Friday, May 17, 2013

SERIKALI YAAHIDI KUWACHUKULIA HATUA KALI VIONGOZI WA WIZARA YA ELIMU WALIOSABABISHA UBOVU WA MATOKEO YA FORM FOUR

                                                                      Mizengo Pinda.
Serikali imeahidi kuwajibisha watendaji watakaobainika kwenda kinyume katika uingizaji wa mfumo mpya wa usahihishaji mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012, ambao matokeo yake yamefutwa.

Akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kinachosubiriwa sasa, ni maelezo ya kina ya Tume ya Taifa aliyoiunda kuchunguza matokeo hayo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Tume hiyo haijakamilisha kazi yake,  lakini muda si mrefu itakuwa imekamilisha na kuwasilisha maelezo ya kina yatakayoipa Serikali majibu kwa maeneo yote.

“Tusubiri kidogo, muda si mrefu tutakuwa tumekamilisha kazi …na kama wapo watu waliosababisha jambo hili, wala haitakuwa tatizo hata kidogo kuchukua hatua za kuwawajibisha. Ni dhahiri kwamba suala hili si dogo,” alisema Waziri Mkuu.

Majibu hayo ya Pinda yalitokana na maswali ya Mbunge Sakaya, ambaye alisema uamuzi wa Serikali wa kufuta matokeo hayo kutokana na kubainika kulikuwa na mabadiliko ya upangaji wa alama bila kuandaa wanafunzi, si jambo dogo.


Sakaya ambaye alitaka kusikia kauli ya Serikali, alihoji, “Hili si jambo dogo, ni kubwa sana. Elimu ni kitovu cha maendeleo ya taifa lolote, haiwezekani utaratibu mpya
ukaingizwa kwenye mfumo bila kushirikisha wadau wakiwemo maofisa elimu na walimu.

Akimjibu, Waziri Mkuu alisema Tume inaendelea kukamilisha kazi yake, ili kuja na maelezo fasaha juu ya nini kimetokea, na athari zilizojitokeza kutokana na hatua hiyo ya matokeo mabaya.


Hata hivyo Sakaya aliendelea kusema matokeo yameleta madhara makubwa kwa jamii, ikiwemo watoto waliopoteza maisha, wengine kukimbia familia zao na baadhi ya wazazi kufedheheka na kupata presha.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, huoni umuhimu wa kuwajibisha watendaji wote waliohusika wakianzia na Waziri mhusika wa wizara hii (Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa) ambaye aliruhusu mfumo huo?” Alihoji Sakaya.

Waziri Mkuu pamoja na kujibu kwamba haitakuwa tatizo kuchukua hatua za kuwawajibisha watendaji husika, alisisitiza baada ya kazi ya Tume, Serikali itapata maelezo ya kina na majibu kwa maeneo yote.

Mwezi uliopita, Serikali ilitoa taarifa bungeni juu ya uamuzi wa kufuta matokeo ya  mtihani wa kidato cha nne, uliofanyika mwaka jana na kutangazwa Februari mwaka huu.
Taarifa hiyo, ilitolewa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya kuchunguza matokeo hayo, iliyoundwa na Waziri Mkuu,  Pinda kutokana na matokeo kushuka kwa kiwango kikubwa.


Kwa mujibu wa Lukuvi, Baraza la Mawaziri liliridhia mapendekezo ya Tume hiyo na kutaka yatekelezwe mara moja. Ilielezwa mfumo uliotumika mwaka jana katika kupanga matokeo na madaraja, ulikuwa tofauti na  uliotumika mwaka juzi na miaka iliyotangulia.

Matokeo yaliyotangazwa Februari 2012 yalionesha kati ya wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, watahiniwa 126,847 ndio waliofaulu. Kati ya hao, waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ni 23,520 sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327 sawa na asilimia 28.1 huku watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 ya wanafunzi wote walipata sifuri.


Tume ya Uchunguzi inayotarajiwa kukamilisha maelezo yake hivi karibuni, ilipewa hadidu za rejea ambazo ni kubainisha sababu za matokeo hayo mabaya, kubaini sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.

Hadidu nyingine za rejea ni kutathmini nafasi ya halmashauri katika kusimamia elimu ya sekondari katika halmashauri zake na kuainisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali hiyo ya matokeo.

No comments: