Thursday, May 2, 2013

CCM WAMVAA MKUU WA MKOA WA ARUSHA.....WANADAI AMEMUONGEZEA UMAARUFU GODBLESS LEMA

 VIGOGO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwemo wabunge, wamemjia juu Mkuu wa Mkoa (RC) wa Arusha, Magessa Mulongo kwa jinsi alivyoshughulikia kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA).

Wabunge hao waliliambia gazeti hili mjini Dodoma kuwa kesi ya uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya Lema kwa shinikizo la mkuu huyo, itaiathiri kwa kiasi kikubwa CCM.

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alisema kuwa amefuatilia kwa makini chanzo cha kesi ya Lema na hatimaye kukamatwa na polisi mithili ya gaidi, na kubaini kuwa hulka
za utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa serikali zinawapa sifa na umaarufu zaidi CHADEMA.

“Mimi sitaki kuingilia kesi, lakini ukiangalia kuanzia ile inayoitwa video ya vurugu za Chuo cha Uhasibu Arusha na jinsi Mkuu wa Mkoa alivyofika eneo la tukio na kuondoka, utabaini udhaifu mkubwa wa kiongozi huyo ambao leo unamfanya Lema aonekane shujaa.
“Leo tunaingia kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani pale Arusha, tunaweza tukashinda, lakini tutafanya kazi ya ziada kwa sababu tu ya udhaifu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,” alisema Lugola.

Mbunge mwingine ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema alichokifanya Mulongo ni sehemu ya tatizo kubwa la viongozi wa serikali kujihusisha na ukereketwa wa kisiasa.
“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa kuna kiongozi, tena hakumtaja jina, kwamba anapendwa kubebwa, alisema mwacheni abebwe. Alisema vile kuwazuia polisi kukabiliana na watu wanaopenda kumbeba kiongozi huyo.

“Mkuu wa Mkoa Arusha na wengine wanaokabiliana na wapinzani kwa nguvu kubwa bila sababu, hii inawaongezea umaarufu,” alisema mbunge huyo kutoka moja ya majimbo ya kanda ya kati.

Mjumbe mmoja wa Kamati Kuu (CC) ya CCM ambaye pia hakutaka kutaja jina lake, alilaani jinsi mkuu wa mkoa huyo alivyojikoroga katika kushughulikia mzozo wa Chuo cha Uhasibu Arusha.

“Niliposoma ujumbe wa simu ya mkononi wa Lema ambao alidai umetoka kwa Mkuu wa Mkoa, nilishangaa sana. Sijui kwanini amefanya vile,” alisema kigogo huyo.

Aprili 24 mwaka huu, Mulongo aliliamuru Jeshi la Polisi mkoani Arusha kumkamata Lema kwa madai kuwa aliwachochea wanafunzi wa chuo hicho cha IAA kumzomea na kumrushia mawe.
Lema alizingirwa nyumbani kwake na maofisa wa polisi kitengo cha upelelezi na wale wa doria Ijumaa saa 5.30 usiku kisha kuchukuliwa hadi Kituo Kikuu cha Polisi kuhojiwa na kuwekwa rumande siku tatu hadi Jumatatu wiki hii alipofikishwa mahakamani.

Hata hivyo, madai ya Mulongo kuwa Lema alichochea wanafuzni hao yanakinzana na ushahidi wa video unaoonesha kuwa mbunge huyo alitumia kila aina ya ushawishi kuwasihi wasiandamane kufuatia mwenzao Elly Kago (22) kuuawa na watu wasiojulikana jirani na chuo.
Mapema kabla ya kukamatwa, Lema aliitisha mkutano na waandishi wa habari akidai kutishiwa na Mulongo kupitia ujumbe wa maandishi wa simu.

“Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonyesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,’’ ulisomeka ujumbe huo uliotumwa kupitia simu namba 0752 960276 ambayo Lema alidai ni ya Mulungo.
Atisha waandishi

Wakati CCM wakiendelea kumlalamikia Mulongo kwa hatua zake dhidi ya Lema, kiongozi huyo jana aliwageukia waandishi wa habari wa Arusha akiwataka wawe makini kipindi hiki, akidai kuwa nao wanatumika na wanasiasa.

Akihutubia katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi, alisema kuwa ikibainika wanatumika nao watafikishwa katika vyombo vya sheria.

“Mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya Bagamoyo, hivi hivi wakawa hawanielewi na ikafika wakati wakanielewa kwani kuna miongoni mwao tulitaka kuwafikisha katika sheria, lakini tukayaacha kwa kuwa sisi ndio walezi,” alisema.
Mulongo aliongeza kuwa vitu ambavyo vinaandikwa si kweli kabisa, na kwamba wataendelea kufuatilia kwani baadhi ya waandishi wanashirikiana na wanasiasa kuwachafua viongozi wa serikali.
Alisema baadhi ya waandishi mkoani Arusha wamekuwa wakifanya kazi zao kwa ushabiki wa kisiasa na kuandika mambo ambayo hawana uhakika nayo.

“Unapoingia katika mkakati wa kudhalilisha kiongozi wa serikali unakuwa umeiweka roho yako rehani, kuweni makini,” alisema.

Aidha alivionya vyama vya wafanyakazi mkoani Arusha kutoruhusu kutumiwa na watu kwa malengo ya kisiasa na pia waajiri waache kufanya kazi bila kufuata taratibu na sheria.

No comments: