Monday, February 25, 2013

WAKUU WA SHULE WADAI KUWA MITIHANI YA KIDATO CHA NNE ILITUNGWA KWA MFUMO TOFAUTI....

  MATOKEO mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yamezidi kuibua mapya, baada ya wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini kusema mitihani ilitungwa kwa mfumo tofauti na uliozoeleka miaka yote, huku tume iliyounndwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ikipondwa na baadhi ya watu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema kwamba maswali waliyoulizwa watahiniwa yalikuwa ya kujieleza tofauti na miaka ya nyuma, ambapo mfumo uliotumika uliwataka watahiniwa kutaja vitu tu bila ya kulazimika kuvielezea kwa undani.

Kauli yake iliungwa mkono na Mkuu wa Taaluma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian, Florence Mapunda ambaye alisema kuwa mtihani wa mwaka jana ulitaka zaidi watoto kujieleza tofauti na miaka ya nyuma wakati wanafunzi walipokuwa wanakariri.

Hata hivyo, Msemaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), John Nchimbi alisema mfumo wa mtihani haukubadilika kwa namna yoyote na kuwa upo kama ule wa miaka yote.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, kwa upande wake alisema madai yanayotolewa hayana msingi, huku akihoji kwa nini yasitoke tangu mitihani ilipokuwa ikifanyika na badala yake yanatoka baada ya kutangazwa kwa matokeo.

Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.

Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu Pinda, juzi alitangaza kuunda tume ya kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya, hatua ambayo hata hivyo imekosolewa na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Tume hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka Taasisi za Elimu, Chama cha Waalimu, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa) inatarajiwa kuanza kazi wiki hii.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuunda tume ni kupoteza muda kwa sababu matatizo na changamoto zote ndani ya sekta hiyo yanajulikana, huku mwenzake, Profesa Chriss Maina pia wa UDSM akisema kuunda tume hakutaisaidia kwa kuwa Serikali inaidharau sekta ya elimu.

“Tatizo ni kutowekeza kikamilifu katika sekta ya elimu, imekuwa na matumizi makubwa katika mambo yasiyokuwa ya lazima,”alisema Profesa Mpangala.

Alisema matatizo mengine ni mazingira magumu ya kufundisha na uhaba wa walimu. “Kinachotakiwa wajipange kufanyia kazi changamoto hizi zilizopo badala ya kuunda tume, wakati fedha nyingi tunasikia inapotea kwenye ubadhirifu,”alisema Profesa Mpangala.

Naye Profesa Maina alisema: “Hiyo tume ya kazi gani kwa sababu matatizo yanafahamika wazi, umewahi kusikia taifa gani ambalo halina mtalaa wa elimu. Hiyo ndiyo hali halisi kwa nchi yetu. ”


No comments: