Saturday, June 29, 2013

OBAMA, MANDELA SIRI NZITO!


MAMBO mawili ndiyo habari ya mjini kwa sasa; umahututi wa Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Rolihlahla Mandela ‘Madiba’ (94) na ziara ya Rais wa Marekani, Barack Husein Obama katika nchi tatu za Afrika.

KUHUSU MANDELA
Habari zimeeleza kuwa baadhi ya wananchi nchini mwake hawaamini kama mzee huyo yu hai pamoja na madaktari wa Hospitali ya Mediclinic Heart iliyopo Pretoria, Sauzi alikolazwa kusisitiza kwamba bado anaishi kwa kupumulia mashine.
Habari kutoka kwa chanzo chetu jijini Pretoria, zimeeleza kuwa wananchi hao wanaamini serikali yao inaficha siri hiyo nzito kutokana na kuogopa kuvuruga ziara ya Obama ambaye jana (Ijumaa) alitarajiwa kutua nchini humo akitokea Senegal ambako alianza ziara yake.
Imedaiwa kwamba serikali ya nchi hiyo inaamini ziara ya Obama ina faida, hivyo kitendo cha kutangaza mtu mkubwa kama Mandela ameondoka duniani itailazimu Ikulu ya Washington itengue ziara hiyo.
Wengi wanaamini baada ya Obama kumaliza ziara yake kesho na kuondoka, mashine inayompa uhai Madiba itazimwa na serikali kutangaza kifo chake.
WENGINE WANAAMINI  SERIKALI INAJIPANGA
Wakati baadhi ya raia wakiamini ziara ya Obama imesababisha serikali kuficha siri ya hatima ya Mandela, wapo wanaoamini sababu si hiyo bali ni wakati wa serikali kujipanga.
Kundi hilo linadai kwamba haiwezekani serikali ya Sauzi itangaze Madiba ametangulia mbele ya haki haraka, lazima iandae mazingira ya kupokea wageni wengi, wakiwemo viongozi kutoka duniani kote watakaokwenda kuhudhuria mazishi yake. Wamesema maandalizi yake ni pamoja na kuimarisha ulinzi na kukiweka kijiji cha Mandela katika hali ya kufikika kirahisi.

ETI ILITOKEA  KWA NYERERE
Wengine wamefikia hatua ya kusema hata katika kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, tarehe iliyotangazwa siyo aliyokufa na kwamba haikutangazwa mapema ili kuipa serikali nafasi ya kujiandaa na ugeni wa viongozi mbalimbali wa dunia. Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999.

OBAMA ATAMUONA KWA SIRI
Hivi karibuni, waratibu wa ziara ya Obama walisema bosi wao huyo hatakwenda hospitalini kumjulia hali Mzee Mandela ingawa atafika kwenye Kisiwa cha Robben lilipo gereza alilofungwa mzee huyo.
Hata hivyo, habari za ndani zinasema Obama atakwenda kumwona Mandela katika mazingira yoyote awe hai au la, lakini kwa siri ili utaratibu wa ziara usivurugwe.

KITENDO CHA ZUMA KUAHIRISHA SAFARI
Hofu zaidi imeongezeka kwa wananchi baada ya rais wa sasa wa nchi hiyo, Jacob Zuma kumtembelea Mzee Madiba hospitalini Jumatano iliyopita na kuwataka watu wamuombee kiongozi huyo ambaye ni nembo ya kupinga ubaguzi wa rangi duniani.
Baada ya kutangaza hali hiyo, Zuma aliahirisha safari yake ya Msumbiji kuhudhuria mkutano uliondaliwa na Jumuiya ya Uchumi Nchi za Kusini mwa Afrika  (SADC), wakiamini ana siri nzito juu ya Mzee Madiba alipokwenda kumwona.

KWA NINI FAMILIA IWEKE KIKAO CHA SIRI NA KWENDA MAKABURINI?
Hivi karibuni familia ya ukoo wa Mandela ilikutana kijijini Qunu katika Jimbo la Eastern Cape kwenye makazi ya mzee huyo na kuweka kikao cha siri kisha kwenda makaburini, jambo ambalo kwa Kabila la Xhosa hufanyika endapo wahusika wanaamini kuna mtu mzito ataaga dunia.
Kitendo hicho kimesababisha wengi waamini kuwa familia hiyo ina siri nzito kuhusu rais huyo mstaafu huku ukiibuka utata wa eneo la kuupumzisha mwili wake.

WACHIMBA KABURI WATINGA MAKABURINI
Juzi, wachimba kaburi walifika kwenye makaburi ya familia ya Mandela wakitaka kuchimba kaburi. Hali hiyo pia imeibua hisia kuwa inawezekana wanajua ukweli juu ya Mzee Madiba.

UCHUMI WA SAUZI BAADA YA MANDELA
Wapo wanaoamini kuwa kama Mandela atafariki dunia, basi uchumi wa nchi hiyo utayumba kwa kuwa wawekezaji wengi walikimbilia Sauzi kwa sababu ya mzee huyo.
Sababu kubwa inayotolewa na wanaoamini hivyo ni kwamba makampuni mengi kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika yataondoka nchini humo kwa kuwa hayatakuwa na imani kwamba Afrika Kusini ni salama kutokana na mtetezi wa amani kuaga dunia. 

OBAMA, MANDELA NA SIRI YA NAMBA 46664
Obama anadaiwa kumkubali Mzee Madiba kutokana na jitihada zake za kisiasa na hata katika kampeni zake za kuingia White House nc
hini Marekani, alikuwa akitumia namba 46664 ambazo zilikuwa za mzee huyo alipokuwa amefungwa gerezani katika Kisiwa cha Robben.
Pia Mzee Madiba amekuwa akizitumia namba hizo katika kampeni ya kupinga Ugonjwa wa Ukimwi baada ya mwanaye Makgatho Mandela kufariki dunia kwa ugonjwa huo mwaka 2005.

OBAMA BONGO
Baada ya kumaliza ziara hiyo nchini humo, Obama anatarajiwa kutua Bongo keshokutwa ambapo atakuwepo kwa siku mbili hivyo kwa sasa Jiji la Dar ni hekaheka tupu.

No comments: