajili ya kusimamia mabadiliko ya uongozi ili yafanyike kwa amani, hivyo kuepusha nchi kuingia katika vurugu na mikanganyiko ya kisiasa.

Kiongozi huyo wa chama hicho alisema, ingawa hiyo inaweza kuonekana kuwa ni dhana mpya, ni vyema Watanzania wakaanza kuitafakari kutokana na umuhimu wake katika mustakabali wa nchi yetu.
Binafsi wazo hilo la Mbowe linafaa kupongezwa bila kujali ni lini chama tofauti na chama tawala kinaweza kupata ushindi katika kuongoza nchi. Nasema tamko hilo linaonekana dhahiri kwa mtu yeyote mwenye mapenzi mema na nchi yetu kwamba limeweka mbele maslahi ya taifa na wananchi wote kuliko kitu kingine chochote.

Hadhari anayotoa kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini ni kuwa, ni hatari kubwa kwa nchi kama yetu ambayo sasa inapitia kwenye mawimbi ya mabadiliko kutokuwa na mfumo huo ambao huhakikisha mabadiliko ya mpito kutoka serikali moja kwenda nyingine yanafanyika kwa amani na maslahi ya nchi yanalindwa bila kutetereka.

Zanzibar wameanza, wao wameamua katika katiba yao kushirikisha chama cha pili kwa ushindi katika uchaguzi kuunda serikali. Hakika uamuzi ule ni mzuri sana na tumeona jinsi ambavyo umeepusha vurugu za kisiasa kwa sababu haiwezekani chama ambacho kimechaguliwa na wengi na kutofautiana kwa kura chache na kilichoshinda kukiacha bila kukishirikisha katika serikali.

Lakini ipo mifano hai ya jambo hili kwa  mfano nchi ya  Ghana iliyopitia misukosuko kutoka katika utawala wa Rais Jerry Rawlings kwenda kwa chama cha upinzani cha Rais John Kufour kilichoshinda uchaguzi mkuu nchini humo na kuunda serikali, walipata fundisho kiasi kwamba baada ya Rais Kufour kuingia madarakani serikali yake ilitunga sheria ya ‘kipindi cha mpito’ kutoka serikali moja kwenda nyingine.
Ukiangalia mfumo wa Marekani kwa mfano,  inachukua takribani miezi miwili na nusu kwa rais mpya kuapishwa na kukabidhiwa rasmi madaraka ya kuongoza nchi tangu achaguliwe. Hii ni kwa sababu kuna mambo muhimu sana ya kufanyiwa kazi kabla utawala mpya haujakabidhiwa Ikulu.

Tofauti sana na nchi za Kiafrika kwa mfano hapa nchini inachukua saa 48 pekee kwa uongozi mpya kukabidhiwa madaraka baada ya kiongozi wa nchi kuchaguliwa, hivyo ni wazi hali hiyo ni hatari kwa sababu kuna mambo ya msingi ambayo yanahitaji muda wa kutosha katika kufanya makabidhiano.
Nakubaliana na wazo la Mbowe kwa asilimia 100 anapotoa mfano wa wizi wa mabilioni ya fedha za ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) hapa nchini mwaka 2010 kwamba fedha hizo zilikwapuliwa na mafisadi kirahisi kutokana na kutokuwepo  mfumo na sheria za kusimamia kipindi cha mpito. Hali hiyo ni mbaya na nchi yetu haiwezi kuvumilia tena kuona ikijirudia.
Nakubaliana pia na Mbowe anaposema sasa ni wakati muafaka kwa nchi yetu kuanza kufikiria kuwa na mfumo wa kikatiba na kisheria kuhusu kipindi cha mpito kutoka serikali moja kwenda nyingine kwani usipokuwepo, wakati wa makabidhiano ya madaraka unajitokeza wasiwasi mkubwa ambao hakika unaibua maswali mengi.

Maswali ya msingi ni nani anasimamia kikamilifu rasilimali za umma wakati huo? Nini hatima ya watumishi wa umma, majeshi yetu na nyaraka za siri za serikali, ulinzi na usalama wa nchi yetu? Haiwezekani serikali mpya iingie madarakani kienyeji bila kuwepo muda muafaka wa makabidhiano.
Hiyo ni changamoto kubwa kwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na pengine kwa Tume ya Marekebisho ya Katiba inayoendelea na kazi yake hivi sasa chini ya uongozi wa Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.

Watanzania wote tusiangalie ushauri huu kupitia mboni za kiitikadi, isipokuwa upokelewe na kufanyiwa kazi kwa kuzingatia maslahi ya nchi yetu na watu wake. Ndiyo maana nasema wazi kwamba katiba mpya ni lazima iyazingatie haya.

No comments: